Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mji wa Mbinga Mkoa wa Ruvuma,Grace Ouintine.
Na Mwandishi Wetu-KTPC.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Mbinga kwa usimamizi mzuri wa miradi hii... Huyu mama timu yake ni ya wanaume watupu, lakini ameweza kuwasimamia... Mpigieni makofi huyu mama kumbe akina mama mnaweza…”

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Mbinga kwa usimamizi mzuri wa miradi hii... Huyu mama timu yake ni ya wanaume watupu, lakini ameweza kuwasimamia... Mpigieni makofi huyu mama kumbe akina mama mnaweza…”
Ndivyo alivyosema hivi karibuni Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwa katika ziara wilayani Mbinga Mkoani Ruvuma na kulazimika kumpongeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Mbinga, Grace Quintine, kwa usimamizi mzuri wa miradi ya maendeleo hususani ujenzi wa nyumba saba za watumishi, ujenzi wa nyumba ya makazi ya mkurugenzi pamoja na ujenzi wa jengo la utawala katika halmashauri hiyo.
Katika ziara hiyo, Waziri Mkuu alisema chini ya usimamizi wa mkurugenzi huyo, majengo yote hayo, yamejengwa kwa viwango vinavyotakiwa na yanavutia.
Kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali, mkurugenzi huyo amekuwa mbunifu na makini katika matumizi ya fedha za umma kwa kutumia mfumo wa P4R yaani, kulipa kwa kadiri ya matokeo na kiwango cha kazi iliyofanyika.
Vyanzo hivyo vinasema Mkurugenzi huyo amekuwa imara katika kusimamia matumizi ya fedha katika miradi mbalimbali na kwa kutumia mfumo wa P4R, fedha inayobaki katika mradi baada ya kuzingatia ubora na ukubwa unaotakiwa, huipeleka kukamilisha mradi mwingine wenye upungufu au kuanzisha mwingine hali iliyoongeza tija kimaendeleo katika Halmashautri ya Mji wa Mbinga.
Kwa mujibu wa vyanzo hivyo, moja ya mambo ambayo ni ubunifu wa mkurugenzi huyo, ni kuagiza na kununua kiwandani vifaa vingi vya ujenzi, badala ya kununua katika maduka ya wafanyabiashara kwa bei ya juu hali inayowezesha kuokoa fedha nyingi za umma.
Miongoni mwa vifaa vya ujenzi ambavyo halmashauri chini ya usimamizi wake huvinunua kiwandani na kuokoa fedha nyingi ni pamoja na saruji, marumaru, rangi na jasi.
Uchunguzi unaonesha kwamba miradi mikubwa inayomnyanyua Grace ni kujikita kwake katika mfumo wa P4R.
Mwezi Mei Mwaka 2020 Serikali ilitoa Sh milioni 87.5 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa saba ya shule za msingi katika Halmashauri ya Mji wa Mbinga, naye akaongeza Sh milioni 29 kutoka fedha za mapato ya ndani ya halmashauri hiyo.
Imebainika kuwa, hali hiyo ndiyo pia ilifanikisha ujenzi wa madarasa 14 na ofisi saba kwa kutumia fedha hizo tena kwa ubora wa hali ya juu kwa Sh milioni 116.5, jambo ambalo ni nadra kwa halmashauri nyingi.
Grace ambaye ni msomi mwenye Shahada ya Uzamili katika Utawala wa Serikali za Mitaa, anasema aliteuliwa kushika wadhifa huo miaka miwili iliyopita akitokea katika Halmashauri ya Mbulu alipokuwa akifanya kazi kama ofisa utamaduni.
Anasema: “Kwa kweli sikuwahi kuwaza kuwa mkurugenzi, ndoto yangu kubwa ilikuwa ni kuwa mbunge wa viti maalum katika Mkoa wa Manyara, lakini wakati najiandaa kwenda kugombea, nikapata uteuzi hivyo, sikutaka tena kwenda kugombea; nimetosheka na hiki cheo changu na sasa nina wajibu wa kutumikia wananchi kwa kuwaletea maendeleo kwa vitendo.”
Anasema, ujasiri, kujiamini na kumtanguliza Mungu kwa kila jambo, ndio mambo na nguzo pekee anazojivunia kwa kuwa anaamini hakuna kisichowezekana kwani hata mambo magumu yanawezekana bila kujali jinsia ya mtu.
“Wote tumeteuliwa tufanye kazi kwa juhudi, maarifa na uadilifu na hivyo, nitazidi kufanya ubunifu na uadilifu ili nionesha kwa vitendo maana halisi ya maendeleo katika Halmashauri ya Mji wa Mbinga ninayoitumikia kwa kuhakikisha kila fedha ya serikali (umma) inatumika kwa teja na thamani yake inaonekana,” anasema Grace.
Mkurugenzi huyo anasema halmashauri yake imefanikiwa kuongeza ukusanyaji wa mapato ya ndani kutoka Sh milioni 800 mwaka 2019 hadi kufikia Sh bilioni 1.2 mwaka 2020.
“Aidha, tumefanikiwa kununua magari mawili katika kipindi cha miaka miwili kwa kutumia fedha za mapato ya ndani; gari moja ni la mkurugenzi na lingine linatumika kufuatilia ukusanyaji wa mapato, lakini hata hivyo, hatuwezi kubweteka kwani tunahitaji kufanya vizuri zaidi ya hapo,” anasema Grace.
Mintarafu namna anavyopunguza gharama na matumizi ya halmashauri yake katika miradi mbalimbali na salio kutumika kwa miradi mingine ya maendeleo, mkurugenzi huyo anatoa mfano akisema kuwa, katika mradi wa boma la mkurugenzi ambalo ni jengo la ghorofa ilitakiwa kujengwa kwa Sh milioni 300.
“Tulisimamia na kujibana kwa kuagiza vifaa vyote kiwandani na kukafanikiwa kubaki na ‘chenji,’ anasema na kuongeza: “Kimsingi zimetumika Sh milioni 251 na fedha zilizobakia, zimetumika kujenga uzio kwenye nyumba ya mkurugenzi, kuweka taa na kujenga choo cha nje.”
Anasema: “Katika mradi wa nyumba mpya saba za wakuu wa idara, halmashauri tulitenga Sh milioni 50; tulijibana na kutumia Sh milioni 45.9 kujenga nyumba hizo ambazo zimeondoa changamoto ya uhaba wa nyumba za watumishi.”
Kwa mujibu wa mkurugenzi huyo, kupitia mapato ya ndani wameweza kulipa deni la posho za madiwani la miezi minane alilolikuta na kwa kushirikiana na watendaji wengine katika halmashauri hiyo wakiwamo madiwani, wamejenga shule nne za sekondari na kuzisajili.
Aidha, wamefanikiwa kujenga shule tatu za msingi na zahanati 11. Kati ya hizo, zahanati tatu zimekamilika n anyingine zipo katika hatua mbalimbali za ujenzi.
Mkurugenzi Grace anasema miongoni mwa changamoto anazokutana nazo ni pamoja na utayari duni wa baadhi ya wananchi katika kupokea miradi kama yao kwani wengine wanaiona miradi hiyo kama mali ya serikali, kumbe ni yao kwani inatokana nafedha zao zinazoatikana kupitia kodi, tozo, rasilimali na kazi mbalimbali wanazofanya hivyo, wanapaswa kuilinda, kuitunza na kuiendeleza.
“Changamoto nyingine ni baadhi ya watumishi kutojituma, hivyo kuhitaji kufuatiliwa muda wote… Tabia hii inarudisha nyuma utendaji kazi, lakini nashukuru kwa sasa wengi ‘tunaimba wimbo mmoja’ wa maendeleo,” anasema Grace.
Anashauri jamii iendelee kujenga imani kwa wanawake na kuwekeza kwao kwani ni waaminifu, wafuatiliaji makini na wana uwezo mkubwa wa kusimamia miradi mikubwa, kukoa fedha na nguvu nyingi za umma na kuongoza kuanzia ngazi za familia, taasisi hadi serikalini.
Anasema: “Watu wanasema nimefanya vizuri kwenye miradi, lakini hii yote inatokana na timu nzuri niliyo nayo kati ya wakuu wa idara, watumishi na madiwani ambao wamekuwa wakinisaidia kutekeleza miradi hiyo na kwa kushirikiana na wananchi, tumeweza kutekeleza Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).”
Grace anasema anamshukuru Rais John Magufuri kwa kumteua huku Rais Samia Suluhu Hassan akiendelea kumwamini.
“Sitamuangusha Rais John Magufuli kwa kuiniamini na kuniteua na pia, katu sitamwangusha Rais wetu wa sasa, Mheshimiwa Mama Samia kwa kuendelea kuniamini na wananchi wa Halmashauri ya Mji wa Mbinga; kwa hili, naahidi sitawaangusha,” anasema.
Anabinisha siri ya mafanikio yake katika kipindi kifupi cha kuitumikia Halmashauri ya Mji wa Mbinga kuanzia mwaka 2018 hadi sasa kuwa ni pamoja na kujituma, umoja, upendo, ushirikishwaji, uaminifu na uwajibikaji wa wakuu wa idara, madiwani pamoja na watumishi wengine.
Anasema: “Nimekuwa nikifuatilia kila kitu na nina ‘teamwork’ nzuri niliyoiunda inayonisaidia katika kila shuguli za maendeleo; ninaenda ‘field’ na kurudi ofisini mimi… Kimsingi, katika suala la maendeleo sina mchezo; nafuatilia kila kitu.”
“Unajua ukitaka shuguli za maendeleo zifanikiwe, washirikishe wote, kuwa mkweli na muwazi, watu watakupenda na watakusaidia; ukijifanya unajua kila kitu, watakususia na hautafanikiwa… Mimi naamini katika uwazi, ukweli na ushirikishwaji na hii imesaidia sana kujenga imani ya kufanya kazi kwa watumishi wenzangu,” anasema.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Mbinga, Kelvin Mapunda, anasema hakuamini kuwa mkurugenzi huyo ana uwezo mkubwa wa kiungozi kiasi cha kuhakikisha fedha zote za umma zinatumika kwa thamani halisi.
“Grace ni mkurugenzi mwenye uwezo mkubwa; anawazidi hata wanaume kwa utendaji wake na kinachovutia zaidi ni kwamba, ni mtu anayeshaurika hata katika masuala ya fedha, lakini yuko makini sana,” anasema Mapunda.
Anasema madiwani na wakuu wa idara wanamuunga mkono na kushirikiana naye kujenga halmashauri hiyo.
“Ni kiongozi wa tofauti sana; ana upendo wa dhati na hii halmashauri ndio maana katika kipindi kifupi alichokaa hapa, amefanya maendeleo makubwa na amesimamia vizuri miradi yetu na kubakisha fedha,” anasema.
Anaongeza: “Tunaomba aendelee kuchochea maendeleo ili kupeleka halmashauri yetu kwenye hadhi ya juu kabisa kimaendeleo…”
Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Ruvuma Oddo Mwisho, anasema Grace (Mkurugenzi) ni mwanamke kiongozi wa kipekee ambaye mapenzi yake kwa wananchi hayafichiki na yanagusa hisia za wanawake na wanaume; wazee kwa vijana; wadogo kwa wakubwa; maskini kwa tajiri; wasomi kwa wasiosoma mradi tu, ni kiongozi anayepigania ustawi kwa watu wake wote.
Gideon Ipyana mkazi wa Mbinga na mdau wa maendeleo anasema, awali alipomuona Grace akiapa baada ya kuteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Mbinga, alikata tamaa na kujihoji moyoni kuwa kwanini wamepelekewa mkurugenzi mwanamke.
Anasema: “Lakini baada ya kuanza kufatilia miradi na kufanikiwa, ninatamani Grace asihamishwe kwani ana uwezo mkubwa wa kusimamia maendeleo na amefanikiwa sana hata kuwazidi wanaume.”
Anawapongeza madiwani kwa kuungana na mkurugenzi huyo katika usimamizi na utekelezaji wa miradi ya maendeleo badala ya migogoro isiyo na tija.