VIRUSI VYA CORONA RAIS SAMIA KUUNDA KAMATI.

Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ametangaza kusudio la kuunda kamati ya wataalamu watakaoshauri juu ya mustakabali wa kukabiliana na corona nchini humo.

Rais Samia amesema Tanzania haiwezi kujitenga kama kisiwa katika janga hilo la corona ambalo linaitikisa dunia kwa mwaka mmoja uliopita.

"Suala la Covid 19 nakusudia kuunda kamati ya kitaalamu. Halifai kulinyamazia bila kufanya tafiti ya kitaalamu. Watuambie upeo wa suala hili... Sio ikitajwa Tanzania basi inakuwa deshi, deshi...Hatuwezi kujitenga kama kisiwa," ameeleza rais Samia.

Rais Samia ameyasema hayo hii leo katika Ikulu ya Magogoni Jijini Dar es Salaam baada ya kuwaapisha Makatibu Wakuu wa Wizara na wakuu wa mashirika

Kiongozi huyo amesisitiza pia kamati hiyo itashauri cha kufanyika na si kufuata tu kila kilichopo duniani; "Rais Kikwete alituambia akili za kuambiwa changanya na zako....Tueleweke kama tunakubali ama kukataa Haifai kulinyamazia tu."

Kauli hiyo ya Rais Samia inadokeza uwezekano wa kubadilika kwa sera rasmi ya mapambano dhidi ya corona nchini humo.

Awali, Tanzania ilianza kwa kuchukua tahadhari za kisayansi mara baada ya kuthibitishwa kuingia virusu hivyo nchini humo katikati ya mwezi Machi mwaka jana. Hata hivyo kadri siku zilivyosogea serikali ilionekana kutochukua hatua zaidi ambazo zimekuwa zikipigiwa chapuo na Shirika la Afya Duniani (WHO) kama kuweka marufuku ya watu kutokutoka nje.

Tanzania pia iliacha kuchapisha takwimu za kila siku juu ya mwenendo wa ugonjwa huo mwaka mmoja uliopita. Mwezi Juni Mwaka jana aliyekuwa rais wa nchi hiyo Hayati John Magufuli alitangaza kuwa nchi hiyo "haina tena maambukizo ya corona kutokana na maombi ya wananchi."

Mapema mwaka huu, Magufuli pia alitangaza kutokuwa na imani na chanjo dhidi ya ugonjwa huo na kuwatahadharisha Wizara ya Afya dhidi ya kuzikimbilia, siku chache baadaye Waziri Doroth Gwajima alitangaza kuwa wizara hiyo haitaagiza chanjo hizo.

CHANZO CHA PICHA,HABARI MAELEZO

Tanzania pia imekuwa ikipigia chapuo matumizi ya tiba mbadala pamoja na kuvuta mvuke wa dawa za asili maarufu kama nyungu, japo vyote hivyo havijathibitishwa na WHO.

Mapema mwanzoni mwa mwaka huu kuliibuka hofu ya wimbi la pili la maambukizi hayo na licha ya taasisi kama Kanisa Katoliki jutoa waraka wa tahadhari na kueleza kuwa watumishi 85 wa kanisa hilo kupoteza maisha kwa kipindi cha miezi miwili wakionesha dalili zote za virusi hivyo.

'Kodi za dhuluma hapana'

Rais Samia pia ameitaka Mamlaka ya Mapato nchini Tanzania (TRA) kutokutumia mabavu katika ukusanyaji wa kodi.

Kwa mujibu wa rais Samia ukusanyaji wa kodi kwa kutumia nguvu umesababisha baadhi ya wafanyabiashara kufunga biashara zao kwa kuhofia kubambikiwa kesi za uhujumu uchumi.

"Kukusanya kodi kwa mabavu haisaidii kwa muda mrefu. Nimepewa takwimu ya zile taskforce mlizoziunda lakini haisaidii, mnawatisha watu wanalazimika kufunga biashara...Tunazitaka lakini kodi za dhuluma hapana. Kwa sababu hazitatufikisha mbali...nafahamu uamuzi huu niliochukua tutayumba kwa miezi miwili mitatu lakini baada ya muda tutarudi vizuri," amesema rais Samia.

Uhusiano wa kimataifa na uwekezaji

Katika hafla hiyo, rais Samia pia amemtaka waziri mpya wa Mambo ya Nje Bi Liberata Mulamula kuboresha mahusiano na jumuiya ya kimataifa.

"Wizara ya Mambo ya Nje mna kazi kubwa ya kwenda kukuza mahusiano na mataifa ya nje. Mhe. Waziri wewe ni hodari sana katika hili ndio maana nikaona nikuteue. Wanakusikiliza, umeshafanya kazi nao sana. Naomba twende tukaweke mahusiano mazuri na mataifa ya nje," amesema rais Samia.

Katika sekta ya uwekezaji rais amewataka mawaziri wa uwekezaji na viwanda na biashara kushirikiana katika kuweka mazingira bora ya kurejesha wawekezaji Tanzania: "Wawekezaji wakiondoka, uchumi wetu unashuka, ajira zinapungua na mzunguko wa pesa unapungua. Hiki ndio kilio kikubwa cha watanzania kuwa mifuko mitupu. Tunataka wawekezaji wafurahie mazingira mazuri Tanzania. Tunapotengeneza vikwazo tunawarudisha nyuma. Makampuni yanafungwa ndugu zangu sio uongo, yanafungwa na wawekezaji wanaondoka

Search This Blog

CHAGUA HABARI

Pages