WIZARA YA AFYA YAWATAKA MAAFISA USTAWI KUZUIA UKATIRI DHIDI YA WATOTO.

 

Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii, Dk. John Jingu akizungmza na Maafisa Maendeleo ya Jamii pamoja na Ustawi wa Jamii wa Mkoa wa Songwe katika kikao kazi cha kujadili changamoto walizonazo, kilichofanyika Mkoani hapo.

Na Mwandishi wetu KTPC,Songwe.

Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. John Jingu amewataka Maafisa Ustawi na Maendeleo ya Jamii nchini kuhakikisha wanakuwa wabunifu ili Jamii itambue umuhimu wa majukumu yao.

Akizungumza na Maafisa wa Mkoa wa Songwe katika kikao kazi chenye lengo la kujadili changamoto wanazokutana nazo, Dkt. Jingu amesema Maafisa hao wana jukumu kubwa la kutatua  migogoro ya familia pamoja na kubadili fikra na mila potofu zinazochangia ukatili hususani kwa watoto

Jingu amesisitiza kuwa, Maafisa Ustawi na Maendeleo ya Jamii wahakikishe wanatumia ujuzi, weledi na utaalamu wao hasa katika kulinda na kutetea maslahi ya watoto.

“Chanzo kikubwa cha ukatili dhidi ya watoto ni migogoro katika familia, lazima sisi kama wataalamu katika jamii, tuone namna gani tunaweza tukaboresha mifumo ya utatuzi wa migogoro ya familia ili watoto wetu wakue vizuri na waweze kulindwa dhidi ya ukatili wa aina yoyote,” amesema Jingu. 

Ameongeza pia Maafisa Maendeleo ya Jamii ni wataalamu wa kushughulikia na kubadilisha Jamii kwenye fikra, mila na desturi zinazoendeleza ukatili huku Maafisa Ustawi katika eneo hilo wana jukumu la kutatua migogoro na kuhakikisha haki inatendeka, ndiyo sababu wanatakiwa kuwepo wakati wa kusikiliza kesi za watoto.

Kwa upande wake Katibu Tawala Mkoa wa Songwe, Dk. Seif Shekalaghe akimkaribisha Dkt. Jingu kuzungumza na Maafisa hao amemshukuru kwa uamuzi huo kwani utawasaidia kutekeleza majukumu yao kwa weledi.

Baadhi ya Maafisa wakimueleza Katibu Mkuu jinsi wanavyohakikisha wanapunguza tatizo la ukatili wamesema wanashirikiana na wadau mbalimbali kama vile viongozi wa Dini ambapo hivi sasa matukio ya ukatili yamepungua.

“Elimu zimeendelea kutolewa kuanzia ngazi ya chini hususani Viongozi wa Dini na Viongozi wa mila ili wakawaelimishe wananchi katika maeneo yao,” amesema Mariam Daniel, Afisa Maendeleo ya Jamii, Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi.

Aidha, Ritha Kamenya na Daud Mdaki wamesema kikao na Katibu Mkuu kimekuwa na manufaa kwao kwani kimewapa nguvu ya kuendelea kufanya kazi kwa juhudi zaidi.

Search This Blog

CHAGUA HABARI

Pages