Katavi
Elimu ya lishe na uhamasishaji kwa jamii kuhusu huduma za lishe Bora zinazotakiwa kwa watoto wadogo katika malezi na makuzi inahitajika lengo ikiwa ni kuondoa tatizo la udumavu.
Uelewa mdogo wa lishe nao unachangia kwa Wazazi kutojua namna sahihi ya ulaji kwa watoto unaofaa ikiwa ni pamoja na kukosa lishe mchanganyiko na bora kwa kila kaya kutokana na kipato kidogo katika familia.
Afisa lishe Mkoa wa Katavi Asnath Mrema anaeleza kuwa kula kwa mazoea nako kunachangia mtoto kupata udumavu kutoka na mtoto kukaririshwa kula vyakula vya aina moja bila kuwa na mchanganyiko wa virutubishi vya lazima Kama kalori,protini,mafuta,wanga, vitamini na madini.
Pia mila na desturi potofu nayo imeonekana kuwa sababu ya watoto kuwa na udumavu kwa kutopewa baadhi ya vyakula Kama mayai,nyama,samaki Wazazi wakihofia vyakula hivyo kuwaletea watoto wao madhara.
"Kuna baadhi ya wazazi wanawanyima watoto wao mayai eti wakila nywele hazitaota au wakila samaki hawatakuwa na akili huo ni upotoshaji,hivyo niwasihi Wazazi kuwapatia watoto wao vyakula vyenye virutubisho hasa katika umri mdogo kadri wanavyoendelea kukuwa" alisema Mrema
Mhudumu wa Afya Hakia Mvungi katika kituo Cha Afya Mwangaza anayewahudumua akina mama wajawazito kliniki anasema kukosa chakula cha kutosha na mtoto kukaa na njaa ya muda mrefu au kushiba bila kujali uwiano wa virutubishi ndani ya chakula nayo ni sababu mojawapo ya mtoto kupata utapiamlo
Aidha aliongeza kuwa udumavu huweza kutokea kati ya siku moja tangu kutungwa mimba hadi siku 1000 hivyo mama mjamzito anatakiwa kupata lishe bora Ili kuweza kurutubisha afya ya mwili wake na kiumbe aliyeko tumboni.
Nae Asia Mbwana mhudumu wa kliniki katika kituo Cha Afya Amec kilichopo mtaa wa madukani Manispaa ya Mpanda aliitaka jamii kuboresha namna ya ulishaji wa Watoto wachanga na wadogo na kushauri pia kunyonyesha kunapunguza viwango vya utapiamlo na vifo kwa watoto.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Mkoa wa Katavi Dr.Omar Sukari aliongeza kuwa maradhi ya kuambukiza Kama homa ya matumbo,nimonia,malaria huongeza mahitaji ya lishe hivyo endapo mtoto atakosa huishia kupata utapiamlo.
Pia Dr Sukari alishauri Elimu ya lishe kutolewa kwa jamii kupitia vyombo vya habari vya ndani ya Mkoa na hata nje ya Mkoa, mikutano ya hadhara pamoja na vituo vya kutolea huduma za Afya.
Taasisi mbalimbali pamoja na mashuleni nako wanatakiwa kupatiwa Elimu ya lishe Ili kuboresha lishe za watoto wetu wawapo mashuleni.