Na Walter Mguluchuma
Katavi
Nyumba kumi katika Kijiji cha Igongwe Kata ya Sitalike Wilaya ya Mpanda Mkoa wa Katavi zimechomwa moto na kuteketea pamoja na kuharibu mali zilikuwemo ndani ya nyumba hizo ikiwemo chakula.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi Sylvester Ibrahimu alisema nyumba hizo kumi zilikuwa zikimilikiwa na Sayi Wema na Nyamizi Luhemela wakazi wa Kijiji cha Igongwe.
Ameeleza kuwa thamani ya mali hizo zilizoteketea kwa moto ikiweo mahindi na mpunga bado hazijafahamika ambapo katika tukio hili watuhumiwa nane wamekamatwa kuhusika na tukio hili .
Ambao amewataja kuwa ni Daud Gembe , Abasi John, Ginius Sindani , Julius Nicholaus, Godfrey Basili( MASAGA), Joseph Lepard, Kilisen Mwananjela wote wakazi wa Kijiji cha Sitalike na Japhari Razaro mkazi wa Kijiji cha Vikonge Wilaya ya Tanganyika .
Kamanda Ibrahimu alisema katika tukio hilo mtuhumiwa mmoja aitwaye Vicenti Mwananjela amefariki dunia wakati alipokuwa akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Katavi kutokana na wananchi kujichukulia sheria mikononi kwa kumshambulia kwa kumpiga baada ya kuhusika kwenye tukio hilo la kuchoma nyumba moto .
Alisema watuhumiwa hao wanaendelea kushikiliwa na Jeshi la Polisi kuhusiana na tukio hilo la kuchoma nyumba hizo moto na upelelezi utakapokamilika watafikishwa Mahakamani .
Kaimu Kamanda amesema Jeshi hilo pia limewakamata watu saba wanaodaiwa kujichukulia sheria kwa kumpiga hadi kumuuwa mtuhumiwa Klisent Mwananjela aliyekuwa anatuhumiwa na watuhumiwa wengine saba kwenye tukio la kuchoma nyumba hizo kumi Moto.