Na Mwandishi Wetu KTPC,Katavi.
Katika hali ya kuhakikisha wazee wa mkoa wa Katavi kuwa wanakuwa
wazima wa afya njema,Jamii imeombwa kutumia muda mwingi kuwakinga na magonjwa
ya mlipuko ya mfumo wa upumuaji (mafua na Corona) pamoja na magonjwa ya
tumbo kama vile kipindupindu na kuhara.
Hayo yalisemwa jana na Mratibu wa kukabiliana na magonjwa ya
mlipuko wa Hosptali teuli ya rufaa ya Mkoa wa Katavi alipokuwa
akizungumza na wazee wa Manispaa ya Mpanda na kuwapatia elimu ya kujikinga na
magonjwa hayo hatari.
Mratibu huyo alisema kuwa magonjwa ya mlipuko kwa wazee
hudhoofisha zaidi kinga ya mwili hivyo kuwa hatarini zaidi kushambuliwa na
magonjwa mengine nyemelezi.
Hivyo kwa sababu ya kushambuliwa na magonjwa hayo kunauwezekano
mkubwa wa kusababisha vifo kwa wazee na kupoteza rasilimali watu katika taifa.
Dkt Machibya alibainisha kuwa kunauwezekano wa kuongeza mzigo wa
utegemezi kwa kulea watoto yatima walioachwa na wazazi wao kwa kufa na magonjwa
ya mlipuko.
Licha ya magonjwa ya mlipuko kuwaathiri wazee,Hosptali teuli ya
rufaa ya mkoa wa Katavi imefanikiwa kufanya juhudi mbalimbali za kuhakikisha
wazee wanakuwa salama,ambapo wamekuwa na kitengo maalumu cha klinik za wazee
ambazo mara kwa mara hutumika kupima afya zao pamoja na kutoa elimu za
kujikinga.
Vilevile kuwaweka wazee katika kundi maalumu la msamaha wa
matibabu kama sera ya serikali inavyoelekeza.
Utoaji wa elimu endelevu wakati wa kliniki ili kuongeza ufahamu
wa wazee kujikinga na magonjwa ya mlipuko ,Kutenga vyumba maalamu vya kuwalaza
wazee na watu wengine wenye magonjwa ya mlipuko pamoja na kuaandaa ziara ya
kuwafikia wazee katika maeneo mbalimbali wanakoishi(Community outreach) ili
kuwasaidia kujikinga zaidi.
“tumeweza kuwaelimisha wazee kuhusu kanuni za afya wa
mwili,chakula na mazingira na hasa wameelewa namna ya kujikinga na
magonjwa ya Corona na Ebola na ndio maana katika kesi za wahisiwa wa Corona
hatukuwa na kesi za wazee” alisema Dkt Machibya.
Pia pamoja na mila na desturi kama za kutokutumia vyoo au
kunywa maji yasiyochemshwa,wengi wameendelea kukiri kubadilika kwenye mazoea
hayo mabaya.
“…kwakweli ninaweza kusema ni kama tumefanikiwa kwa asilimia 75
kwa wazee tuliowafika kupata huduma zetu japo sio wote tumefanikiwa
kuwafikia”alisisitiza Mratibu huyo.
Nao baadhi ya wazee waliofika kwenye kikao hicho Kulwa
Sayi,Mwabulambo Charles na Fatuma Shabain waliipongeza serikali kwa kuwajali
wazee kwa kupatiwa matibabu bure,kwani kwa kufanya hivyo kumewafanya wajione
bado wanathamani kubwa kwenye jamii.
Waliongeza kuwa jamii inawajibu wa kuendelea kuwalinda dhidi ya
magonjwa ya mlipuko kutokana na umri wao kutokuwa na uwezo wa kukabiliana na
kazi mbalimbali za kufanya usafi kwenye mazingira yanayowazunguka.