
Na Walter Mguluchuma KTPC ,Sumbawanga
KITUO cha uwekezaji nchini TIC kanda ya nyanda zajuu Kusini kimewataka wakazi wa mkoa wa Rukwa kushirikiana na kituo hicho kuwatafuta na kuwashawishi wawekezaji kuwekeza mkoani humo kwani Kuna fursa nyingi,masoko na miundombinu mizuri kwaajili ya uwekezaji.


Meneja wa kituo hicho Venance Mashiba aliyasema hayo mwishoni mwa wiki wakati alipokuwa akikagua kiwanda cha nyama cha Kampuni ya SAAFI Meat Limited kilichopo katika Manispaa ya Sumbawanga mkoani Rukwa.
Alisema kuwa mkoa wa Rukwa hivi sasa umefunguka kwani serikali imejenga barabara na miundombinu mingine hali inayosaidia katika uwekezaji kwani ni rahisi kulifikia soko la nje na ndani ya mkoa huo.
Mashiba alisema kuwa pia mkoa huo una ardhi ya kutosha kwa uwekezaji, malighafi zinapatikana kirahisi nguvu kazi ipo pamoja na soko hivyo kila mwekezaji atakaye wekeza anauhakika wa kupata faida kilichopo ni wanachi wakishirikiana na serikali ili kushawoshi wawekezaji wakubwa na wadogo kuwekeza mkoani humo.
Kwaupande wake Meneja wa kiwanda cha SAAFI meat limited James Katubuka alisema kuwa kiwanda hicho awali kulikuwa kikifanya vizuri lakini baada ya kufungua mnada wa ng'ombe Kasesya imesababisha ng'ombe wengi kuuzwa nchini Zambia hivyo kiwanda kukosa malighafi.
Katubuka alisema pia wafugaji wamekuwa kupata hasara kwa kuuza ng'ombe wazima huku serikali ikipoteza mapato, tofauti na mifugo ingechinjwa katika kiwanda hicho na kuuza nyama nchi jirani kwa bei nzuri kwani kiwanda pia kingetoa ajira tofauti na sasa ambapo kimepunguza wafanyakazi kutokana na kutokuwepo kwa uzalishaji mkubwa.
Mmoja wa wakazi wa Sumbawanga mjini Epifania Adolf aliiomba serikali kutengeneza mazingira bora kwa wawekezaji kwani wamekua wakiona faida nyingi kwa baadhi ya wawekezaji waliopo mkoani humo, kwani wamekuwa wakitoa ajira, kupatikana na bidhaa wanazozalisha kwa bei naafuu pia wananufaika na wanapochangia huduma za jamii.