Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Katavi Beda Katani akitoa mchango wake katika Ujenzi unaoendelea kwenye Shule ya Sekondari Kasansa iliyopo kata ya Maji moto Halmashauri ya Mpimbwe |
Na Irene Temu
Katavi
Kamati ya siasa ya Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Katavi kupitia Mwenyekiti wake Beda Katani wameupongeza Uongozi wa Serikali ya Mkoa wa Katavi kwa kusimamia kwa umakini na weledi mkubwa miradi ya Ujenzi wa vyumba vya madarasa katika Halmashauri ya Wilaya ya Mlele na Halmashauri ya Mpimbwe yaliyojengwa kutokana na fedha za Mapambano dhidi ya Uviko 19 kutoka IMF.
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Katavi Beda amesema kitendo Cha Halmashauri ya Mlele kukamilisha Ujenzi wa vyumba vya madarasa na kubakiza ziada ya zaidi ya shilingi Milioni 100,halijawahi kutokea hivyo inaonyesha ni namna gani serikali wamesimamia miradi hiyo kwa uaminifu wa hali ya juu.
Katika pongezi hizo aliendelea kusisitiza swala la amani na mshikamano baina ya Viongozi kuanzia ngazi za juu hadi kwenye shina lengo likiwa ni kushirikiana katika shughuli za Maendeleo kwani pasipo na maelewano Maendeleo hayawezi kupatikana.
Mwenyekiti Beda aliwataka Wenyeviti wa serikali za Mitaa kuwasomea wananchi taarifa ya mapato na matumizi ili kuondoa maswali juu ya fedha zilivyotumika na kuona kuwa mchango wao katika kuchangia Ujenzi wa miradi inayoendelea katika Halmashauri hiyo unadhaminiwa.
"wananchi wasomewe mapato na matumizi na kuonyesha ule mchango wao walioutoa wakati miradi hii inaendelea kwa kusogeza tofali,kubeba mchanga,kuchota Maji na mengineyo umedhaminiwa"alisema Mwenyekiti Beda
Mjumbe wa kamati ya siasa Mkoa wa Katavi ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa wa Katavi Mwanamvua Mrindoko katika ziara iliyoanzia Shule shikizi ya Msingi Utende iliyojengwa vyumba vya madarasa 3, Shule ya Sekondari Inyonga vyumba vya madarasa 3 na Shule ya Sekondari Ilela vyumba vya madarasa 2 katika Halmashauri ya Wilaya ya Mlele na Shule ya Sekondari Kasansa vyumba 2 pamoja na Shule ya Sekondari Mbede vyumba vya madarasa viwili katika Halmashauri ya Mpimbwe
Aliwataka wanafunzi wa Shule zote kusoma kwa bidii na kuzifikia ndoto zao kwani serikali tayari imekwisha tengeneza miundombinu mizuri ya Elimu kazi ni kwao kutulia na kusoma.
Pamoja na hayo aliwahimiza wazazi wote ambao watoto wao wamechaguliwa kujiunga kidato cha kwanza katika shule zote zilizopo ndani ya Wilaya ya Mlele na Mpimbwe kuhakikisha wanakwenda Shule kutoka na idadi ya wanafunzi waliochaguliwa kujiunga katika Shule ya Sekondari Kasansa na Mbede kutoridhisha.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mlele Teresia Irafay ameeleza kuwa Ujenzi wa vyumba vya madarasa 34 vimekamilika na walipokea jumla ya shilingi Milioni 680 huku wakibakiwa na kiasi Cha zaidi ya shilingi milioni miamoja na fedha hizo wanampango wa kujenga shule ya English medium katika Halmashauri hiyo ya Mlele ikumbukwe fedha hizo ni mkopo kutoka IMF zilizotolewa kwa ajili ya Mapambano dhidi ya Uviko 19.
HABARI PICHA