Mstahiki Meya wa Manispaa ya Mpanda Haidary Sumry alipotembelea Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Katavi inayoendelea kujengwa na Viongozi mbalimbali wa serikali ya Mkoa pamoja na Wazee Maarufu |
Na Walter Mguluchuma
Katavi
Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Katavi kupitia mpango wa maendeleo kwa ustawi wa Taifa na mapambano dhidi ya UVIKO 19 imetengewa kiasi cha zaidi ya shilingi bilioni 8 kwa ajili ya uendeshaji wa jengo kuu la Hospitali na majengo mbalimbali pamoja na ununuzi wa kipimo cha CT Scan na Digital xray.
Hayo yameelezwa na Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Katavi Dr Yustina Tizeba wakati akitoa taarifa ya maendeleo ya ujenzi wa Hositali ya Rufaa Mkoa wa Katavi inayoendelea kujengwa na kupandishwa hadhi kuwa Hospitali ya Rufaa ya Kanda kwa Viongozi wa Madhehebu ya dini,Wazee maarufu na Viongozi wa Kimila walipokuwa wameongozana na Mkuu wa Mkoa wa Katavi Mwanamvua Mrindoko kwenye ziara ya kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa ndani ya Mkoa huo.
Alisema Serikali kupitia Wizara ya Afya na Ofisi ya Mkoa inaendelea kutekeleza mradi wa Ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Katavi kama ilivyoelekezwa na Waziri Mkuu Kasim Majaliwa alipokuwa kwenye ziara ya kikazi Mkoa wa Katavi Agost 21 mwaka jana alipotembelea Hospitali hiyo na kutoridhishwa na kasi ya ujenzi uliokuwa ukiendelea .
Amebainisha kuwa Hospitali hiyo kupitia Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Jamii wa Taifa na Mapambano dhidi ya UVIKO 19 imetenga kiasi cha jumla ya Tshs bilioni 8.5 kwa ajili ya uendelezaji wa Jengo kuu la Hospitali ambazo zimepangiwa kufanya shughuli mbali mbali kama ifuatavyo .
Ujenzi wa jengo la ICU utakaogharimu Milioni 560,Ujenzi wa Jengo la EMD milioni 300, Ununuzi wa vifaa tiba vya ICU na Emd Tsh bilioni 1.4, Ununuzi wa CT Scan na Digital Xray Tshs Bilioni 2.6, Ujenzi wa Hospitali Bilioni 3,Nyumba ya mtumishi Tshs milioni 90, mafunzo ya watumishi Tshs milioni 90,gari la kubebea wagonjwa na Utawala milioni 430.
Dr Tizeba ameeleza kuwa mpaka sasa wamepokea fedha kiasi cha Tshs Bilioni 2.6 kwa ajili ya ujenzi wa jengo la wagonjwa mahututi na jengo la wagonjwa wa dharura pamoja na vifaa vyake na kamati ya ujenzi itakaa ili kazi iweze kuanza mara moja na wanahakikisha watasimamia kwa umahiri mkubwa na kwa uzalendo ili ujenzi ukamilike kwa wakati na kwa kiwango chenye ubora.
Pia Serikali imetowa kiasi cha Tshs bilioni 5.9 kwa ajili ya matumizi ya ununuzi wa vifaa tiba kwa ajiri ya Hospitali hiyo na tayari fedha hizo zipo bohari kuu ya dawa mara tuu ujenzi utakapo kamilika itakuwa na uwezo wa kuanza kazi.
Aidha Dr Tizeba aliishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwapatia fedha za kuendeleza ujenzi wa mradi huo kwani ni imani yao mradi ukikamilika utasaidia kuboresha afya kwa wana Katavi na Taifa kwa ujumla .
Mkuu wa Mkoa wa Katavi Mwanamvua Mrindoko alisema kuwa lengo la Serikali ni kuifanya hospitali hiyo kuwa ya kisasa huku mchakato wa kuifanya kuwa ya kanda ukiendelea na haoni sababu yoyote kwa Mkandarasi Suma Jkt kushindwa kumaliza kazi kwa wakati kwani fedha zipo na nyingine zaidi ya Bilioni 5 zimeletwa hivi karibuni.
Meya wa Manispaa ya Mpanda Haidari Sumry amesema kukamilika kwa hospitali hiyo kutawasaidia wakazi wa Mkoa wa Katavi ambao walikuwa wakilazimika kwenda Hospitali za Rufaa kupatiwa matibabu na wengine kwenda kwa ajili ya vipimo .
Na pia itakuwa ni furusa kwa wakazi wa Mkoa wa Katavi kunufaika kwa kujiongezea kipato kwani kukamilika kwa Hospitali hiyo kutaongeza idadi ya watumishi na familia zao .
Nae Mwenyekiti wa Mila na Destuli Mkoa wa Katavi Michael Lusambo amezipongeza jitihada zinazofanywa na Serikali koboresha huduma za afya kwani ndio Msingi wa Maendeleo bila Afya imara Maendeleo yatakwama.