WAKAZI WA KATA 5 HALMASHAURI YA MPIMBWE MKOA WA KATAVI KUONDOKANA NA ADHA YA KUVUKA MAJI

 

Daraja la muda la watembea kwa miguu lililopo katika Mto Msadya ambalo lilijengwa mwaka 2020 kwa maelekezo ya Mtendaji Mkuu wa TARURA baada ya kuona taabu na usumbufu waliokuwa wanaupata wananchi katika eneo hilo wakati wa kuvuka kutoka kata moja kwenda kata nyingine.

Katavi

Wakazi wa kata 5 katika Halmashauri ya Mpimbwe Mkoa wa Katavi kuondokana na adha waliyokuwa wakiipata ya kuvuka kwenye Maji katika daraja la mto Msadya baada ya TARURA kuanza kujenga daraja la kudumu katika mto huo.

Akisoma taarifa fupi ya uzinduzi wa Ujenzi wa daraja la kudumu la mto Msadya kwa Mgeni rasmi Mkuu wa Wilaya ya Mlele Filberto Sanga kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Katavi Mwanamvua Mrindoko katika eneo la mto Msadya lilipo daraja la muda.

Meneja wa TARURA Mkoa wa Katavi Innocent Mlay amesema kuwa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mjini (TARURA) inaanza kutekeleza Ujenzi wa daraja la kudumu katika mto Msadya kuanzia Februari 7,2022 kwa muda wa miezi 18 na kukamilika August 7,2023.

Meneja wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mjini(TARURA) Mkoa wa Katavi Innocent Mlay

"lengo la kujenga daraja la kudumu katika mto Msadya ni kunusuru  adha waliyokuwa wakiipata wananchi wa kata ya Chamalendi na Mwamapuli wanaounganishwa na mto huu kuvuka  kwenye maji pindi wanapokwenda katika shughuli za uzalishaji mali kama kilimo na mengineyo"alifafanua Mhandisi Mlay

Aidha Mhandisi Mlay alisema zaidi ya Bilioni 4.1 zimetengwa kwa ajili ya Ujenzi wa daraja hilo la kudumu la mto Msadya fedha zilizotokana na tozo ya mafuta katika Bajeti ya mwaka wa fedha 2021/2022.

Mhandisi Mlay aliongeza pia Mkandarasi aliyepatikana kwa ajili ya kujenga daraja hilo la mto Msadya anaitwa Safari General Business Co.Ltd wa Sumbawanga Mkoa wa Rukwa na tayari wameshasaini mkataba na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mjini (TARURA) tayari kutekeleza mradi huo.

Pia katika kutekeleza mradi huo Mhandisi Mlay alisema yupo Mhandisi Mshauri ambaye atakuwa Mshauri Mkuu katika muda wote wa kutekeleza mradi huo anayeitwa Edge Engineering and consultant Ldt wa Dar es salaam.

Mkuu wa Wilaya ya Mlele Filberto Sanga kwa niaba ya Mgeni rasmi Mkuu wa Mkoa wa Katavi Mwanamvua Mrindoko alisisitiza kuwa kukamilika kwa Ujenzi wa daraja hilo la kudumu la Msadya kutasaidia kutatua changamoto ya usafiri na usafirishaji kwa wananchi wa Halmashauri ya Mpimbwe kwani katika maeneo ya Chamalendi na Ukingwamizi kuna uzalishaji mkubwa  wa mazao ya Biashara na chakula.

Nae Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mpimbwe na Diwani wa Kata ya Chamalendi  Yohana Magembe aliupongeza Uongozi wa Serikali kupitia kwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutenga fedha kwa ajili ya Ujenzi wa daraja hilo la Msadya  kwani lilikuwa kikwazo kikubwa katika maendeleo ya kata tano zilizopo katika Halmashauri hiyo ya Mpimbwe.

Search This Blog

CHAGUA HABARI

Pages