MKAZI WA KIJIJI CHA MTISI MKOA WA KATAVI AUAWA KIKATILI BAADA YA KUTUHUMIWA KUUWA KWA RADI ALIYOTENGENEZA



Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Katavi,ACP Ali Hamad Makame

Na Walter  Mguluchuma

     Katavi

Mtu mmoja mkazi wa  Kijiji cha  Mtisi  Kata ya Sitalike Wilaya ya  Mpanda  Mkoa wa Katavi aliyefahamika kwa jina la Baraka  Said Kabisu (30) ameuawa kikatili  kwa kupigwa  na silaha za jadi na kitu chenye  uzito mkubwa  na ncha kali  na kundi la watu  wenye hasira kali baada ya kutuhumiwa kwa ushirikina wa kutengeneza radi iliyompiga Angelina  Levocatus Kifua(16) Mkazi wa Kijiji hicho .

Kwa mujibu wa  Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Katavi Ali Hamad Makame amesema tukio hilo la mauwaji limetokea January 24 majira ya saa 12 jioni kijijini hapo baada ya taarifa za kifo cha Angelina kuwafika majira ya saa kumi na mbili jioni Kijiji hapo.

Ndipo kundi kubwa la wananchi lilijikusanya huku wakiwa na silaha mbalimbali za jadi na baada ya kuwa wamekunyika kundi hilo liliamua kwenda nyumbani kwa marehemu huyo kwa lengo la kumshambulia kwa kumtuhumu kuwa ni mchawi aliyetengeneza radi iliyompiga na kumuuwa mwanakijiji mwenzao .

Kamanda amesema kuwa  baada ya kuwa wamefika nyumbani kwake walimshambulia sehemu mbalimbali za mwili wake kwa silaha za jadi na kupelekea kifo chake ambapo walimpiga kwenye paji la uso na kisogoni.

Wananchi hao baada ya kuwa wamefanya mauwaji hayo ya kikatili kwa marehemu huyo waliyemtuhumu kuwa mchawi aliyetengeneza radi iliyouwa mwanakijiji mwenzao walitokomea kusikojulikana.

Aidha Kamanda ameeleza kuwa watuhumiwa nane  wa tukio hilo tayari wamekamatwa na wanaendelea kuwahoji na wengine ambao watatajwa kuhusika na mauwa hayo wataendelea kuwa kamata na uchunguzi utakapo kamilika hatua za kisheria zitachukuliwa juu yao.

Kamanda Makame ametowa wito kwa wananchi wa Mkoa wa Katavi kuacha tabia ya kuamini mambo ya kishirikina kwani kuna mambo mengine  yanayotokea uasili wake ni ya kimungu  wala sio ya kibinadamu  yapo mambo ya kimungu wamwachie mungu mwenyewe.

Amesisitiza Jeshi la Polisi wataendelea kuwakamata watu wote wanao kiuka taratibu za sheria ya nchi kwani kila  mtu ana haki ya kuishi na kuendesha maisha yake kwa kuzingatia kanuni na taratibu hizo.

 

Search This Blog

CHAGUA HABARI

Pages