Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Brigadia Jenerali Wilbert Ibuge, |
Na Muhidin Amri KTPC,Tunduru
MKUU wa mkoa wa Ruvuma Brigadia Jenerali Wilbert Ibuge, ameagiza wataalam wa Halmashauri ya wilaya Tunduru ambao wamesababisha Halmashauri hiyo kupata hati yenye mashaka kutokana na hoja za mkaguzi na mdhibiti mkuu wa hesabu za Serikali(CAG) wachukuliwe hatua.Brigadia Jenerali Ibuge ametoa agizo hilo jana kwenye kikao cha baraza la madiwani la Halmashauri hiyo, kilichokaa kwa ajili ya kujadili hoja zilizotolewa na mkaguzi na mdhibiti wa hesabu za Serikali kwa mwaka wa fedha 2019/2020.
Amesema, hoja zilizotolewa na CAG katika Halmashauri hiyo zimetokana na uzembe kwa baadhi ya wataalam wake kwa kutofuata sheria na kanuni za ukusanyaji mapato na matumizi ya fedha zinazopatikana kutoka kwenye vyanzo vyake vya ndani.
“kwa hoja zilizotolewa na mkaguzi na mdhibiti mkuu wa hesabu za Serikali katika Halmashauri yenu kwa kiasi kikubwa zimetokana na uzembe wa watumishi, na hoja hizo zimekuwa zinajirudia mwaka hadi mwaka kwa hiyo dhahiri watumishi hawataki kujifunza na kujirekebisha, badala yake wanafanya kazi kwa mazoea”amesema.
Mkuu wa mkoa amesisitiza kuwa,ni lazima watumishi hao wawajibike na kuchukuliwa hatua ili iwe fundisho kwa watumishi wengine wanaoshindwa kutekeleza wajibu wao na kusababisha upotevu wa mapato na kuwepo kwa hoja za mkaguzi na mdhibiti mkuu wa hesabu za Serikali.
Amesema, katika matokea ya ukaguzi wa hesabu kwa mwaka wa fedha ulioisha tarehe 30 Juni 2020 Halmashauri hiyo imefanya vibaya tofauti na miaka ya nyuma ambapo kwa miaka mitano kuanzia mwaka 2014/2015 hadi 2018/2019 imepata hati safi.
Amesema, kupata hati yenye mashaka inatokana na sababu mbalimbali ikiwemo kutofanyika kwa marekebisho ya hati za madai yaliyofanyika kwenye mfumo wa ukusanyaji wa mapato bila ya kuwa na nyaraka toshelezi ambayo ni shilingi 1,232,598,827.
Alitaja sababu nyingine iliyosababisha Halmashauri kupata hati yenye mashaka ni kuwepo kwa maelezo yasiojitosheleza kuhusiana na madai yaliyopoteza zaidi ya shilingi 24,296,173.
Amesema, Halmashauri ya Tunduru kupata hati yenye mashaka siyo jambo jema hasa kwa Halmashauri yenye sifa ya kufanya vizuri katika suala zima la maendeleo na kuagiza kila mmoja ahakikishe anawajibika ili Halmashauri hiyo iendelee kupata hati safi kama ambavyo imekuwa kwa miaka ya nyuma.
Hata hivyo, amewapongeza kwa namna wanavyoifanyia kazi taarifa ya mdhibiti na mkaguzi mkuu wa Hesabu za Serikali ambapo katika utekelezaji wa hoja na mapendekezo yaliyotolewa kwenye taarifa ya CAG Halmashauri imefanikiwa kufunga hoja 98 kati ya 108 za miaka ya nyuma hivyo kusalia hoja 8 kwa hesabu jumuishi.