KABURI LA MAREHEMU LAFUKULIWA SIKU MOJA BAADA YA KUZIKWA.


Wakazi wa Manispaa ya Mpanda wakishangaa kaburi la Mwili wa Marehemu Veronica Wambali aliyezikwa Desemba 26,2021 likiwa limefukuliwa


Na Walter Mguluchuma 

KATAVI

 Mwili wa   wa marehemu  Veronika Wambali (69) ambae alikuwa ni mkazi wa Mtaa wa Mji Mwema Manispaa ya Mpanda Mkoa wa Katavi aliyefariki na kuzikwa katika makaburi ya Mwangaza Manispaa ya Mpanda  kaburi lake limekutwa likiwa limefukuliwa siku moja baada ya kufanyika maziko yake .

 Tukio hilo la kusikitisha limefanywa na watu wasiofahamika alfajiri ya leo katika makaburi ya Mwangaza Manispaa ya Mpanda na kuzua taharuki kubwa kwa wakazi wa Manispaa hiyo.

Akielezea  tukio hilo Mwenyekiti wa  Mtaa wa  Mpadeco Kata ya Makanyagio  Evod Chambala alisema kuwa taarifa ya kufukuliwa kwa kaburi hilo ameipata leo Oktoba 27 majira ya saa moja kasorobo asubuhi kufuatia wananchi waliokuwa wakipita kwenye  eneo la makaburi hayo kuona kaburi likiwa wazi .

 Baada ya kupokea taarifa hizo alikwenda kwenye uongozi wa ofisi ya kata Makanyagio na kutoa taarifa kwa Jeshi  la Polisi ambao walifika kwenye eneo hilo na kukuta kaburi likiwa wazi huku ndani yake kukiwa na jeneza la mwili wa marehemu Veronika Wambali .

Chambala amesema  mawasiliano yalifanyika baina ya Jeshi la Polisi na ndugu wa marehemu ambao walifika  kwenye makaburi hayo na  kuthibitisha kuwa kaburi hilo walikuwa wamemzika ndugu yao Veronika Desemba 26,2021

 Hali hiyo ilipelekea Jeshi la Polisi kuendelea na uchunguzi wao ambapo ndani ya kaburi walikuta jeneza la mwili wa marehemu likiwa linaonekana  kutokana na kaburi hilo kuwa wazi .

 Mwenyekiti huyo wa mtaa amesema walipochunguza jeneza la mwili wa marehemu walikuta misumari iliyokuwa imewekwa kwa ajili ya kufungia jeneza la marehemu imefunguliwa lakini mwili wa marehemu ulikuwepo ndani ya jeneza hilo .

Amebainisha kuwa baada ya ndugu kujiridhisha na kufanyika mashauriano kati yao na Jeshi la Polisi mwili wa marehemu huyo ulizikwa upya kwenye kaburi hilo.


Mwili wa Marehemu Veronica Wambali ukizikwa Tena kwa Mara ya pili.


Mkwe wa Marehemu  Chifu Malack amesema kuwa marehemu huyo alifariki  hapo  Desemba 24 huko  Dares salaam ambapo alikuwa akifanyiwa  matibabu na mazishi yake yalifanyika Mpanda Desemba 26 majira ya saa kumi jioni kwenye makaburi ya Mwangaza ambapo ibada ya mazishi iliongozwa na Kateksta  Mbaruku wa Kanisa Katoliki

Ameeleza  kuwa taarifa ya kufukuliwa kwa kaburi lao wameipata majira ya saa moja asubuhi wakati walipokuwa kwenye kikao cha kifamilia kumalizia taratibu za msiba huo.

 Chifu amesema kuwa baada ya kuwa wamepokea taarifa hiyo walilazimika kusitisha kikao chao na kwenda moja kwa moja makaburini ambako walikuta kuna kundi kubwa la watu kwenye eneo la makaburi wakiwa wanashuhudia kufukuliwa kwa kaburi la ndugu yao .




Nae Mkazi wa Mji wa Mpanda Venance Majani amesema kuwa kitendo hicho kinaweza kikawa kinahusiana na imani za kishirikina au kutafuta mali kwa kudhani marehemu alizikwa na vitu  vya thamani.

Amesisitiza kuwa ni vema watu  wakaheshimu marehemu wanao kuwa wamezikwa  kwani wanastahili kuheshimiwa  na makaburi yanatakiwa kuheshimiwa.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Katavi limethibitisha kutokea kwa tukio hilo la kufukuliwa kwa kaburia la mwili wa  marehemu katika makaburi hayo ya Mwangaza  Manispaa ya Mpanda.

Search This Blog

CHAGUA HABARI

Pages