| Mkurugenzi wa Hospitali Teule ya Rufaa Mkoa wa Katavi Dr Yustina Tizeba |
Na Walter Mguluchuma
Katavi
Msongamano wa idadi ya wajawazito wanaojifungulia katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Katavi imepungua kutoka wajawazito 600 hadi kufikia wajawazito 180 kwa mwezi baada ya kuongezeka kwa vituo vya afya katika Halmashauri zote za Mkoa wa Katavi .
Hayo yameelezwa na Mkurugenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Katavi Dkt Yustina Tizeba wakati alipokuwa akiongea na wandishi wa habari katika utoaji wa huduma bure za magonjwa mbalimbali ikiwemo huduma ya kinywa na meno,macho, presha,sukari kuelekea miaka 60 ya uhuru wa Tanzania .
Amesema Hospitali hiyo ilikuwa na msongamano wa wajawazito waliokuwa wanakwenda kujifungulia kwenye hospitali hiyo na wengine kufanyiwa upasuaji kufuatia hapo awali kuwa na vituo vichache vya afya vilivyokuwa vikitowa huduma ya upasuaji .
Amefafanua kuwa kwa mwezi walikuwa wakipokea wajawazito mia sita waliokuwa wakijifungulia hapo lakini kwa sasa idadi hiyo imepungua kwa kiasi kikubwa ambapo wanapokea wajawazito 180 hadi mia mbili kwa mwezi .
Dkt Tizeba amebainisha kuwa msongamano wa wajawazito kujifungulia hospitalini hapo umepungua baada ya kujengwa kwa vituo vya afya nane na Hospitali za Halmashauri zinazo toa huduma ya upasuaji .
Alisema kuwa idadi ya wataalamu wa afya imeongezeka hali ambayo imefanya huduma kuzidi kuboreka zaidi ambapo hata idadi ya wagonjwa wanaopewa rufaa kwenda Hospitali za Kanda imezidi kupungua imebaki kwa yale magonjwa makubwa kama upasuaji wa kichwa .
Hata hivyo Dkt Tizeba alieleza kuwa bado hospitali hiyo Teule ya Rufaa Mkoa wa Katavi imeendelea kupokea wagonjwa wanaotoka kwenye maeneo mbalimbali ya Mkoa huo kutokana na baadhi ya huduma kutopatikana kwenye maeneo yao hali inayopelekea kufika katika Hospital hiyo ilikupatiwa huduma.
Aliwaasa wakazi wa Mkoa wa Katavi kujitokeza kwa wingi kipindi hiki cha maadhimisho ya miaka 60 ya uhuru kwa ajili ya kupata huduma bure za matibabu yanayotolewa kwenye Hospitali Teule ya Rufaa ya Mkoa wa Katavi .
Alizitaja baadhi ya huduma zinazotolewa bure ni upimaji wa presha ,sukari,uzito,matibabu ya kinywa na meno,macho pamoja na kupatiwa ushauri .
Nae Mkazi wa Manispaa ya Mpanda Fransis Watosha amebainisha kuwa huduma zinazotolewa kwenye hospitali hiyo zinatolewa vizuri hivyo aliomba Serikali iongeze dawa .
Nae Benadeta Ulaya amesema kuwa yeye ni miongoni mwa wananchi waliopatiwa huduma bure ya macho hivyo ameomba huduma iwe ina tolewa mara kwa mara.