MILA NA TAMADUNI NI KIKWAZO KUFIKIA USAWA WA KIJISIA SEKTA YA ELIMU KATAVI.


 Na George Mwigulu, Katavi.

USAWA wa kijisia ni nyezo muhimu katika jamii yoyote kwa ajili ya kufanikisha hatua ya upatikanaji wa rasilimali na fursa zingine bila kujali jinsia ambapo utawezesha maendeleo ya kweli ndani ya jamii.

Usawa huo utafikiwa endapo pia elimu ya afya ya uzazi ndani ya jamii itapewa kipaombele na jukumu hilo halibaki kwa njinsi moja aidha ya kike au ya kiume inayositahili kupata fursa hiyo.

Kwa mujibu wa utafiti wa afya ya uzazi na mtoto wa mwaka 2015/16, uliofanywa na Ofisi ya Takwimu ya Taifa (NBS) kwa kushirikiana na Wizara ya Afya viwango vya mimba/uzazi kwa wasichana wa miaka 15-19 kwa mikoa ya Tanzania bara inaonyesha mkoa wa Katavi unaongoza kwa asilimia 45 huku wasitani wa kitaifa ukiwa ni asilimia 27 ya wasichana wameanza uzazi na asilimia 21 wameshazaa mtoto hai mmoja na asilimia 6 ni wajawazito.

Viwango hivyo vinaonesha namna mwanamke yuko nyuma katika kupata fursa sawa ya elimu Mkoani Katavi ambapo chanzo kikubwa ni mila na tamaduni ambazo zinawanyima wanawake na wasichana kupata elimu ya afya ya uzazi itakayowezesha kuondoa ombwe kati ya wanaume na wanawake la elimu ambapo kwa sasa ni kubwa.

Kuificha elimu ya afya ya uzazi kwa vijana imeleta sura nyingine ya hatua ambayo baadhi ya vijana wamejikuta wakiingia kwenye mapenzi ambayo sio salama,huku hatima ya elimu yao ikisalia mashakani na pengine kushindwa kutimiza ndoto za kimaisha.

Agelina Mashala mkazi wa kijiji cha Ilangu Wilaya ya Tanganyika Mkoa wa Katavi anathibitisha kuwa hawezi kuwaambia vijana wake kuhusu  afya ya uzazi kama kutumia kondomu ama vidonge kwani atakuwa kama anawaelekeza katika hatua nyingine ya uzinzi kwenye maisha yao.

"…sisi ni waafrika hatujafundishwa na mababu zetu kuwaeleza watoto wetu mambo ya aibu namna hiyo,haitupasi hata kidogo masuala ya kitandani kuyaweka hadharani kwa watoto,naomba fahamu hivyo habari za maisha ya kizungu hayana maana kwetu" amesema Agelina.

Mitizamo kama hiyo wasichana wengi inawafanya kutokujua haki zao au wahajui watafute wapi msaada isipokuwa kwenye famila zao au taasisi za kitamaduni ambazo zimegeuka na kuwafanya wahanga wa mimba na ndoa za utotoni.

Kwa maana hiyo  vijana wengi wamejengewa woga wa kutokutoa taarifa za kushawishiwa na kulazimishwa kufanya vitendo vya ngono  hata wakiwa na umri mdogo iwe kunyanyaswa kwenye ndoa kwa sababu hawana imani na mfumo wa kisheria pamoja na familia na jamii kwa ujumla.

Mzee wa kimila Shigera Funuki mkazi wa kijiji cha Mazwe wilaya ya Tanganyika mkoani  humo amesema suala la kutokubaliana na elimu ya afya ya uzazi inadhaniwa kuwa ni njia ya kuwalinda dhidi ya ngono  na mimba kabla ya ndoa.

Shigera anasema ‘’ afya ya uzazi inawafanya wasichana kuwa na ufahamu mkubwa wa masuala ya kingono ambayo yanamfanya mtoto kutamani kufanya majaribio ya kujamiana na kupata mimba ambazo zinashusha heshima za familia na kushusha kiasi cha mahari ambayo familia inayopokea’’.

Mkazi wa Kijiji cha Mishamo Wilaya ya Tanganyika, Mariam Hussein ambaye mwanaye wa kike (jina limehifadhiwa) amepata ujauzito  akiwa na umri wa miaka 13 na kukatisha masomo yake amesema kuwa utendaji wa kitamaduni  unadhoofisha upatikanaji wa elimu ya afya ya uzazi na kutengeneza ukuta kati ya wazazi/walezi na watoto.

"sikuona umuhimu wa kumpatia elimu ya afya ya uzazi binti yangu  kutokana na jinsi alivyokuwa mtulivu na mpole mwenye kupenda elimu sana…nilishangaa ghafula kuona mabadiliko kwenye mwili wake na kuwa tayari  amepata mimba,nimejiidanganya mwenyewe na kumwangamiza mwanangu’’ amesema Mariam.

Jambo la kusitaajabu zaidi ni namna mbavyo wazazi/walezi wa kiume wamekaa mbali zaidi na suala la afya ya uzazi huku wakiwaachia majukumu hayo wanawake pekee huku kiza cha ni nani awajibike kikiwa bado hakifahamiki kutokana na ukandamizaji wa afya ya uzazi inayodhorotesha kufikia usawa wa kijinsia kwenye sekta ya elimu.

Elida Machungwa,Mratibu wa Huduma za Afya ya Uzazi na Mtoto Mkoa wa Katavi, wakati wa mdahalo unaohusu Usawa wa Kijisia,Afya ya Uzazi na Ukatili wa Kijinsia uliofanyika katika ukumbi wa Madini Manispaa ya Mpanda hivi karibuni amesema kuwa tatizo la mimba za utotoni ni changamoto ambayo inahitaji juhudi za pamoja kati ya serikali,wananchi na wadau wa maendeleo kutoa elimu kwa jamii.

Mratibu huyo meweka wazi kuwa baadhi ya makabila katika mkoa huo yana mila na desturi ya kusisitiza mwanamke kuzaa watoto wengi,hivyo kusababisha watoto wa kike kuingia katiks ndoa  wakiwa na umri mdogo wakiwa chini ya umri wa miaka 18.

Aidha baadhi ya taasisi za kidini kutokuwa na mpango wa kutoa elimu kwa watoto wa kike kuhusu athari za mimba za utotoni na kuona kuwa ni jambo la kawaida kwa watoto chini ya miaka 18 kupata ujauzito.

Ubaguzi mkubwa wa kujisia kwa wanawake na wasichana majumbani,shuleni na katika jamii imekuwa ni tatizo kubwa inayochangia mimba za utotoni kwa jamii nyingi hasa zinazoishi vijijini.

“ katika maeneo mengi ya mkoa wa Katavi watoto wa kike ndio wanashiriki zaidi kufanya kazi zisizo na kipato,matokeo yake wasichana hawana thamani ya kiuchumi inayotambulika kwenye kaya,zaidi ya mahari na elimu haichukuliwi kama kipaombele” amesema Elida.

‘’ Elimu inapaswa kuzidi kutolewa kwa vijana pamoja na jamii kwa ujumla ili jamii iweze kubadili mitizamo hasi hasa ambayo inahusuiana ukatili dhidi ya watoto na kuwanyima haki yao ya kupata elimu ya afya ya uzazi’’ amesema Mratibu huyo.

Amefafanua kuwa  ni wakati sasa umefika kwa jamii mkoani humo kupinga kwa nguvu zote mimba na ndoa za utotoni na kuhamasisha usawa wa kijisia kutokana na waathirika zaidi kuwa ni wasichana ambao hukatishwa masomo na kukosa fursa za kiuchumi kwa ajili ya maendeleo huku wanaume wakizidi kupiga hatua zaidi kwenye elimu.

Kwa upande wa mashirika ya siyo ya kiserikali (NGO) ya mkoa wa Katavi,Taasisi ya kuwakomboa vijana  inaendeleza  mapambano dhidi ya mila na tamaduni zinazowanyima vijana hasa wanawake na wasichana kupata elimu ya afya ya uzazi itakayowafanya kufikia usawa wa kijinsia kwenye elimu.

Mkurugenzi wa Taasisi hiyo, Saimoni Kanyuro amesema wameamua kuishirikisha makundi ya jinsia zote katika utoaji wa elimu hasa kwa wanaume ambao wanamatumizi ya mfumo dume kwenye ngazi za familia zao.

Kanyuro ameeleza kuwa kuna hatua makubwa imefikiwa kwani wanaume wameonesha utayari wa kuwapigania watoto wa kike kupata elimu sawa na wanaume.

Amebainisha kuwepo kwa changamoto ya kuwafikia watu wenye ulemavu hasa wasichana kwani jamii bado inadhana potofu ya kuwaficha.hivyo bado wanaendelea kuwatafuta popote pale walipo moani Katavi na kuwafikia  kuwapa elimu.

Search This Blog

CHAGUA HABARI

Pages