![]() |
| Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi ACP Ali Makame Hamad |
Na Irene Temu
Katavi
Wazazi na Walezi Mkoa wa Katavi wametakiwa kuwa karibu na watoto wao kwa kuwapa huduma zote muhimu zinazostahili kupata mtoto ili kujiepusha na vitendo vya kihalifu na kuhakikisha wanakuwepo nyumbani muda unaostahili.
Wito huo umetolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi ACP Ali Makame Hamad na kueleza kuwa baadhi ya wazazi wamesahua majukumu yao ya kulea watoto na kuwaachia Waalimu na watu wengine wanaokuwa wakiwapa masomo ya ziada kuwa nao kwa muda mrefu.
Ameeleza kuwa watoto hao muda mrefu wamekuwa katika masomo ya ziada na watu tofauti na Wazazi hivyo kukosa muda wa kuzungumza na Wazazi wao hali inayopelekea watoto hao kujihusisha katika vitendo hatarisha na hata kupelekea watoto wengine kulawitiwa na hata kubakwa.
"kutokana na muda mwingi mtoto kuwa anajiongoza peke yake na kukosa muda wa kuzungumza na wazazi kueleza shida zao hali hiyo sio nzuri hivyo niwatake wazazi japo mnakimbizana na maisha mpate muda wakuzungumza na watoto wenu na kuwapa mapenzi na malezi ya wazazi"alisisitiza Kamanda Makame
Pia alisema kutokana na wazazi kutofuatilia mienendo ya watoto wao kumeibuka makundi ya uhalifu yanayojiita damu chafu,kaburi moja,mazombi na manyigu majina wanayojipa wenyewe kutokana na matendo wanayoyafanya katika kundi.
Hivyo Kamanda Ali Makame Hamad amewata wazazi kuwa karibu na watoto wao kwa kuwapa malezi Bora na kufuatilia mienendo yao pindi wawapo Shule hata Mazingira ya nyumbani.
Nae Afisa Maendeleo ya Jamii Mkoa wa Katavi Kiame Kiame amesema kuwa kwa baadhi ya watoto wanaokumbana na madhila mbalimbali katika jamii kama kulawitiwa au kubakwa inatokana na baadhi ya wazazi kuwaachia majukumu watoto wadogo kulea familia wao wakiwa katika kuhangaikaji na kusahau majukumu yao ya kutunza familia.
"unakuta mtoto ni muda wa kuwa Shule lakini yupo barabarani na ungo wa ndizi,mchicha na mihogo kichwani anazunguka kuuza mzazi yupo na kazi nyingine,mtoto huyo anapita katika maeneo mengine hatarishi yanayopelekwa kubakwa au kulawitiwa"alifafanua Kiame.
Alisema wanapambana na Jamii kwa kutoa Elimu kwa wazazi kulea watoto na kuwachukulia hatua wazazi wanaowapa watoto kazi ya kulea watoto wenzao na kuwafanyisha biashara za mitaani kuuza matunda na mbogamboga hali inayopelekea ongezeko la mimba za utotoni na watoto wa mitaani.
Miongoni mwa wazazi akiwepo Hellena Mkapa anasema tabia ya watoto wadogo kuanzia umri wa miaka 5 hadi 8 kupewa majukumu ya kulea familia wazazi wakiwa mashambani inasikitisha na kusababisha watoto wadogo kuruka hatua za ukuaji kwa kubebeshwa majukumu makubwa ili hali yeye bado ni mtoto na anahitaji malezi ya mzazi Ila anageuka kuwa mzazi.
Inviolatha Masawe ni mzazi anasema kitendo cha wazazi wa siku hizi kuhangaika na maisha zaidi kuliko kulea familia na kuwaachia Dada wa nyumbani inapelekea watoto kuharibika na kufanyiwa vitendo vya ukatili bila mzazi kugundua kwani hana muda wa kuzungumza na watoto.
"Wazazi tubadilike ni kweli familia ili zistawi lazima tufanye kazi lakini na muda wa kuwa karibu na familia zetu uwepo sio watoto wanaharibikiwa kwa kisingizio cha ugumu wa maisha tunahangaika"alisisiza Inviolatha
Hivyo wazazi wameaswa kutowafanyisha kazi watoto wadogo na badala yake wahakikishe wanawalea katika maadili mema na kuhakikisha usalama wao wawapo shuleni na hata nyumbani.
