Walter Mguluchuma,Katavi .
Takukuru Mkoa wa Katavi katika pindi cha miezi mitatu ya kuanzia Januari hadi Machi mwaka huu imefanya kazi ya kufatiliaji wa fedha za utekelezaji wa miradi ya Maendeleo saba yenye thamani ya zaidi ya shilingi Bilioni 2.3.
Hayo yasemwa na Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Katavi Festo Mdede wakati alipokuwa akitowa taarifa ya utekelezaji wa Takukuru mbele ya Waandishi wa Habari kwa kipindi cha kuanzia mwezi Januari hadi Machi mwaka huu.
Alisema Takukuru wamefanya kazi ya ufatiliaji wa fedha za utekelezaji wa miradi ya Maendeleo saba yenye jumla ya thamani ya shilingi 2,346,844,793 vilevile wamefuatilia ujenzi wa vyumba vya madarasa vya shule za sekondari na vituo shikizi namba 5,441 chini ya mpango wa maendeleo na Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya UVIKO 19.
Fedha hizo zilitolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Samia Suluhu Hassan kupitia mpango huu Mkoa wa Katavi ulipokea jumla ya sh Bilioni 8,580,000,000.
Alibainisha kuwa lengo la ufatiliaji huo ni kuangalia iwapo kuna mianya ya Rushwa kwenye utekelezaji wa miradi na kuongeza uwazi na upatikanaji wa thamani ya fedha za miradi ya Serikali.
Mdede alieleza kuwa katika kusimamia miradi hiyo Mkuu wa Mkoa wa Katavi aliunda timu za ufuatiliaji katika maeneo yote ya Halmashauri za Mkoa wa Katavi katika ufuatiliaji huo ukiukwaji wa taratibu katika kukamilisha miradi ulibainika .
Alizitaja kasoro zilizobainika kwenye miradi hiyo kuwa ni wizi wa vifaa vya ujenzi,matumizi mabaya ya fedha za miradi ,ujenzi kutokamilika kwa wakati na baadhi ya thamani kutengenezwa chini ya kiwango .
Mkuu huyo wa Takukuru Mkoa wa Katavi alisema baada ya ubainishwaji wa makosa hayo Takukuru ilichukua hatua stahiki ikiwa ni pamoja na kutoa maelekezo kwa waliotengeneza thamani za shule chini ya kiwango kurudia utengenezaji kwa gharama zao binafsi .
Pia kuanzisha uchunguzi kwa makosa mengine ya wizi na vifaa vya ujenzi na matumizi mabaya ya fedha za miradi ili hatua stahiki zichukuliwe.