Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Katavi akipokea cheti kutambua mchango wake katika kuhabarisha umma kuhusu Afya ya uzazi |
Imekuwa
ni jambo la kawaida kwa wazazi na walezi kukwepa kuwaelimisha watoto
wanaokaribia umri wa kupevuka au kubalehe kuhusu afya ya uzazi. Hulka hii
imetokana na dhana potofu ambayo imejengeka miongoni mwa jamii kuwa
kuwaelimisha watoto/vijana kuhusu afya ya uzazi ni sawa na kuwahasisha kufanya
ngono.
Kutokana na wazazi/walezi wengi ama kuona aibu au kushindwa kabisa kuwaelimisha watoto na vijana wao kuhusu afya ya uzazi, kumekuwapo na ongezeko kubwa la vijana wenye uelewa finyu kuhusu afya ya uzazi katika jamii.
Hayo yamebainishwa na Bi. Elida Machungwa Mratibu wa Huduma za Afya ya Uzazi na Mtoto Mkoa wa Katavi, wakati wa mdahalo unaohusu Afya ya Uzazi na Ukatili wa Kijinsia uliofanyika katika ukumbi mdogo wa Polisi klabu na kuhudhuliwa na viongozi wa dini, wazazi, vijana, viongozi wa kimila na waandishi wa Habari.
Bi. Elida amebainisha kuwa tatizo la mimba za utotoni Mkoani bado ni changamoto ambayo inahitaji juhudi za pamoja kati ya Serikali, wananchi na wadau wa maendeleo kuendelea kutoa elimu kwa jamii ili ziweze kubadili mitazamo hasi hasa ambayo inahusiana moja kwa moja na ukatili wa kijinsia ambayo kwa sehemu kubwa inawagandamiza watoto wa kike
Amesema kuwa wakati sasa umefika kupinga kwa nguvu zote mimba za utotoni na ndoa za utotoni kwani waaathirika wakubwa na wasichana ambao wengi wao wanakatishwa masomo na kukosa fursa za kiuchumi kwa ajili ya maendeleo yao na mapambano haya lazima yaende sambamba na elimu ya Afya ya uzazi kwa vijana kwani elimu hii ikitolewa kwa vijana wote mijini na vijijini itasaidia sana vijana kufahamu nini wanatakiwa kufanya na nini hawatakiwi katika rika lao.
Naye Afisa Vijana wa Manispaa ya Mpanda Bi. Rozina Ngonyani amewaambia washirikiki wa mdahalo huo kuwa Ili kuwawezesha wanafunzi na Vijana kujielimisha mambo mbalimbali kuhusu afya ya uzazi Serikali kwa kushirikiana na wadau wanaofanya kazi katika Mkoa wa Katavi utaendelea kuandaa midahalo mbalimbali kwa kupitia klabu zilizoanzishwa katika shule za sekondari na kwa vijana walio nje ya mfumo wa elimu ili kuhakikisha kuwa vijana wote wanakuwa na uelewa wa kutosha kuhusu Afya ya uzazi na kupinga ukatili wa kijinsia na mimba za utotoni katika maeneo yao.
Katika
mdahalo huo vijana hao waliiasa jamii kuacha kuwadanganya watoto pindi
wanapohitaji taarifa na eimu kuhusu afya ya uzazi, kwani wao kutokuwa na
uelewa mzuri kuhusu afya ya uzazi ni tatizo ambalo haliitaji kulifumbia macho,
kwani wazazi/walezi wakificha mambo haya wakadhani ni dhambi basi kupitia
vijiwe tunavyokaa tutaendelea kupata elimu isiyo sahihi, hivyo muda wa wazazi
kuzungumza na vijana kuhusu Afya ya uzazi ni sasa. Wamesema katika vijiwe
wanavyokaa kumekuwa na tafsiri mbalimbali kuhusu mwanaume halisi ni nani? Mmoja
wa vijana hao amesema kuwa wao wanafahamu mwanaume halisi ni yule anayechelewa
kurudi nyumbani, shupavu, mwenye watoto wengi na michepuko, hivyo amesema dhana
hizi ambazo siyo sahihi ni lazima zitolewe vichwani mwa watu kwa kutoa elimu ya
Afya ya uzazi na ukatili wa Kijinsia.
Naye Mwenyekiti wa Chama cha Waandishiwa wa Habari Mkoa wa Katavi Bw.Walter Mguluchuma, anasema ili kukabiliana na hatari ya mimba za utotoni na ukatili wa kijinsia, kuna umuhimu kwa jamii na wazazi kwa ujumla kuweka ulinzi kwa watoto wa jinsia zote mbili pasipo kujali msichana au ni mvulana. Pia, wazazi wawe wazi kwa watoto wao bila kificho kuwafundisha kuhusu Afya ya uzazi kwani ni jambo ambalo hata kama wazazi/walezi hawata zungumza na watoto basi watoto wanaweza kuwa na uelewa mdogo kuhusu afya ya uzazi hivyo kuleta madhara makubwa katika jamii.
“Nasema hivyo kwa sababu tunaona siku hizi watoto wetu wa kike wanapata elimu zisizo sahihi kuhusu uzazi wa mpango hivyo kuwa na mitazamo hasi, hivyo sisi kama wazazi na wataalamu toka Idara ya Afya na wadau wa maendeleo Mkoani Katavi lazima tuwafikie vijana, lazima tuzungumze nao na hii itasaidia kupunguza mimba za utotoni, maambukizi ya VVU na magonjwa mengine ya hatari kwa vijana.
Akifunga
mdahalo huo Bi. Elida Machungwa kwa niaba ya Mganga Mkuu wa Mkoa amesema kuwa
ni vema sasa jamii kuwa na mkakati wa kuwasaidia vijana waliopo kwenye mfumo wa
shule na waliopo nje ya mashule, kupitia kwa walimu na maafisa maendeleo ya Jamii
ngazi ya Kata kwa kushirikiana na wataalamu wa Afya katika maeneo yao kuhamasisha
mijadala mbalimbali kuhusu Afya ya uzazi ili vijana wajitambue na kuwa na
uelewa sahihi kukusu Afya ya uzazi hii itajenga morali hata kwa wazazi/walezi kutambua
wajibu wao ambao mbali ya kuwapatia vijana mahitaji muhimu, pia suala la afya
ya uzazi kwao ni muhimu katika ulimwengu wa sasa.