HALMASHAURI YA WILAYA YA TANGANYIKA YASHAURIWA KUTUNZA MAZINGIRA ILI KUONGEZA MAPATO YA NDANI


Baraza la Madiwani Halmashauri ya Tanganyika

Na  Walter Mguluchuma

     Tanganyika

Halmashauri ya Wilaya ya  Tanganyika  Mkoa wa Katavi imeshauriwa kuweka mkakati endelevu wa kutunza mazingira  kwani bado uharibifu wa Mazingira ni mkubwa kwenye baadhi ya sehemu za Halmashauri hiyo .

Ushauri huu umetolewa na Diwani wa Kata ya Kapalamsenga  Jefu  Lameck wakati wa kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri hiyo walipokuwa kwenye kikao cha kupitisha rasimu ya bajeti ya mwaka wa fedha 2022/2023 kilichofanyika katika Ukumbi wa Halmashauri hiyo .

Ameeleza kuwa  bado  mkakati wa  kutunza mazingira haujawa wakuridhisha kwenye baadhi ya maeneo ya Halmashauri hiyo kutokana na uharibifu wa Mazingira unaofanywa kwenye maeneo hayo ambao unaweza kuifanya Halmashauri kukosa mapato yatokanayo na misitu .

Diwani Lameck ameyataja baadhi ya maeneo ambayo misitu yake imekuwa ikivamiwa na kufanyiwa uharibifu ni pamoja na kwenye  Kata yake ya Kapalamsenga .

"maeneo ya Lyamgoloko,Kaseganyama na kwingineko ambapo kama hali hiyo itaendelea inaweza kusababisha  Halmashauri kukosa mapato wanayopata kutokana na fedha za kuuza hewa ya ukaa"alifafanua Lameck

Pia Lameck ameomba ufanyike ukarabati wa Zahanati ya Itunya kwani kwa sasa ina hali mbaya ya uchakavu wa jengo vilevile ameomba makazi ya nyumba za walimu ziboreshwe kwani kuna nyumba wanazoishi walimu zipo kwenye hali mbaya na zimekuwa zikiuliza  nikuuwe lini alisema diwani huyo kwa uchungu

Nae Diwani wa Kata ya Ikola Philimoni  Molo alisema kuwa Halmashauri hiyo imekuwa ikipoteza mapato ya ndani kutokana na kutokusanya fedha kwa wavuvi wanaovua katika ziwa Tanganyika .

Alisema kuwa Maafisa Uvuvi wanapaswa kushirikiana na Madiwani waliko kwenye mwambao mwa Ziwa Tanganyika ili kufuatilia takwimu sahihi za idadi ya mitumbwi iliyoko katika maeneo ya Halmashauri hiyo inayofanya Uvuvi katika Ziwa Tanganyika .

Mwenyekiti wa Halmashauri ya  Wilaya ya Tanganyika  Hamad  Mapengo  aliwasisitiza madiwani waendelee kubuni vyanzo vya mapato  ili kuweza kusaidia kuongeza mapato ya ndani katika Halmashauri hiyo.

 

Search This Blog

CHAGUA HABARI

Pages