Naibu waziri wa Katiba na Sheria Godfrey Pinda akisalimiana na baadhi ya Maofisa wa Jeshi la Magereza katika Gereza la Mahabusu Mpanda |
Daniel Kimario KTPC,Katavi.
Naibu Waziri wa Wizara ya Katiba na Sheria Mhe. Geophery Mizengo Pinda amefanya ziara ya kikazi Mkoa Katavi ambapo ametembelea gereza la mahabusu Mpanda na kuonyesha kutoridhishwa na msongamano wa mahabusu katika gereza hilo.
Akitoa taarifa kwa naibu waziri huyo Disemba 30,2020 katibu tawala wa Mkoa wa Katavi Abdallah Malela alisema tatitizo hilo linasababishwa na uwepo kwa gereza moja la kuhifadhi mahabusu la Mpanda lililojengwa tangu mwaka 1974 ikilinganishwa na ukuaji wa haraka wa Mkoa wa Katavi na ongezeko la watu hivyo kushindwa kumudu mahitaji kutokana na vitendo vya uhalifu kuongezeka.
Malela aliendelea kueleza kuwa changamoto nyingine ni ukosefu wa mahakama ya wilaya ya Tanganyika ambapo wananchi wamekuwa wanalazimika kusafiri umbali mrefu zaidi ya kilometa 130 kufuata huduma za kimahakama katika mahakama ya Wilaya Mpanda na mkoa wa Katavi.
‘’Kwa umbali huo wananchi wengi hukata tamaa kufuatilia mashauri yao au kutoa ushahidi na hivyo kuzorotesha mfumo wa haki jinai, kukosekana kwa chombo maalumu cha kusafirisha mahabusu wanaotoka mahakama za mwanzo na hivyo huwa vigumu kuhudhuria mara kwa mara wanapohitajika katika mashauri yao hali hii inawanyima watuhumiwa haki ya kesi zao kusikilizwa kwa wakati,’’ alisema Malela.
“Jiographia ya mkoa wa Katavi siyo rafiki sana Mpimbwe na Mlele kutoka Halmashauri moja kwenda Halmashauri nyingine ni zaidi ya kilometa 135 anachukuliwa mtuhumiwa kutoka Mpimbwe anapelekwa Mlele kesi yake ikimalizika analetwa huku ni zaidi ya kilometa 125, mashauri kama hayo unayakuta yapo Wilaya ya Tanganyika nako kuna umbali sawa,”alisema Pinda
Aidha, kwa upande wake Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Geophrey Mizengo Pinda baada ya kutembelea gereza la mahabusu Mpanda alisema kutokana na Mkoa wa Katavi kukua kwa kasi ameushauri uongozi wa magereza kuwa na mpango mkakati wa kuanza kujenga mahabusu mpya ya kisasa itakayokuwa msaada mkubwa na itakayokidhi mahitaji kwa sababu eneo wanalo na rasilimali watu pia wanayo.
Katika hatua nyingine Mhe. Pinda alimuagiza Mkuu wa magereza mkoa wa Katavi ahakikishe anasimamia kwa ukaribu wale wafungwa waliokaa muda mrefu katika gereza la mahabusu Mpanda wapelekwe katika gereza la kilimo Kalilankulukulu ili iwe sehemu ya mafunzo na kuongeza uzalishaji badala ya kubaki gereza la mahabusu Mpanda mjini, huku akiahidi kutoa mifuko 100 ya saruji kwa ajili kuchangia kuboresha majengo kutokana na hali aliyoshuhudia.