Na George Mwigulu,Mpanda.
Mbunge wa Jimbo la Mpanda mjini Mkoa wa Katavi,Sebastian Kapufi amesikitishwa na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA)-Manispaa ya Mpanda kwa kasi ndogo ya utekelezaji wa ujenzi wa miradi ya miundombinu ya barabara.
Kapufi amekosoa waziwazi mwenendo mbovu wa Tarura wa ujenzi wa miradi hiyo ya maendeleo ya wananchi hapo jana katika Kata ya Airport Manispaa ya Mpanda mkoani hapo wakati wa ziara yake ya siku 5 ya kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo jimboni kwake.
Amebainisha kuwa Tarura-Manispaa ya Mpanda ina nafasi ya kukaa imara kujitafakari kwa kina namna ambavyo imekuwa sehemu ya kuzorotesha na kuwa kikwazo cha kutokukamilisha miradi ya ujenzi ya barabara kwa muda muafaka.
" kwa nafasi yangu ya kuwa mwakilishi wa wananchi siwezi kukubali mwenendo wa kuchelewesha kukamilisha miradi ya ujenzi wa barabara...wananchi wamechoshwa na jambo hilo wakati wanaambiwa fedha za miradi zipo"amesisitiza Kapufi.
Mbunge huyo alisema kuwa licha ya Tarura kukabiliwa na changamoto zao lakini inapaswa kutoa kandarasi kwa Wakandarasi waaminifu wasio kuwa na tamaa ya kushikilia miradi mingi ya ujenzi wa barabara pamoja na kuhakikisha inasimamia kwa makini ujenzi wa miradi hiyo kuwa inakamilika kwa wakati muafaka.
Kapufi alifafanua kuwa katika kata ya Kazima kwa mwaka wa fedha 2021/2022 ilipitishiwa bajeti ya kufanyiwa matengenezo barabara ya urefu wa KM 7 ambapo amedai kuwa hakuna hata km1 ambayo imetengenezwa na hii kuonesha uzembe wa Tarura.
" Tarura hata kwenye kata ya Kawajense hawajafanya lolote licha ya kutengewa Km 7 za fedha zipo ila hata moja haijatengenezwa ikiwa pamoja na barabara inayounganisha Stendi ya zamani na Mtaa wa Msufini Kata ya Uwanja wa Ndege inaenda kwa kusuasua, hali kadhalika barabara inayotoka Junction ya Kasimba Darajani kwenda shule ya Msingi Kasimba nayo inaenda kwa kusua sua" Alisema mbunge huyo.
Katika hatua nyingine Mbunge huyo ili kuhakikisha miradi jimboni kwake inakamilika ametoa jumla ya Mil 27. fedha Tsh10,000,000 kusaidia ujenzi wa Darasa moja shule ya Msingi Mkapa ili kupunguza Msongamano wa Wanafunzi,Tsh 5,000,000/- kusaidia matengenezo ya barabara inayotoka kijiji cha Shankala- kuja Mtaa wa Kapalangao Kata ya Kazima,Tsh 700,000/- Kwa ajili ya kusaidia ununuzi wa kiwanja kitakachotumika kujengea shule ya msingi Kijiji cha Shankala.
Fedha Tsh 2,000,0000 kusaidia nguvu za Wananchi katika Mradi wa Kituo cha Afya Nsemulwa,Tsh. 10,000,000/- kusaidia umaliziaji wa Madarasa shule ya Msingi Kasimba iliyopo kata ya Uwanja wa Ndege ambapo baada ya kukamilika madarasa hayo itaondoa msongamano wa wanafunzi madarasani.
Ambapo katika shule ya msingi Kasimba Manispaa ya Mpanda ametoa mil 10 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa madarasa mawili ambayo baada ya kukamilika yataweza kuondoa msogamano wa wanafunzi madarasani.
Vilevile ametoa Mil 5 katika kijiji cha Shankala,Fedha ambazo zitatumika kwenye ujenzi wa barabara ya kutoka kijijini hapo kwenda Mtaa wa Kazima ambapo barabara hiyo itaifungua zaidi Manispaa ya Mpanda ili iweze kufikika kutoka pande zote za ndani na nje ya manispaa hiyo.Huku akiahidi kuzifuatilia fedha zingine mil 3 ambazo awali alizitoa kwa ajili ya barabara hiyo na kukwama kutolewa na halmashauri pia ametoka milion 2 katika zahanati ya kata Nsemulwa.
Joel kaleman Mkazi wa kata ya Uwanja wa Ndege ametoa shukrani kwa mbunge kwa ujenzi wa daraja la mtaa wa Mbuyuni linalo unganisha kata 3 ambapo amekiri kuwa changamoto waliokuwa nayo imeondoka.
Mkazi huyo alieleza kuwa serikali bado wanaiomba kuendelea kutatua kero za wananchi ikiwa pamoja na kwenye sekta ya maji ambayo bado ni changamoto kubwa kwao.
Marry Kaboneka Mkazi wa Uwanja wa Ndege licha ya kumshukuru mbuge kwa kazi nzuri amemuomba kuzidi kuwatumikia wananchi kwa bidii zaidi ili wasijute kwa maamuzi ambayo walifanya ya kumchagua kuwa mbunge wao.
Alifafanua kuwa jukumu la mbunge ni pamoja na kuwatumikia wananchi kwa kuwaletea maendeleo ambayo ni muhimu kwa jamii yoyote yenye nia ya kuondokana na maisha duni.
Moja ya mradi wa kituo cha Afya Nsemlwa Manispaa ya Mpanda kikiwa kwenye hatua ya ujenzi,Kituo hicho kitakapo kamilika kitaondoa kero ya wananchi wa mtaa huo wanaotembea umbali mrefu kutafuta huduma za matibabu.(Picha na George Mwigulu).