Mbunge wa Jimbo la Mpanda Mjini Sebastian Kapufi wa pili kutoka kulia alipotembelea kituo Cha Afya Ilembo |
Na George Mwigulu,Mpanda.
Kituo cha Afya Ilembo Manispaa ya Mpanda Mkoa wa Katavi kimepiga hatua kubwa kwa utoaji wa huduma za afya kibingwa na kufanikiwa kwa asilimia 95 kudhibiti vifo vya mama na mtoto wakati wa kujifungua.
Yamebainishwa hayo katika kituo hicho cha afya na Mganga Mkuu wa Manispaa ya Mpanda Mkoani humo,Dkt Paul Swakala wakati wa ziara ya Mbunge wa Jimbo la Mpanda Mjini Sebastian Kapufi alipokuwa akisomewa taarifa ya mafanikio na changamoto ya kituo hicho.
Mganga Mkuu huyo ameeleza kuwa licha ya kituo cha afya Ilembo kuwa na Madaktari wanne wa ngazi ya shahada lakini wamejipambanua kwa utoaji wa huduma zao za afya kwa ubora wa kiwango cha kibingwa,jambo ambalo limekuwa kivutio kikubwa kwa watu kutoka nje ya manispaa na mkoa wenye uhitaji wa huduma za matibabu ya kiafya.
Huduma ambazo wamekuwa wakizitoa ni pamoja na upasuaji wa aina mbalimbali,huduma ya mama na mtoto pamoja na wanawake wajawazito waohitaji huduma za upasuaji ambapo kwa huduma hizo wanazozitoa kibingwa kituo cha afya Ilembo kimekuwa kikipokea rufaa za wagonjwa walioshidikana kutoka maeneo yote ya ndani na nje ya mkoa na kuokoa maisha ya wagonjwa na wanawake wajawazito.
‘’…ubora wa huduma za kibingwa unaotolewa hapa imetufanya kuwa na idadi kubwa ya wanawake wajazito wanaojifungua hapa ambapo ni wazi kuwa zaidi ya watoto 400 huzawaliwa kila mwenzi ikiwa idadi hii ni zaidi ya hosptali ya rufaa ya mkoa wa Katavi ambayo watoto zaidi ya 100 huzawali pekee” alisema Dkt Swakala.
‘’ wajibu wetu ni kutoa huduma bora zaidi baada ya kutafakari kuwa vifo vya mama na mtoto wakati wa kujifungua tukaona kuwa havikubaliki tena kwenye jamii yetu,Ni aibu na haifai kuona vifo kwani suala la mama kuwa mjamzito sio mateso na adhabu ya kifo” amesisitiza Mganga Mkuu.
Aidha amebainisha kuwa changamoto zinazokabili kituo hicho ni kukosekana kwa wigo wa ukuta unaozunguka kituo cha afya,Uhaba wa wodi za wagonjwa hasa wodi ya kinababa pamoja na vitanda vyake na kukosekana kwa jenereta kubwa ya kufua umeme haraka pindi umeme wa grade ya taifa unapokatika.
‘’ kukosekana kwa jenereta kubwa la kufua umeme ni hatari sana,kwani hapa tunafanya upasuaji wa aina mbalimbali laikini tunasehemu ya kukuzia watoto ambao wamezaliwa kabla ya wakati (Njiti) ambapo wanahitaji sana huduma hiyo” aliongeza Dkt Swakala.
Hivyo alimwomba mbunge wa jimbo la Mpanda Mjini kwa kushirikiana na serikali na wadau mbalimbali wa afya kutatua kero hizo ambazo zinaweza kuzorotesha ufanisi wa kazi.
Mratibu wa afya ya uzazi na mtoto Manispaa ya Mpanda Muna Sumury alisema kuwa kituo cha afya Ilembo kwa Takwimu kuanzia mwenzi January hadi June mwaka huu walikuwa na idadi ya vifo vitatu vya wanawake wajawazito ambapo kwa kuanzia mwenzi June hadi Desember hakuna kifo chochote cha mama mjamzito.
Ameeleza kuwa mikakati waliyo nayo ni pamoja na kutolala hadi pale mama na mtoto wanapokuwa salama baada ya kujifungua hivyo tunafanya kwa umoja hasa pale tunapopokea pia rufaa ya akina mama kutoka wilaya ya Tanganyika,Mlele na nje ya mkoa.
Mbunge wa Jimbo la Mpanda Mjini Mkoa wa Katavi licha ya kuwapongeza wataalamu wa afya kwa kazi nzuri amesema kuwa changamoto hizo amezipokea,na kama mwakilishi wa wananchi atazishughulikia haraka kwa masilahi ya jamii.
Kapufi ameeleza kuwa kituo hicho kinapaswa kuwa mfano wa vituo vingine vya afya kuiga kazi nzuri inayofanywa kwa ajili ya kuokoa maisha ya watu.