Na Walter Mguluchuma
Katavi
Pamoja na jitihada kubwa zilizofanywa na Serikali za kujenga jumla ya madarasa 425 Mkoa wa Katavi yaliyotokana na fedha za Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya Uviko 19 bado Mkoa huu unakabiliwa na changamoto ya utoro wa wanafunzi kuto kwenda shule na badala yake wamekuwa wakizurura mitaani kufanya biashara za vyuma chakavu na biashara ndogo ndogo za kuuza matunda .
Hivyo jitihada kubwa zinahitajika kutatua tatizo hizo kuanzia kwa mzazi na mamlaka za Serikali vinginevyo tunajiandalia bomu la siku za baadae katika Mkoa huu.
Wakiongea na mwandishi wa habari hizi majira ya saa tano na nusu asubuhi wakiwa kwenye harakati zao kufanya biashara za vyuma chakavu mmoja wa watoto hao amesema kuwa wamekuwa wakizunguka kwenye mitaa mbalimbali ya Mji wa Manispaa ya Mpanda kutafuta vyuma chakavu na kisha kwenda kuviuza kwa mfanya biashara mmoja waliyemtaja kwa jina moja la John.
Amebainisha kuwa kilo moja ya vyuma chakavu wamekuwa wakiuza kwa bei ya shilingi mia sita na wamekuwa wakiona biashara hiyo ni ya kawaida kwani wamekuwa hawasumbuliwi na mamlaka yoyote ile ya Serikali.
Nae mtoto mwingine ambae jina limehifadhiwa amesema kuwa yeye anaishi Kawajense pamoja na wazazi wake ameona kufanya biashara hiyo ni nzuri kwa kuwa inampatia kipato.
Watoto wakiwa mtaa wa madukani na mfuko mgongoni kusaka vyuma chakavu muda wa shule |
"hakuna mtu ambae amekuwa akiniuliza kwanini nafanya biashara hii badala ya kwenda shule ni wewe tuu mwandishi ndio umeniuliza na tupo wengi tuu tunaofanya biashara hii na hasa mida ya asubuhi na jioni"alisema mtoto huyo
Nae mkazi wa Makanyagio Paulo Mathias amesema kuwa tatizo hilo la watoto wadogo kufanya biashara limekuwa sugu Mkoa wa Katavi na hasa Manispaa ya Mpanda hali inayosababishwa na wazazi kutowajibika kwa malezi ya watoto wao na mamlaka husika kutowajibika kuwachukulia adhabu watoto hao.
Hali hii imekuwa ikisababisha Mkoa wa Katavi kuendelea kuwa na idadi kubwa ya mimba za utotoni kwani watoto wakike wenye umri mdogo nao wamekuwa wakipata vishawishi wanapokuwa wakifanya biashara za matunda kama ndizi ,matango karanga na embe .
Nae Anna John ameleza kuwa swala la watoto kupata mimba za utotoni halitakwisha Mkoa wa Katavi kutokana na watoto wadogo wa kike kuruhusiwa kufanya biashara za mitaani,mbona maeneo mengine Mikoani hakuna hali kama hii au Wakuu wa Mikoa na Wilaya huwa wanatofautiana?ni swali kutoka kwa mwananchi Anna
Diwani wa Kata ya Majengo Magreti John (Kitunguru) amesema kuna shida ya utekelezaji wa zoezi hilo lipo kwa watendaji wa Mitaa na Kata kwani wamesha pewa maagizo ya kuwakamata watoto wote wanaofanya biashara za kuuza mboga za majani ,matunda na vyuma chakavu muda wa shule lakini hawafanyi hivyo.