JAMBO GANI RAIS WA DRC CONGO LINAMFANYA KUPAMBANA NA KABILA


 Na Mwandishi Wetu KTPC.

Licha ya kwamba alifariki takribani miaka 60 iliyopita, Patrice Lumumba - Waziri Mkuu wa kwanza wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) baada ya Uhuru wake, anabaki kuwa mmoja wa wanasiasa mashuhuri zaidi wa taifa hilo.

Bahati mbaya pekee aliyonayo ni kwamba hakudumu madarakani kwa muda mrefu.

DRC ilipata Uhuru wake mwaka 1960 na mwaka mmoja tu baadaye maisha yake yakahitimishwa kikatili.

Nini lilikuwa kosa la Lumumba wakati ule?

Wengi wa wachambuzi wa siasa za DRC wanaamini kilichomponza ni kuonesha mapema nini anataka kuwafanyia watu wake na kipi atakifanya kwa wakoloni wa zamani.

Rais wa sasa wa DRC, Felix Tshisekedi, anaonekana kuepa kurudia kosa lililomponza mtangulizi wake huyo wa zamani.

m

Imemchukua takribani miaka miwili madarakani kuanza kufunua makucha yake na kushughulika na wale anaodhani wanatishia madaraka yake.

Wakati anaingia madaraka miaka mitatu iliyopita, Tshisekedi - kwa kiasi kikubwa, alisafiria nyota ya aliyemtangulia kwenye wadhifa huo, Joseph Kabila.

Tshisekedi hakuwa na ujanja.

Chama cha Kabila cha FCC kilipata kura nyingi na ndicho kilichoshinda viti vingi bungeni.

Katika Bunge la watu 500, FCC walipata watu 300 na chama cha Tshisekedi kilipata watu 50 tu.

Kwa wafuatiliaji wa siasa za DRC, uswahiba wa Kabila na Tshisekedi, haukuwa wa kupenda.

Kila mmoja aliuona utafaa kwa wakati huo.

Kabila hakutaka Martin Fayulu awe mbadala wake kwa sababu ya migogoro walokuwa nayo.

Kwake yeye, Tshisekedi alikuwa salama kwake na maslahi yake.

Kwa Felix, cha msingi kwake ilikuwa ni kuingia Ikulu - haijalishi anaungama na nani.

Kabila anajulikana kwa ujanja wake na ubabe wake wa kijeshi.

Tshisekedi ameishi maisha ya ukimbizi kwa muda mrefu na wengi tukitaraji kwamba itakuwa rahisi kwake kudhibitiwa na Kabila ambaye ni mzoefu wa mambo.

Baada ya Bunge kumtimua Waziri Mkuu wa DRC, Sylvester Ilunga na Bunge pia kumfukuza aliyekuwa Spika, Jeanine Mabunda - wote kutoka FCC, ni wazi kwamba sasa Tshisekedi amekabidhiwa rasmi funguo za kuongoza taifa hilo.

Wakati akitangaza uamuzi wa kujiondoa katika muungano wake wa CACH uliomwingiza madarakani, Rais Tshisekedi alidai kwamba umoja uliompa ushindi wa kishindo, uligeuka kuwa kikwazo cha utekelezaji wa majukumu yake kiutawala.

Tofauti ya Tshisekedi na Lumumba ni kwamba inaonekana huyu wa sasa alijitunza kutofungua mdomo wake mapema kuzungumza angevifanya akiwa madarakani.

Nini kimempa Rais Tshisekedi jeuri ya kuachana na Kabila sasa?

bbb

Kuelewa hili, ni muhimu walau katika hatua za mwanzo, kuielewa DRC na siasa zake. Hili ni taifa la pili kwa ukubwa barani Afrika na kubwa zaidi miongoni mwa nchi za Afrika zilizo Kusini mwa Jangwa la Sahara.

Ingawa kijiografia DRC ni taifa moja - ndani yake kuna mgawanyiko na tofauti kubwa miongoni mwa watu wake.

Kwa mfano, DRC ina takribani lugha nne zinazoweza kuitwa lugha za taifa; Kilingala, Kikongo, Kiluba, Kiswahili na Kifaransa.

Kuna maeneo ya nchi hiyo ambako lugha moja inatumika lakini nyingine hazitumiki.

Kwa hiyo, ni kete muhimu kisiasa kuonekana unaungwa mkono na watu wa maeneo tofauti.

Kwa kukubali kushiriki na Kabila, Felix aliweza kupata kuungwa huku mkono na hatimaye kufanikiwa kuingia madarakani.

Kupitia kile kinachojulikana kama Ushirikiano Mtatatifu, Tshisekedi anapata uungwaji huu mkono kutoka watu wa maeneo tofauti.

Kitendo chake cha kuwa kundi moja na Moise Katumbi na chama chake cha Ensemble pour la Democratique na kile cha Jean Pierre Bemba, kumempa watu wenye ushawishi mkubwa nje ya lugha na kabila moja.

Kwa mujibu wa mmoja wa maswahiba wake wakubwa wa kisiasa, Modeste Bahati Lukwebo, tayari sasa Tshisekedi ana wajumbe 391 ndani ya Bunge la DRC wakiwakilisha vyama tofauti 24.

Unaweza pia kusoma:

Ni wazi kwamba taratibu na nje ya macho ya wengi, Tshisekedi alikuwa akifanya makubaliano na mahasimu wake wa zamani na mara tu alipoona kazi imemalizika, ndipo sasa alikwenda kutangaza hadharani.

Hakutaka kufanya makosa yaliyofanywa na Lumumba takribani miaka 60 iliyopita.

Kama kuna jambo ambalo Tshisekedi amelionyesha kwa wengi katika sakata lake hili dhidi ya Kabila ni kwamba upole au umaamuma wa kisiasa unaoonekana usoni kwake ni changa la macho - kwamba Felix Tshisekedi ni zaidi ya anavyoonekana machoni.

Muungano Mtakatifu utadumu?

muungano

Hili ni mojawapo ya maswali ya kujiuliza. Katika siasa za DRC, hakuna ushirika unaoundwa kwa ajili ya kudumu milele. Lengo mara zote ni kupata kitu.

Ushirikiano wa Rais Mobutu Seseseko na Moise Tshombe haukudumu. Mobutu na Joseph Kasavubu haukudumu. Ushirikiano wa baba wa Kabila, na Banyamulenge haukuisha vizuri. Akina Katumbi walikuwa pamoja na Fayulu lakini sasa wamemuacha.

Tshisekedi alikuwa kundi moja na Kabila - wakati fulani FCC ikionekana kama oksijeni inayoendesha serikali ya DRC. Leo hawako pamoja tena.

Tayari kuna mambo hayaendi sawa kwenye muungano huu mpya. Bemba na Katumbi waliomba kupewa wadhifa wa Uwaziri Mkuu na Spika wa Bunge ama wao wenyewe au kupitia vyama vyao. Tshisekedi amekataa.

Yeye anataka watu wenye sifa tatu tu ndiyo wapewe nyadhifa za kuongoza vyeo vikubwa vya DRC; watu wenye utii, watu ambao hawatakuwa na ndoto za kumrithi madarakani na wale anaoweza kufanya nao kazi.

Magazeti ya DRC, kwa mfano, yameanza kubashiri kuwa pendekezo la Tshisekedi kwa nafasi ya Waziri Mkuu ni Christopher Mboso.

Kama akina Bemba wataona kwamba ndoto zao za kuja kuongoza DRC haziwezi kukamilika kupitia Muungano huu, wataachia ngazi.

Na bila shaka yoyote, Kabila atakuwa amekaa tayari kuwapokea na kutengeneza muungano wa aina nyingine utakaompa kila aliye ndani yake kile anachotaka.

Tshisekedi na AU

drc

Tangu Septemba mwaka jana, jarida la Africa Report liliripoti kuhusu namna Tshisekedi anavyojipanga kuwania Uenyekiti wa Urais wa Umoja wa Nchi za Afrika (AU).

Nafasi hiyo ilikuwa ikishikiliwa na Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa, na sasa amemaliza muda wake.

Kama atapata nafasi hiyo, Tshisekedi atakuwa ameua ndege wawili kwa jiwe moja; ataongeza kujulikana na hadhi mpya na pili itakuwa vigumu kumfanyia Mwenyekiti wa AU jambo lolote la kumwondoa madarakani kwa njia zisizo za kidemokrasia.

Changamoto kubwa kwa Rais mpya wa AU takuwa ni suala zima la ugonjwa wa Covid 19 na hasa kwenye upatikanaji wa chanjo.

Afrika yenye idadi ya watu takribani bilioni 1.2 ina uhakika wa kupata chanjo - hadi kufikia sasa, kwa asilimia 20 tu ya watu wake.

Kuna suala la mkataba wa kibiashara miongoni mwa nchi za Afrika (AfTA).

Endapo Tshisekedi atafanya ndoto hiyo kutimia, atakuwa amelifanyia bara lake jambo kubwa.

Afrika pia bado ina migogoro ya hapa na pale katika nchi tofauti. Itakuwa kazi ya Rais mpya wa Umoja wa Nchi za Afrika kupambana na changamoto hizo.

Baada ya vitendo vilivyotokea DRC katika mwezi mmoja uliopita, ni wazi sasa Felix Tshisekedi si tena mwanasiasa wa kubezwa.

Ni mgumu na uwezo wa kucheza karata zake kimyakimya na kwa umahiri mkubwa.

Chanzo ni BBC/Swahili

Ezekiel Kamwaga

  • Mchambuzi

Search This Blog

CHAGUA HABARI

Pages