Na Irene Temu
Katavi
Wanafunzi wote waliochaguliwa kujiunga kidato cha kwanza katika shule zote za Sekondari Mkoa wa Katavi wametakiwa kuwa shuleni baada ya Mkuu wa Mkoa wa Katavi Mwanamvua Mrindoko kuondoa vigezo vya kujiunga kwa baadhi ya Shule kutoka na Mazingira.
Baadhi ya shule zimekuwa zikiagiza katika fomu za kujiunga kidato cha kwanza mwanafunzi kuripoti shuleni akiwa na panga,kwanja la kufyeka majani,rimu na mahitaji mengine kwa ajili ya usafi na kujifunzia.
Mkuu wa Mkoa wa Katavi Mwanamvua ametoa ruhusa hiyo kwa mwanafunzi yoyote aliyechaguliwa kujinga kidato cha kwanza kuripo shule hata kama bado wazazi wake hawajamnunulia sare za shule kuanza masomo na mambo mengine yatatekelezwa akiwa darasani anasoma.
Aidha amewaasa wanafunzi wote kuzingatia masomo wawapo darasani na kwa upande wa wasichana wasikubali kurubuniwa na kujiingiza katika vishawishi vitakavyopelekea kuacha masomo na kupoteza ndoto zao.
" kwa upande wa wanaume niwatake msome kwa bidii na kuacha kwenda kwenye vijiwe vya mitaani pamoja na kutazama video zinazoonyeshwa katika mabanda zisizo na maadili muache kukimbilia maisha kwa kusema nitakuwa bodaboda japo ni kazi lakini zina muda wake wakati huu ni wakusoma kwanza"aliwaasa Mkuu wa Mkoa Mrindoko
Mkuu wa Mkoa wa Katavi Mwanamvua Mrindoko |
Mrindoko ameyasema hayo katika siku ya pili ya ziara iliyoanza jana kwa kukagua miradi ya Ujenzi wa vyumba vya madarasa vilivyojengwa kutokana na mkopo wa fedha za Mapambano dhidi ya Uviko 19 zilizotolewa na IMF.
Ziara hiyo ilianzia Halmashauri ya Wilaya ya Mlele na Halmashauri ya Mpimbwe hapo jana na kamati ya siasa ya Mkoa na leo kumalizia katika Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika,Manispaa ya Mpanda pamoja na Halmashauri ya Wilaya ya Nsimbo.
Kwa upande wake Afisa Elimu Mkoa wa Katavi Dr.Baganda Elpidius aliwasisitiza wanafunzi kwenda kuwaambia mwanafunzi waliochaguliwa kujiunga kidato cha kwanza hakuna vigezo vya kujiunga Shule.
Afisa Elimu Mkoa wa Katavi Dr.Baganda Elpidius akizungumza na wanafunzi wa Shule ya Sekondari Kabungu iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika Mkoa wa Katavi |
Kwani serikali imetoa nafasi kwa mwanafunzi aliyeacha shule kutokana na sababu mbalimbali kurudi shuleni na kuendelea na masomo Ila asiwe na mimba na pia isiwe kigezo cha kushawishika kufanya mambo mabaya na kusema nitarudi Shule.
Nae Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Katavi Beda Katani aliwataka wanafunzi pamoja na Waalimu wao kutunza madarasa hayo kwa kuwa weka Safi,kuacha kuyachorachora kwani ni kwa kizazi cha sasa na kijacho.
Aliutaka uongozi wa serikali kusimamia baadhi ya vyumba vya madarasa ambavyo bado vinahitaji ukarabati kumalizika na wanafunzi kusoma kwa bidii.