TAKUKURU MKOA WA KATAVI IMEPOKEA MALALAMIKO 61 YA TUHUMA ZA RUSHWA TAMISEMI YAONGOZA



Mkuu wa Takukuru  Mkoa wa Katavi Festo  Mdede akitowa taarifa ya utekelezaji kazi wa Taasisi hiyo  kwa kipindi cha miezi mitatu kuanzia Januari hadi Aprili ambapo jumla ya malalamiko 61 yamepokewa huku malalamiko 57 yakihusu vitendo vya  Rushwa(Picha na  Walter  Mguluchuma)


 Na Walter Mguluchuma 

Katavi 

Taasisi ya kuzuia,kupambana na Rushwa(TAKUKURU) Mkoa wa Katavi katika kipindi cha kuanzia mwezi Januari mwaka huu wamepokea malalamiko 61 kati ya malamiko hayo malalamiko 57 yanahusu vitendo vya Rushwa huku TAMISEMI wakiongoza kwa kulalamikiwa.

Hayo amesema Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Katavi Festo Mdede mbele ya Waandishi wa Habari wakati alipokuwa akitoa taarifa ya utendaji kazi wa Taasisi hiyo kwa kipindi cha miezi mitatu kuanzia Januari hadi machi mwaka huu. 

Alisema jumla ya malalamiko 61 yamepokelewa kwenye Taasisi hiyo kwa kipindi hicho ambapo malalamiko 57 yalihusu vitendo vya Rushwa na malalamiko manne hayaku husu Rushwa huku TAMISEMI wakiongoza kwa kulalamikiwa malalamiko 37 wakifuatiwa na idara ya ardhi yenye malalamiko matano. 

Alizitaja idara na sekta nyingine zilizolalamikiwa ni Amcos , Ujenzi , Polisi , Mahakama , Maliasili , Mazingira ,Maji , Tanesco,Utawala , TFS na Bima. 

Mdede alisema katika kipindi hicho kesi mpya mbili zimefunguliwa Mahakamani na kufanya kuwa na kesi 11 zinazoendelea Mahakamani ambapo kesi moja tayari imehukumiwa Mahakamani na mshitakiwa alipatikana na hatia na kesi kumi bado zinaendelea Mahakamani zikiwa katika hatua mbalimbali ya usikilizaji.   

Amebainisha kuwa katika kipindi cha Aprili hadi June mwaka huu Takukuru Mkoa wa Katavi wanatarajia kuongeza nguvu katika uchunguzi wa malalamiko yanayopokelewa hasa yanayo husu ubadhilifu wa fedha za mpango wa Maendeleo kwa ustawi wa Taifa na Mapambano Dhidi ya UVIKO 19 katika Halmashauri zote za Mkoa wa Katavi. 

Pia wataendelea kutowa elimu kwa umma juu ya wajibu wa kila mwananchi kushiriki katika kupambana na Rushwa na kutoa taarifa zinazohusiana na Rushwa kwa Takukuru.

Mkuu huyo wa Takukuru Mkoa wa Katavi alisema bado kumeendelea kuwa na wimbi la matapeli wanaojifanya ni Maafisa wa Takukuru ambao wamekuwa wanapiga simu kwa watu mbalimbali wakiwapa maelekezo na maagizo kwa watu hao ikiwa ni pamoja kuwataka waripoti ofisi ya Takukuru au kutaka kuonana nao huku lengo lao likiwa ni kuwatishia ili waweze kuwapatia fedha . 

MWISHO

Search This Blog

CHAGUA HABARI

Pages