Mkuu wa Wilaya ya Tanganyika Onesmo Busweru ambaye pia ni Kaimu |
Na Paul Mathias
Katavi
Halmashauri ya Manispaa ya Mpanda Mkoa wa Katavi imeanza kutoa Tuzo ya Cheti kwa Kata zinazounda Manispaa hiyo na kufanya vizuri katika Usafi.
Akizungumza katika kikao cha Watendaji wa Kata, Mitaa na Madiwani kilichofanyika katika Ukumbi wa Mikutano Manispaa ya Mpanda,Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa ya hiyo ya Mpanda Sophia Kumbuli ameitaja Kata ya Kashaulili kuongoza katika zoezi la Usafi na kuizawadia Cheti cha Usafi kwa Mwezi January 2022 pamoja na fedha taslimu kiasi Cha Shilingi laki Moja.
Katika hatua nyingne kwenye zoezi hilo la kuzitambua kata zinazofanya vizuri katika zoezi hilo la usafi kata ya Shanwe imeshika nafasi ya pili huku kata ya Majengo ikishika nafasi ya Tatu kwa usafi .
Kata ya Kawajense imetajwa kuwa kata ya mwisho katika Usafi na kuzawadiwa Kinyago cha uchafu ikiwa ni Ishara ya kuwafanya kuhakikisha kata hiyo inajipanga vizuri katika zoezi hilo la Usafi.
Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Kashaulili Magreth Kitungulu amesema Kuwa wao katika kata yao ya Kashaulili wamejiwekea utaratibu wa kila Alhamisi kuhamasisha wakazi wa kata hiyo kufanya usafi katika maeneo yao ili kuimarisha na kuendeleza zoezi la Usafi na kuahidi kuendelea kufanya vizuri katika zoezi la Usafi katika Manispaa ya Mpanda.
Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Mpanda |
Nae Diwani wa Kata ya Kawajense Uwezo Bachu amepongeza Mpango wa Usafi ndani ya Manispaa ya Mpanda na wao Kata ya Kawajense wamepokea Kinyago hicho kama changamoto ya kuwafanya wao Viongozi wa Kata kuongeza bidii katika suala la Usafi na kuahidi kufanya vyema kwenye suala la Usafi kwa kuongeza hamasa ya Usafi kwa wakazi wa Kata ya Kawajense.
Mstahiki Meya wa Manispaa ya Mpanda Haidary Sumry amesema wao Baraza la Madiwani katika vikao vyao ajenda ya Usafi wa Manispaa ya Mpanda imekuwa ya kudumu kwa kuhamasisha Madiwani kuendelea kusimamia Usafi kwenye kata zao hivyo zoezi hilo litatia chachu ya kufanya Usafi Kwa kina ndani ya Manispaa ya Mpanda.