| Picha na mtandao |
Na Irene Temu
Katavi
Wazazi wameaswa kuzingatia utaratibu wa kuwanyonyesha watoto wao tangu wanapozaliwa bila kuwapa chakula au kinywaji chochote kwa afya bora ya kimwili na akili.
Mtoto anatakiwa kunyonya ndani ya saa moja mara baada ya kuzaliwa na maziwa ya mama huwa na rangi ya njano inayokuwa imebeba virutubisho vyote muhimu anavyohitaji katika miezi 6 ya mwanzo tangu kuzaliwa.
Hivyo maziwa ya Mama kuwa lishe muafaka kwa mtoto mchanga aliyezaliwa yenye uwiano mzuri wa wanga,protini,mafuta,vitamini pamoja na madini.
Kutokana na mila potofu wazazi wengi katika jamii wamekuwa wakiwanyima watoto maziwa hayo ya mwanzo kabisa kutoka yenye rangi ya njano kwa kuyakamua na kuyamwaga swala linalokwamisha watoto wachanga kupata lishe bora inayostahili kwa kusema kuwa maziwa hayo sio mazuri kwa mtoto mchanga.
Imani potofu hizo pia zimesababisha wakina mama kuogopa kunyonyesha watoto wao wakisema watanenepa kupindukia na kuwa maziwa ya mama hayawezi kumtosheleza mtoto wa umri wa miezi 0 hadi 6 na baadhi ya vyakula sio vizuri kwa mama anayenyonyesha.
Wakina mama wengine walisema mtoto mchanga anatakiwa kunywa maji mara baada ya kuzaliwa kwa kuwa maziwa ya Mama humfanya mtoto ajihisi kiu na baadhi ya wanawake hudai wanaponyonyesha matiti yao husinyaa na kudondoka.
Mratibu wa huduma za Afya ya uzazi na mtoto Mkami Makindi kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Nsimbo anasema maziwa ya kwanza ya mama kwa kitaalam huitwa colostrum na ndio maziwa muhimu zaidi kuliko maziwa yoyote yale Mama atakayokuja kuyatoa.
"maziwa ya kwanza ambayo huwa Kama chanjo ya kwanza kabisa kwa mtoto yanavirutubisho vinavyomtosheleza mtoto hadi miezi sita na pia yana kinga ambazo humsaidia mtoto kutopata maradhi huko mbeleni"alifafanua Mtaalamu Makindi
Pia alisema kuwa maziwa ya Mama yanaweza kuchangia nusu au zaidi ya nguvu za mtoto katika umri wa miaka 6 hadi 12 na kusaidia kutokuwa na uzito wa mwili wa kupindukia na hutengeneza vichocheo vya mwili(hormone) ambazo humtuliza mama na mtoto.
Vile vile unyonyeshaji wa mtoto akiwa mchanga humsaidia kuboresha uwezo wa utambuzi wa akili(IQ),mahudhurio mazuri ya shule na mapato ya juu katika maisha yake ya utu uzima.
Sambambana hayo alisema kunyonyesha kwa muda mrefu huchangia afya na maisha bora ya Mama kwani humpunguzia hatari ya kupata saratani ya mfuko wa mayai ya uzazi na matiti.
Mtaalamu wa Afya anaeleza unyonyeshaji pia husaidia kupunguza matumizi ya pesa kwa kuwa mama hana haja ya kununua maziwa ya kopo kwani maziwa yake yapo tayari kwa usafi unaotakiwa na baba anatakiwa kumsaidia mama ili maziwa yatoke vizuri kwani unyonyeshaji sio wa mama pekee.
Shirika la watoto la Save the Children linasema kuwa watoto wenye utapiamlo unaochangiwa na kutonyonyeshwa ipasavyo unakadiriwa kusababisha vifo vya watoto wachanga M 2.7 kila Mwaka.
Tafiti zimeonyesha kwamba watoto wanaotunzwa kwa maziwa ya mama bila lishe nyingine mpaka miezi sita wanaepuka hatari ya kupata maambukizi ya ugonjwa wa masikio na magonjwa mengine ya upumuaji.
Shirika la Afya Duniani (WHO) linasema Kama viwango vya kunyonyesha vingekuwa vya hali ya juu duniani takribani maisha ya watoto zaidi ya laki nane yangenusurika kila Mwaka.