MAAFISA AFYA MKOA WA KATAVI WABADILISHANA UZOEFU WA UTEKELEZAJI WA SHUGHULI ZA AFYA NA USAFI WA MAZINGIRA MKOA WA KATAVI


Maafisa Afya Mkoa wa Katavi wakiwa katika kikao kazi cha kubadilishana uzoefu katika utekelezaji wa shughuli za Afya na usafi wa Mazingira ndani ya Mkoa wa Katavi

Na Irene Temu
Katavi

Maafisa Afya Mkoa wa Katavi wametakiwa kuzingatia ukaguzi wa Mazingira katika maeneo wanayoyasimamia na kuhimiza matumizi ya choo na maji tiririk lengo likiwa kuepuka magonjwa ya mlipuko.

Akizungumza katika kikao kazi  cha Maafisa Afya kilichofanyika Ukumbi wa Idara ya Maji Manispaa ya Mpanda Mkoa wa Katavi,Katibu Tawala Mkoa wa Katavi Rodrick Mpogolo amesema eneo la biashara ya nyama ni moja wapo ya eneo linalotakiwa kuangaliwa kwa ukaribu kwenye swala la usafi.

Mpogolo amesema walifanyie kazi swala la usafi wa nyama kuanzia kwenye machinjio na usafiri unaotumika kusafirisha nyama hiyo kuelekea buchani na katika eneo la kuuzia nyama hiyo.

Katibu  Tawala Mkoa wa Katavi Rodrick Mpogolo

"Tunalo jukumu la kufanya maana yapo maeneo ni lazima tuyafikie ili tuweze kuboresha swala la usafi lazima tuwapange wafanya biashara, bodaboda, natamani kuona nyama zinauzwa mazingira salama kuna nyama zinasafirishwa kwenye baiskeli hii sio sawa na sio nyama tu hata mikate" alisema Mpogolo.

Kwa upande wake Mganga Mkuu Mkoa wa Katavi Dr Omar Sukari amesema kwa kuhakikisha wanasimamia swala zima la usafi na afya za watu watakaa kikao kwa kushirikisha sekta mbalimbali ikiwemo Maji, Barabara,Elimu,Wakurugenzi, Wakuu wa Wilaya pamoja na makundi ya wafanya biashara.


Mganga Mkuu wa Mkoa wa Katavi Dr Omar Sukari

"Lengo la kikao tunachokifanya ni kuhakikisha tunaepuka hili gonjwa la kipindupindu na magonjwa mengine ya milipuko maana kupitia kikao hiki kila mtu atajua akasimamie eneo gani pia tutafuatilia sehemu uliotuelekeza hasa kwenye uchakataji wa swala la nyama," alisema Dr Sukari.

Kwa mujibu wa Afisa afya Mkoa wa Katavi Suzana Komba amesema kikao hicho cha Maafisa Afya ni kwaajili ya kuweka mikakati ya kuhakikisha Mkoa wa Katavi unakuwa na vyoo bora katika Halmashauri zote.

Suzana amesema wanataka kusiwepo na kaya isiyokuwa na choo bora ikiwemo kusimamia miundo mbinu ya choo katika vituo mbalimbali vya afya.


(Kushoto)Afisa Afya Mkoa wa Katavi Suzana Komba

"kila kaya kuwe na vyombo vya kunawia mikono na maji tiririka pamoja na sabuni, hiyo ndio njia bora ya kujikinga na magonjwa ya milipuko kama kipindupindu na kuharisha wanasema nyumba ni choo maisha ni kubalansi"alisema Komba.

Baadhi ya maafisa afya walioshiriki kikao hicho akiwemo Erick Kisaka Afisa afya (Manispaa ya Mpanda),Dulla Makala(Nsimbo),Ridhiwan Mohamed(Mpimbwe)na Henrick Mwasibale(Tanganyika),wamesema watayafanyiakazi maagizo yote yaliyotolewa ikiwemo kusimamia usafi kila eneo na kuwa na vyoo bora kwa kila kaya.

Maafisa Afya wa Wilaya zote za Mkoa wa Katavi wakiwa katika picha na Katibu Tawala wa Mkoa wa Katavi Rodrick Mpogolo (katikati),Mganga Mkuu wa Mkoa wa Katavi Omar Sukari (kushoto)pamoja na Afisa Afya Mkoa wa Katavi Suzana Komba (kulia)


Search This Blog

CHAGUA HABARI

Pages