Na Walter Mguluchuma
Tanganyika
Baraza la Madiwani Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika Mkoa wa Katavi limepitisha rasimu ya bajeti ya fedha kwa kipindi cha mwaka 2022/2023 kiasi cha zaidi ya shilingi Bilioni 27 ikiwa ni ongezeko la asilimia 2.06 ya bajeti ya msimu uliopita .
Akiwasilisha Rasimu ya Bajeti hiyo mbele ya Kikao cha Baraza la Madiwani Afisa Mipango wa Halmashauri ya Tanganyika Doto Kwigema alieleza kuwa bajeti hiyo imezingatia mahitaji muhimu ya Halmashauri na wananchi wa ngazi zote na mwongozo wa mpango wa bajeti.
Amebainisha kuwa kwa mwaka wa fedha 2022/ 2023 Halmashauri hiyo imepanga kutumia kiasi cha shilingi 27,157,790,000 kati ya fedha hizo mapato ya ndani ni kiasi cha shilingi Bilioni 4,931,335.
Amesema kuwa bajeti hiyo imeongezeka kutoka Tshs 26,326,111,169 Bajeti ya mwaka 2021/2022 kwa kiasi cha zaidi ya bilioni 27.1 ambayo ni sawa na asilimia 3.06
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Tanganyika Hamad Mapengo aliwasisitiza Madiwani na Watumishi wa Halmashauri hiyo kuhakikisha wanashirikiana katika kukusanya mapato ili Halmashauri iweze kuwahudumia wananchi wake na kukua zaidi.
Alisema pamoja na kuwa wamepitisha Rasimu hiyo ya Bajeti yeye kama Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo haoni kama itakuwa dhambi kukusanya mapato ya ndani zaidi ya makisio waliyoyaweka.
Diwani wa Viti Maalum Theodela Kisesa alishauri kuwa fedha ambazo zimepitishwa kwenye Rasimu hiyo ya bajeti za kupambana na afua za Ukimwi bado hazi toshi kwani tatizo hilo bado lipo kwenye Halmashauri hiyo.