Mapolomoko ya maji yaliyo katika hifadhi ya Nkondwe Wilaya ya Tanganyika Mkoa wa Katavi. |
Na Walter Mguluchuma KTPC.Nkondwe.
Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika mkoani Katavi imezindua kituo kipya cha utalii chenye vivutio kadhaa.
Kituo hicho cha Nkondwe kinapambwa na vivutio vingi vya utalii kama maporomoko
ya maji, sokwe na ndege wanaoitwa fundi chuma ambao ndio 'chifu wa ndege wote'
.
Ndege hao wa aina yake huishi wawili katika kiota chenye uzito wa hadi kilo 60.
Eneo hilo pia lina mapango, mojawapo ndani kuna bangili sita za shaba na meno
ambayo hayajajulikana ni ya kiumbe gani.Pia kuna wanyama adimu kama kakakuona
na mhanga.
Uzinduzi wa kituo hicho ulifanyika wiki mbili zilizopita na Mkuu wa Mkoa wa
Katavi, Juma Homera, aliyewataka wananchi kutembelea kituo hicho kuona fursa
zilizopo.
Mwenyekezaji wa kituo hicho cha utalii, Mohamed Yusuph Mohamed maarufu kwa jina
la Bila, anasema wapo tayari kuanza kupokea watalii.
Muonekano wa hali ya mandhari ya hifadhi ya Nkondwe yakiwa tayari kwa ajili ya watalii wa ndani na nje ya nchi. |
"Mbali na maporomoko ya maji na sokwe, hapa kuna wanyama kama chui, swala, mbawala na mhanga. Ni eneo salama na wanyama hawa huonekana bila shida," anasema.
Kuhusu ndege hao wa ajabu, Bila anasema huishi kwenye kiota walichotengeneza wenyewe chenye uzito wa kilo 60 na ndani yake kumetengenezwa mithili ya nyumba ya kuishi binadamu.
"Ndani ya kiota kuna sebule ambayo hutumiwa na ndege hao kwa mapumziko; na kuna chumba cha kulala," anasema.
Maporomoko ya maji ya Mto Nkondwe yana mapango na Bila anaiomba serikali
kufanya utafiti kujua meno yaliyomo ndani ya moja ya mapango hayo ni ya kiumbe
gani na kiliishi hapo miaka gani.
"Itakuwa vyema iwapo wataalamu wa kisasa pamoja na wazee wa kimila waje
hapa kwenye pango hili, wazitoe bangili hizo pamoja na hayo meno
wakayatafiti," anasema.
Wakati sokwe wakiaminika kupatikana katika hifadhi za Gombe na Mahale mkoani KIgoma, wanyama hao wapo pia Nkondwe na tayari wameanza kuwa rafiki na watu kutonana na usalama uliopo kwenye eneo hilo la kituo cha utalii.
Bila anabainisha kuwa kabla ya kuzinduliwa rasmi kwa kituo hicho amekuwa akipokea wageni mbalimbali ambao huvutiwa na eneo hilo.
Ni moja ya aina ya ndege wa aina yake wanaopatika katika hifadhi Nkondwe wakifurahi uasiri wa mazingira ya kuvutia. |
Hata hivyo, wageni wake wengi ni kutoka nje ya Mkoa wa Katavi.
"Wabende wanaoishi Dar es Salaam wamekuwa wakifika hapa kwani huamini kuwa eneo hilo ni maalumu kwa matambiko ya kabila lao ambao ndio wenyeji wa Wilaya ya Tanganyika," anasema.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Tanganyika, Rojas John, anasema pamoja na kutenga maeneo ya utalii, Halmashauri watahakikisha maeneo hayo yanalindwa kwa nguvu zote yasiharibiwe na watu.
"Kituo hiki ni sehemu muhimu katika kukuza uchumi wa Halmashauri na wananchi. Pia ni sehemu nzuri ya kupumzika," anasema John.
Baadhi ya watali kutoka maeneo tofauti tofauti barani ulaya wakiwa kwenye hifadhi ya Nkondwe. |
Gharama za malazi kituoni hapo ni Sh 30,000 huku ada ya kuigia ikiwa ni Sh 5,000.
Bruno Nicas ni ofisa maliasili na mazingira mwenye mchango mkubwa katika kukuza utalii wilayani Tanganyika anayesiika kwa kuhakikisha misitu inakuwa salama.
Mnyonge mnyongeni lakini haki yake mpeni hivi ni watumishi wangapi wanaoweza kufanya kazi kama anazofanya Bruno; kutembea kwa miguu usiku na mchana bila kuchoka?
Ni bahati mbaya kuwa wapo 'wakubwa' fulani wanaotaka kumkwamisha, wengine wakiwa ni viongozi wa serikali wilayani Tanganyika.
Kiota cha ndege katika hifadhi ya Nkondwe Wilaya ya Tanganyika Mkoa wa Katavi |
Mkazi wa Ntongwe, Yassin Kibigazi, anasema eneo hilo la kituo cha utalii ni maarufu tangu zamani, isipokuwa halijatangazwa.
"Wapo ndugu zetu wanaoamini kuwa ni sehemu muhimu kwa matambiko kwa kuwa wazee wa zamani walikuwa wakifika hapa kuondoa shida mbalimbali kama maradhi ya muda mrefu, mikosi na kuombea mvua," anasema Kibigazi.
Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Homera, alionekana kufurahishwa sana kwa kuanzishwa kwa
kituo hicho na kutoa maelekezo kwa viongozi wa Halmashauri ya Tanganyika.
Miongoni mwa maelekezo hayo ni kupeleka wataalamu wao na wazee wa kimila eneo
hilo kufanya utafiti ulioombwa na Bila.
"Ili eneo hili liwe salama, ni vema Halmashauri iendelee kufanya doria za
mara kwa mara kuwaondoa watu wanaovamia vyanzo vya maji na misitu,"
anasema Homera.
Amempongeza mwekezaji Bila kwa ubunifu wake huo kwani sasa watu wengi
wanatamani kwenda kupumzika hapo, akiwepo yeye mwenyewe.
Homera anasema eneo hilo litawafumbua macho watu ambao walikuwa hawajui
historia na kwamba mcheza filamu maarufu duniani, Arnold Schwarzenegger,
amewahi kulitumia katika moja ya filamu zake na kumpa umaarufu mkubwa.
"Wangapi mlikuwa mnalifahamu hilo? Basi fanyeni jitihada za kutembelea hapa," anasema.
Takwimu zinaonyesha kuwa Mkoa wa Katavi ndio wenye sokwe wengi zaidi barani
Afrika.Msitu wa Ntongwe Mashariki kuna sokwe zaidi ya 2,500 na Ntongwe
Magharibi wapo zaidi ya 1,000 idadi ya sokwe waliopo Kigoma haifikii hata nusu
ya waliopo Katavi.