NMB YATOWA SAMANI ZENYE THAMANI YA SHILINGI MILIONI 10 CHUO CHA AFYA MPANDA

 


Meneja wa Benki ya NMB Kanda ya Magharibi Sospeter Magese(kushoto) akimkabidhi Mkuu wa Mkoa wa Katavi Mwanamvua Mrindoko(kulia) kiti kimoja kikiwakilisha viti 100 na meza 100 zilizotolewa na Benki hiyo katika Chuo Cha Afya Mpanda Mkoa wa Katavi


Na Walter Mguluchuma

      Mpanda

Benki ya NMB Tawi la Mpanda Mkoa wa Katavi imetowa viti mia moja na meza mia moja zenye thamani ya shilingi milioni 10 kwa Chuo cha Afya Mpanda ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono jitihada zinazofanywa na Serikali kuboresha miundo mbinu ya sekta ya Afya na Elimu hapa nchini.

Msaada huo umekabidhiwa na Meneja wa Nmb Kanda ya Magharibi Sospeter Magese kwa niaba ya benki ya Nmb katika hafla iliyofanyika katika chuo hicho kilichopo Manispaa ya Mpanda Mkoa wa Katavi

Akikabidhi  samani hizo Meneja wa NMB Kanda ya Magharibi Sospeter Magese amesema wao kama benki ya Nmb wamekuwa na utamaduni wa kutenga asilimia moja ya faida ya mapato yao kwa ajili ya kusaidia jamii katika sekta mbalimbali hasa za elimu na afya .

Magese amebainisha kuwa benki ya NMB huwa inatoa kipaumbele cha misaada yake katika sekta ya elimu na afya zaidi hapa nchini.

Hivyo utaratibu waliojiwekea ni kuwa wadau wakubwa wa maendeleo kwa kusaidia huduma za afya na elimu ili kuiunga mkono Serikali katika jitihada wanazo zifanya za uboreshaji wa miundo mbinu ya elimu na afya .


Baadhi ya Wanafunzi wa Chuo Cha Afya Mpanda wakiwa katika darasa lililo na meza pamoja na viti kutoka Benki ya NMB wakifuatilia kwa makini somo linaloendelea kwa furaha na umakini mkubwa

Aidha alisema kuwa katika hatua nyingine benki hiyo kwa sasa imeanza kutoa mikopo kwa wakulima na wafanyabiashara wa mazao ya kilimo hivyo kwa wale wenye sifa za kukopesheka wachukue mikopo hiyo ili waweze kukuza uchumi wao .

Alisema kuwa NMB ndio benki kubwa kuliko benki zote zilizopo hapa nchini na ndio maana wanafika kila sehemu alipo mwananchi kwa ajili ya utoaji wa huduma za kibenki na kwa Mkoa wa Katavi kwa sasa wanatowa huduma kwenye Wilaya zote na huku kukiwa na mawakala zaidi ya mia tatu.

Mkuu wa Mkoa wa Katavi Mwanamvua Mrindoko alishukuru kwa msaada huo na kusema utasaidia sana kuwafanya wanafunzi wa chuo hicho kusoma huku wakiwa wamekaa katika mazingira mazuri ya kujifunzia .

Pia aliomba Benki hiyo iendelee kushirikiana na Serikali katika kutatua changamoto zitakazokuwa zimejitokeza katika kusaidia jamii ya wananchi wa Mkoa wa Katavi .

Nae Mkuu wa Chuo hicho Lightness Michael aliomba msaada kama huo uendelee kutolewa chuoni hapo kwani bado wanakabiliwa na changamoto ya uchache wa vyumba vya madarasa kwani madarasa yakiwa mengi na udahili wa wanafunzi utaongezeka chuoni hapo.

Mkuu wa Mkoa wa Katavi Mwanamvua Mrindoko akiwa kwenye chumba cha Darasa akiangali viti 100 na meza 100 zilizotolewa na Benki ya NMB kwa ajili ya Chuo cha Afya  Mpanda ambavyo vimegharimu kiasi cha shilingi milioni 10 miongoni mwa walioshudia makabidhiano hayo ni  Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Mpanda Askofu Euzebius Nzigirwa(Picha na Walter Mguluchuma)


 


 

Search This Blog

CHAGUA HABARI

Pages