Katavi.
Mkazi wa kata ya Ilunde Tarafa ya Inyonga Wilaya ya Mlele Mkoa wa Katavi Seda Mbutula(47) anashikiliwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Katavi akiwa na nyara za serikalli katika pori la akiba Rungwa.
Nyara hizo ni mafuta ya Simba,ngozi ya kakakuona,ngozi ya paka pori,ngozi ya simba,vipande vinne vya meno ya ngiri na mkia wa nyumbu akiwa amehifadhi kwenye mfuko wa salfleti na kuficha nyumbani kwake.
Akiongea na waandishi wa habari ofisini kwake Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi ACP Ali Makame Hamad alisema mnamo Novemba 23 mwaka huu majira ya saa Tisa alasiri katika pori la akiba Rungwa lililopo kata ya Ilunde Wilaya ya Mlele Kikosi Cha jeshi la Polisi Mkoa wa Katavi kilimkamata mtuhumiwa Seda Mbutula akiwa na nyara hizo.
Hivyo mtuhumiwa bado anashikiliwa na Jeshi la Polisi na atafikishwa mahakamani kwa hatua zaidi za kisheria.
Katika hatua nyingine,Kamanda Hamad aliwasisitiza wananchi wote wa Mkoa wa Katavi wanaomiliki silaha kinyume na Sheria kuendelea kuzisalimisha silaha hizo kwa kipindi hiki Cha msamaha uliotolewa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mh.George Simbachawene.
"Kwa wale wote watakao zisalimisha silaha zao ndani ya muda uliotolewa watapewa msamaha wa kutoshtakiwa hivyo wazisalimishe kwenye vituo vya Polisi,ofisi za serikali za mitaa na ofisi za watendaji Kata"Alisisitiza Kamanda Hamad
Hivyo alisema kwa muda uliobaki Viongozi wa serikali za mitaa na watendaji wa kata kuendelea kutoa ushirikiano katika kufanikisha zoezi hilo.
Aidha baada ya muda uliotolewa kumalizika Jeshi la Polisi Mkoa wa Katavi litaendesha oparesheni ya kuwasaka wale wote waliokaidi kusalimisha silaha zao kwa kuwachukulia hatua kali za kisheria pamoja na kuwafikisha mahakamani.
Kamanda Hamad anawataka wananchi wote Mkoa wa Katavi kuendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa za kihalifu na wahalifu ili kuendelea kuuwela Mkoa katika Hali ya usalama.