Na Walter Mguluchuma, Katavi
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU )Mkoa wa Katavi imefanikiwa kuokoa kiasi cha zaidi ya shilingi milioni 34 na ng`ombe 6 kupitia kazi walizofanya za uzuiaji wa Rushwa kati ya fedha hizo Tsh 28,258,040.00 zimeokolewa Halmashauri ya Mlele ikiwa ni fedha zilizofanyiwa ubadilifu na na baadhi ya watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mlele .
Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Katavi Sipha Mwanjala wakati akitowa taarifa mbele ya vyombo vya Habari juu ya utendaji kazi wa Taasisi hiyo kwa kipindi cha miezi mitatu ya kuanzia Januari hadi Machi .
Mwanjala amesema wameweza kusaidia kuokoa kiasi cha tsh 34,851,040 pamoja na Ng`ombe 6 kupitia kazi ya uzuiaji wa Rushwa na uchunguzi hali iliyofanya kuongezeka kwa mapato katika Halmashauri ya Wilaya ya Mlele
Amefanua kuwa sh ,28,258,040.00 zimerejeshwa katika akaunti ya Halmashauri ya Wilaya ya Mlele ikiwa ni fedha ambazo zilifanyiwa ubadilifu na baadhi ya watumishi waliokusanya ushuru kupitia mashine za POS na baada ya kuzikusanya fedha hizo hawakuziwakilisha benki kama ambavyo inatakiwa .
Ng`ombe 6 pamoja na sh 1,700,000 zimerejeshwa kwa kwa mwananchi ambae alikuwa amezitowa kama faini baada ya kusingiziwa kesi ya mauaji na Askari Polisi aliyeshirikiana na wananchi wawili pia sh 3,184,000 zimerejeshwa katika kitongoji cha Mbongwe Wilaya ya Tanganyika kufatia baadhi ya viongozi na Sungusungu kugawana fedha za kutoka kwa wananchi walizochanga za ujenzi wa shule ya Msingi.
Kuhusu ufatilaji wa miradi ya maendeleo Takukuru Mkoa wa Katavi imeweza kufatilia miradi ya Maendeleo 22 yenye thamani kiasi cha shilingi Bilioni 14.8 kwenye sekta za Elimu ,Afya, uchumi , na miundombinu ili kuweza kubaini viashiria vinavyoweza kusababisha upotevu wa rasilimali za umma .
Mwanjala amesema katika kipindi hicho wamepokea malalamiko 64 yliyohusiana na tuhuma za Rushwa na uchunguzi ulifanyika na kubaini malalamiko 26 hayakuwa yanahusiana na tuhuma za Rushwa hivyo walalamikaji walisaidiwa na kushauriwa sehemu sahihi za kupeleka malalamiko yao

