Na George Mwigulu KTPC,Katavi.
Wanafunzi wa shule za msingi na sekondari katika halmashauri ya wilaya ya
Tanganyika Mkoani Katavi wamendelea kunufaika na vifaa kwa ajili ya
utakasishaji ili kuwawezesha wanafunzi hao kujikinga na magonjwa ya mlipuko
mashuleni.
Vifaa hivyo kwa wakati tofauti vimeendelea kutolewa na shirika la Hope Centre
for Children,Girls and Women in Tanzania (HCCGWT) kwa Halmashauri hiyo ili
kuhakikisha wanafunzi hususani wa kike wanakuwa wenye afya njema na kufurahia
mahala pa kujifunzia.
Akikabidhi jana vifaa hivyo kwa Mganga Mkuu wa Wilaya ya Tanganyika Dr Selemani
Mtenjela katika umbumbi wa idara ya Maji Manispaa ya Mpanda Mkoani Katavi
Mkurugenzi Mtendaji wa HCCGWT,Halma Lila aliweka wazi kuwa tafiti
walizofanya na kwa takwimu za serikali zinaonesha kunauhitaji kubwa kwenye wilaya
hiyo wa vifaa hivyo.
Uhitaji huo mkubwa unasababishwa na wingi wa watu waliopo wilaya ya Tanganyika
ikilinganishwa na wilaya zingine za mkoa wa Katavi,Changamoto za kijiografia
kama vile wilaya hiyo kuwa mbali zaidi aidha kushuhudiwa kwa idadi kubwa
ya mimba za utotoni.
Kwa kuzingatia hayo Halima alisema licha ya kutoa vifaa vya utakasishaji pia
wametoa taulo za kujisitiri kwa wasichana katika shule husika ili kuhakikisha
wasichana wanakuwa na hedhi salama nyakati za dharula.
"tumeona ni vema kutoa vifaa vya kujifungulia pia kwa wakinamama
wajawazito katika zahanati mbili za wilaya ya Tanganyika hasa kwa
wakinamama wasiokuwa na uwezo na wanaishi kwenye mazingira magumu" alisema
Halima.
Vilevile wametoa sabuni kwa ajili ya zahanati,mashine za kunawia mikono kwa
ajili ya utakasishaji pamoja na kondomu za kiume kwa ajili ya kujikinga na
maambukizi ya virusi vya ukimwi na magonjwa ya zinaa ambapo vifaa vyote
vimegharimu milioni tatu na laki nane na therathani na tano elfu.
Aidha Halima alifafanua kuwa licha ya kutofa vifaa mbalimbali pia Hope Centre
for Children,Girls and Women in Tanzania wanaendelea kutoa elimu kuhusu
utakasishaji,kuelimisha kuhusu maswala ya afya ya uzazi kwa ujumla pamoja
na kuelimisha jamii jinsi ya kujikinga na maambukizi ya virusi vya ukimwi
na magonjwa mengine ya zinaa.
Mganga Mkuu wa Wilaya ya Tanganyika Dkt Selaman Mtenjela akipokea vifaa hivyo
aliishukuru Hope Centre kwa kuja mkoani Katavi na kufanya kazi katika maeneo
muhimu ,ambapo vifaa vyote walivyotoa vina lengo la kuhakikisha usalama wa
binadamu mama,kijana na watoto wachanga.
Dkt Mtenjela alisema kuwa kwa muda ambao wamefanya kazi na Hope centre wamekuwa
wakitoa mchango mkubwa hasa wa kutoa elimu kwa kuhakikisha vijana wanakuwa na
uelewa kwenye maeneo ya uzazi salama na kufanya maamuzi katika masuala ya
mahusiano.
"tunahitaji Watanzania hasa vijana wenye uelewa kwenye masula ya uzazi ili
uzazi uwe salama na wenye manufaa kwa mazazina jamii kwa ujumla" alisema
Dkt Mtenjele.
Naye Mwl Venas Tesha Mratibu wa elimu ya afya mashuleni Wilaya ya Tanganyika
alisema kuwa kabla ya Hope Centre kulikuwa na matatizo kwenye shule za msingi
na sekondari kuhusuana na wasichana ambao wanaingia hedhi walikuwa wanakosa
namna ya kujisitili hasa wakiwa mashuleni.
Mwl Tesha alisema kuwa matokeo yake pindi wanapopatwa na hali hiyo ya hedhi
mashuleni walikuwa wanakimbia masomo aidha kuwa watoro kabisa na kuathiri
ufaulu wao kitaaluma.Hivyo baada ya Hope Centre kutoa vifaa hivyo tatizo hilo
limepungua.