KUREJESHWA MASOMONI WANAFUNZI WALIOPATA MIMBA UTAFANIKIWA KATAVI?.


Moja ya kituo ambacho kinatumiwa na wanafunzi ambao walipata matatizo ambayo yaliwafanya kushindwa kuendelea na masomo shuleni katika mfumo rasmi.Kituo hiki kinapatikana Manispaa ya Mpanda Mkoa wa Katavi.


Na George Mwigulu.

WARAKA wa elimu namba mbili wa mwaka 2021 kuhusu urejeshwaji shuleni wa wanafunzi waliokatiza masomo katika elimu ya msingi na sekondari kwa sababu mbalimbali hususani ujauzito nakuanza rasmi kutekelezwa nchini mwaka 2022 ni faraja kubwa kwa wanafunzi wa kike ambao ndoto zao zilififia na kukosa matumaini ya elimu.

Beatrice Gati,Afisa Elimu ya Watu wazima Mkoa wa Katavi akielezea hivi karibuni ofisini kwake mipango ya Mkoa huo namna wamejipanga kufanikisha kurejeshwa masomoni wanafunzi waliopata mimba na matatizo mengine .

Serikali ya awamu ya sita chini ya rais Samia Suhulu Hassain kwa kutambua umuhimu wa masuala ya usawa wa kijinsia kwenye upatikanaji wa fursa ya elimu amefanikisha urejeshwaji wa wanafunzi hao darasani na kupongezwa dunia kote ambapo Mkoa wa Katavi unaendelea kufanikisha adhima hiyo licha ya baadhi ya wazazi na walezi bado hawajawa na mwitikio mzuri kwa ajili ya kuwarejesha masomoni wanafunzi wa kike.

Serikali ya Mkoa huo chini ya utaratibu wa kuboresha elimu ya sekondari Tanzania (SEQUIP) inatekeleza mpango huo ambapo licha ya kupiga hatua ya kuanzisha vituo vitatu vya shule na kudahili wanafunzi 71 lakini bado matatizo yanawarudisha nyuma.

Beatrice Gati,Afisa elimu ya watu wazima Mkoa wa Katavi amebainisha hayo hivi karibuni ofisini kwake ambapo amesema dira ya elimu nchini ni kuwa na watu walioelimika,maarifa,stadi,uwezo  na mtizamo chanya utakaochangia kuleta maendeleo kwa kila mtoto bila kujali jinsi anapata fursa sawa ya kupata elimu bora.

Gati ameweka wazi kuwa kutokana na serikali  kuongeza fursa na kuboresha elimu kwa ngazi zote kwa kutunga sheria,kanuni,miongozo na nyaraka lakini jamii inapaswa kuwa sehemu ya kukataa mambo yanayomrudisha nyuma mwanafunzi hususani wa kike.

Akielezea mpango wa SEQUIP amesema wanafunzi wanaokatiza masomo wazazi na walezi ni chanzo kikubwa cha kushindwa watoto hao kunufaika na elimu kwani wanakosa ndugu wa kuwaachia watoto ili waendelee na masomo.

“Unakuta mzazi anasema aah!,mtoto atamwachia nani.Mimi nina shughuli zangu za kwenda shambani na nafanya biashara…kwahiyo wanakosa walezi ambao watakuwa waangalizi wa watoto pindi wawapo shuleni” Amesema Gati.

Wasichana kukata tamaa baada ya kupata ujauzito na ugumu wa maisha umetajwa pia kuwa ni sababu zinazokwamisha kurejea masomoni wanafunzi hao kwa maana baadhi yao baada ya kupata ujauzito wamelazimishwa kuolewa na kuendelea na maisha mengine.

Afisa Elimu huyo amesema “wasichana wengi wa kike wanaopata ujauzito wanakata tamaa kwa kuhisi wamefanya makosa makubwa,kubaguliwa na kutengwa na wanafunzi wenzao ambapo changamoto zote hizo zinawafanya kuathirika kisaikolojia”.

Katika kuhakikisha mpango wa kuwarejesha masomoni wanafunzi waliopata mimba Katavi unafanikiwa. Mkoa huo umepitisha maazimio mwezi wa nane mwaka huu kuwa kila halmashauri kuanzisha kituo cha wanafunzi wa kike cha SEQUIP na kudahili wanafunzi kuanzia 50 ambapo kwa halmashauri tano watakuwa na wanafunzi hao zaidi ya 250 kuanzia mwezi wa kwanza mwaka ujao.

Mwl, Idrisa Meru na Mtaalamu wa masuala ya saikolojia ya wanafunzi kutoka kituo cha Elimu ya Mfumo usio rasmi Kashato,Manispaa ya Mpanda Mkoani hapa anadhibitisha ugumu wa kufanya vizuri kitaaluma wanaoupata wanafunzi hao kwa sababu ya ushirikiano mbovu kati ya wazazi/walezi na waalimu uliopo.

Mwl Idrisa anasema “...Mwanafunzi mmoja wa kike alinifuata na kunieleza namna anavyobaguliwa na familia yake kutokana na kupata ujauzito kwa bahati mbaya baada ya mtoto kuzaliwa wazazi wake walimwita ni haramu lugha ambayo ilimvunja moyo msichana huyo na kuathiri mahuzulio yake darasani”.

Mwalimu Idrisa Meru na Mtaalamu wa masuala ya saikolojia ya wanafunzi kutoka kituo cha Elimu ya Mfumo usio rasmi Kashato,Manispaa ya Mpanda Mkoani Katavi hivi karibuni ofisini kwake akielezea mambo kadha ya kisaikolojia ambayo yanawakabili wanafunzi hao

Moja ya jengo jipya la vyumba vya madarasa ambalo limejengwa hivi karibuni na Manispaa ya Mpanda Mkoa wa Katavi,Ikiwa ni jitihada zinazofanywa na manispaa hiyo ya kuimarisha miundombinu ya kujifunzia kwa wasichana ambao wamepata changamoto mbalimbali na kushindwa kuendelea na masomo.

 

Licha ya changamoto hizo ameeleza kuwa hali ya kitaaluma ya wanafunzi hao ni nzuri kutokana na Moduli za masomo wanazotumia zimerahisisha namna ya kujifunza na kwa ushirikiano uliopo kati ya wanafunzi na walimu kwa mtihani ujao wa QT utakao fanywa na Stage One kwa asilimia 95 watafaulu” Amesema Mwl Idrisa.

Akijibu hoja ya mfumo wa elimu usio rasmi kuwa unawatenga wanafunzi na kuonekana kama kundi maalumu amesema “Kuna faida kubwa kwenye mfumo huu,kuliko wakosoaji wanavyofikiria,mbali na kusoma masomo ya sekondari waliyokatisha,wanafundishwa masuala mengine yatakayowapa ujuzi na kuendesha maisha yao na kulea watoto wao huku ikiwa ni sehemu nzuri ya kuepuka kubaguliwa na wanafunzi wengine wasio na watoto na kuwaathiri kisaikolojia” Amebainisha Mwl Idrisa.

Kwa upande wa mwanafunzi wa kike wa kituo cha Elimu ya Mfumo usio rasmi Kashato,Patricia Mpagama amesema zipo sababu zinawafanya wasichana  kutokurudi shule ambazo ni wazazi  kukosa mwamko wa kuwapigania watoto wa kike na badala yake kulenga kuwaozesha,kuwapa jukumu la kuwa walezi wa watoto wa ndugu zao na mazingira mabovu ya kutokuishi na wazazi kwa sababu ya vifo na kuwa kikwazo kwa wasichana waliopata ujauzito kutokurudi shule.

 “Unakuta binti wa miaka 18 anaishi na bibi yake kwa kuwa wazazi wake walishafariki anaogopa kumwacha bibi yake nyumbani maana yeye ni nguzo ya kuhudumia familia bila kujali umri wake kuwa bado ni mdogo” Amesema Patricia.

Patricia anashukuru rais Samia Suhulu Hassain kwa mpango huo kwani anaimani atatimiza ndoto zake za kuwa daktari bingwa kwani dada yake alishindwa baada ya kupata changamoto inayofanana na yake “Lakini mimi nahitaji kuzitimiza kwa sababu ndoto ya kuwa daktari nilikuwa nayo tangu nikiwa mtoto mdogo” Amesisitiza Patricia.

Charles Mabula,Mkazi wa Mtaa wa Rungwa Manispaa ya Mpanda Mkoa wa Katavi,kama mzazi anaeleza kuwa suala la wanafunzi kukatizwa masomo hasa kwa kupata ujauzito wazazi wengi wameshindwa kupokea na kukubali makosa yanayofanywa na watoto wao hivyo kukata tamaa ya kuwarudisha shule kuendelea na masomo pindi wanapojifungua licha ya serikali kuweka mfumo mpya wa kuwarejesha shule.

Mabula amesema kuwa mfumo mpya wa elimu hiyo bado haujapewa msukumo mkubwa kama ilivyo kwa elimu iliyo ya mfumo rasmi ambapo utaona viongozi mbalimbali wa serikali wakitoa matamko makali ya kuhakikisha wazazi na walezi wanaandikisha watoto shule kuingia darasa la kwanza au kidato cha kwanza.

Ameeleza ili Mkoa wa Katavi uweze kufikia mpango huo mpya wanapaswa kutoa hamasa kwa nguvu kwenye jamii yote ya Mkoa wa Katavi licha ya kuwa na changamoto mbalimbali ambazo zinaweza kujitokeza kukwamisha juhudi hizo kutokana na kuwa suala la mwanafunzi wa kike kurudi shule ni hiali yao kama mtu anayefahamu umuhimu wa elimu au la!.

Search This Blog

CHAGUA HABARI

Pages