Na Walter Mguluchuma
Katavi
Viongozi wa madhehebu mbalimbali ya Dini,Wazee maarufu na vyama vya siasa Mkoani Katavi wamefurahishwa na hatua ya Serikali ya Mkoa kuwashirikisha kukagua miradi iliyotekelezwa kutokana na fedha za Uviko 19 na miamala ya tozo mbalimbali za mashirika ya simu.
Kauli hiyo wameitolewa wakati wa ziara waliyoifanya ya kutembelea miradi mbalimbali ya vyumba vya madarasa,mabweni,vituo vya afya pamoja na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa inayojengwa eneo la Rungwa ziara iliyoandaliwa na ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Katavi kwa ajili ya kuona jinsi fedha za uviko 19 na tozo za miamala ya simu zilivyotumika katika kutekeleza miradi ya maendeleo Mkoa wa Katavi.
Akizungumza wakati wa ziara ya kutembelea miradi hiyo Mwenyekiti wa Wazee Mkoa wa Katavi Thomasi Ngozi ameeleza kuwa ni mara ya kwanza kundi hilo kushirikishwa katika ziara ya kutembelea miradi iliyotekelezwa na inayoendelea kutekelezwa katika Mkoa.
"haya ni mapinduzi makubwa yaliyofanyika katika kuleta maendeleo kwani tumeweza kujionea wenyewe jinsi ambavyo miradi ya fedha za uviko 19 na fedha za miamala ilivyoweza kutekelezwa kwa ustadi mkubwa katika Mkoa "alisema Mzee Ngozi
Nae Mzee Vicenti Nkana alisema kuwa Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa muwazi kwa kuwaambia wananchi kila Serikali inapokopa fedha kutoka kwa wahisani na malengo ya kukopa fedha hizo tofauti na ilivyokuwa hapo awali .
Mwenyekiti wa Mila na Desturi Mkoa wa Katavi Michael Lusambo hakusita kumwombea Rais Samia asikate tamaa kwa kazi anazozifanya na Mungu azidi kumtia shime kwa kazi anazoendelea kuzifanya.
Mkuu wa Mkoa wa Katavi Mwanamvua Mrindoko nae alieleza kuwa Mkoa wa Katavi hadi sasa umeisha pokea zaidi ya shilingi bilioni 33 kwa ajili ya miradi mbalimbali ya maendeleo ambayo ni vyumba 425 vya madarasa ambayo yamekamilika kwa asilimia 100, ujenzi wa barabara , Hospitali ya Rufaa ya Mkoa,Hospitali za Wilaya na vituo vya afya
Mwenyekiti wa Chama cha ACT Wazalendo Mkoa wa Katavi Joseph Mona alieleza kuwa nia ya Rais kuleta fedha Mkoa wa Katavi ni njema hivyo ni vema watu waliopewa jukumu la kusimamia miradi hiyo wakalifanya kwa uadilifu mkubwa na uaminifu.
Nae Meya wa Manispaa ya Mpanda Haidary Sumry amebainisha kuwa miradi hiyo imekuwa ni chachu ya maendeleo katika Mkoa na imetowa ajiri kubwa kwa vijana wa Mkoa wa Katavi.