Na Walter Mguluchuma
Aliwasisitiza wanafunzi chuoni hapo kusoma kwa makini na uadilifu mkubwa wakiwa chuoni na nje ya chuo wasitake kufaulu kwa kutumia njia ya ujanja kwani taaluma yao inagusa uhai wa binadamu.
Katavi
Shirika la Christian Social Services Commission(CSSC) kwa kushirikiana na shirika la Action Medeor la Nchini Ujerumani wamekabidhi maabara ya kisasa na darasa lenye uwezo wa kubeba wanafunzi 102 kwenye Chuo cha Afya na Sayansi Shirikishi Mpanda Mkoa wa Katavi .
Makabidhiano hayo yamefanyika kwenye chuo hicho kilichopo Manispaa ya Mpanda ambapo mgeni rasmi alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Katavi Mwanamvua Mrindoko .
Akizungumza kwenye makabidhiano hayo Mkurugenzi wa Huduma za afya wa CSSC Josephine Balati alisema miundo mbinu ya darasa hilo imefadhiliwa na kampuni ya madawa ya nchini Ujerumani iitwayo Saitomius na ni matokeo ya majadiliano yaliofanyika Kati ya wadau wa famasia katika kutatua changamoto zinazoikabili sekta ya famasia Tanzania kupitia mradi wa MAP/ITRAP.
Mradi huu unatekelezwa Nchini Tanzania na Shirika la Christian Social Services Commission kwa kushirikiana na Action Medeor na Baraza la wafamasia Tanzania (pst) lengo likiwa kuboresha elimu ya famasia nchini.
Dkt Balati ameeleza kuwa miundo mbinu waliyoboresha kwenye chuo hicho ni ujenzi wa darasa moja la kisasa lenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 102 kwa wakati mmoja lililo jengwa kwa kufuata miongozo ya Wizara ya Afya na limegharimu zaidi ya shilingi milioni 150.
Amebainisha kuwa darasa hili walilo kabidhi limechochea uanzishwaji wa kitivo cha elimu ya famasia ngazi ya cheti na stashahada kwa mara ya kwanza kwenye chuo hicho kilichoanza kupokea wanafunzi wa famasia mwezi novemba 2020.
Pia wamekabidhi maabara iliyokarabatiwa yenye uwezo wa kuruhusu wanafunzi 25 kujifunza kwa vitendo kwa wakati mmoja maabara hii imejengwa kwa kuzingatia viwango vya ubora wa baraza la mafamasia nchini.
"wanafunzi wa famasia 50 waliodahiliwa chuoni hapa mwaka 2020 wameanza kutumia tayari maabara hii ambayo imegharimu kiasi cha zaidi ya shilingi milioni 70 na kufadhiliwa na Serikali ya Ujerumani kipitia BMZ.
Dkt Balati ameeleza pia mradi huo umechangia juhudi zilizoanzishwa na Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Afya ya kuboresha mazingira ya vyuo vya afya na kuongeza vyuo vinavyotowa elimu ya ufamasia nchini.
Mkuu wa Mkoa wa Katavi Mwanamvua Mrindoko aliyashukuru mashirika hayo ya dini kwa mchango huu kwani wamefanya kazi ambayo Serikali inafanya ya kuwahudumia wananchi.
Aliwasisitiza wanafunzi chuoni hapo kusoma kwa makini na uadilifu mkubwa wakiwa chuoni na nje ya chuo wasitake kufaulu kwa kutumia njia ya ujanja kwani taaluma yao inagusa uhai wa binadamu.
Nae Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Mpanda Euzebius Nzigilwa akiongea kwa niaba ya mashirika hayo alisema kazi yao ya kwanza ni kutowa huduma kwa watu ya kiroho na kumkomboa mtu kiroho,kimwili pamoja na akili.
Aidha alieleza pia wanawajibu wa kutowa huduma kwenye jamii kama vile elimu, maji,afya,kulea wazee wasio jiweza na watoto yatima yote hayo ni katika kumweka binadamu katika ustawi bora wa maisha.
Mkuu wa Chuo cha Afya Mpanda Lightness Michael alishukuru kwa Chuo hicho kukabidhiwa darasa na maabara na kubainisha bado Chuo kinakabiliwa na changamoto ya miundo mbinu ya majengo ya madarasa,ofisi na mabweni .