Naibu Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Katavi Faustine Maijo |
Na Walter Mguluchuma
Katavi
Katika kipindi cha Oktoba hadi Disemba,2021 Takukuru Mkoa wa Katavi wamefanya ufuatiliaji wa fedha za utekelezaji wa miradi ya Maendeleo yenye jumla ya zaidi ya shilingi milioni 67.
Hayo yameelezwa na Naibu Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Katavi Faustine Maijo wakati akitoa taarifa mbele ya Waandishi wa Habari juu ya Utendaji kazi wa Taasisi hiyo kwa kipindi cha miezi mitatu iliyopita .
Amebainisha kuwa katika kipindi cha miezi hiyo mitatu Takukuru Mkoa wa Katavi wamefuatilia miradi ya maendeleo yenye thamani ya shilingi 67,500,000.
Ambapo ameitaja miradi hiyo ni umaliziaji wa madarasa mawili katika shule ya Msingi Shikizi Halmashauri ya Manispaa ya Mpanda wenye thamani ya Tsh 25,000,000, Umaliziaji wa madarasa mawili katika shule ya Msingi Misunkumilo wenye thamani ya sh,2,500,000.
Na ujenzi wa madarasa mawili na ofisi moja ya walimu katika shule ya msingi Igalula Halmashauri ya Tanganyika wenye thamani ya Tshs 40,000,000.
Maijo amesema lengo la ufuatiliaji huo ni kuangalia iwapo kuna mianya ya rushwa kwenye utekelezaji wa miradi na kuongeza uwazi na upatikanaji wa thamani ya fedha kwenye miradi ya serikali ili kuboresha huduma kwenye shughuli za serikali .
Amefafanua kuwa mapungufu machache yaliyobainika katika ukaguzi wa miradi hiyo yangeweza kusababisha mianya ya rushwa lakini wameyafanyia kazi kwa kufanya vikao na wadau wa miradi husika pamoja na kuwapa elimu kwa lengo la kuondoa mianya hiyo ya rushwa .
"elimu hii itasaidia katika kuimarisha usimamizi wa miradi kwa kusisitiza uzingatiaji wa sheria na kanuni za manunuzi ya umma ili kupata miradi bora yenye kukidhi thamani ya fedha"alisisitiza Maijo
Aidha katika hatua nyingine Takukuru wameweza kufuatilia utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa vyumba vya madarasa ya shule za sekondari na vituo shikizi namba 5441 chini ya mpango wa maendeleo na Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya UVIKO 19 kupitia mpango huo Halmashauri ya Wilaya ya Mlele ilipokea jumla ya Tshs 680,000,000.
Katika kusimamia mradi huo Mkuu wa Mkoa wa Katavi Mwanamvua Mrindoko aliunda timu za ufuatiliaji katika Halmashauri ya Mlele ikiongozwa na Naibu mkuu wa Takukuru Mkoa wa Katavi Faustine Maijo .
Mkuu wa Mkoa wa Katavi Mwanamvua Mrindoko |
Timu hiyo iliweza kufuatilia ujenzi wa vyumba 34 vya madarasa , madawati 360, meza 433, na viti 412 ambapo jumla ya kiasi cha Tsh,100,724,838 timu hiyo iliweza kuokoa na kupelekea Mkuu wa Wilaya ya Mlele Filiberto Sanga kumtunuku Naibu Mkuu wa Takukuru Cheti cha usimamizi bora .
Mkuu wa Wilaya ya Mlele Filberto Sanga |
Pia kwenye kipindi cha miezi mitatu Takukuru wameweza kupokea jumla ya malalamiko 51 huku Tamisemi na Amcos zikiwa zinaongoza kwa kulalamikiwa.