Katavi
Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya TCB Sabasaba Moshingi amewahakikishia wajasiriamali na wastaafu huduma Bora za mikopo kutoka Benki hiyo na riba rafiki isiyoumiza ili kuweza kujiendeleza kimaisha na katika biashara zao.
Picha ya pamoja Uongozi wa Serikali ya Mkoa wa Katavi na Uongozi wa Benki ya TCB
Akiongea mbele ya Mgeni rasmi Mkuu wa Mkoa wa Katavi Mwanamvua Mrindoko katika hafla ya uzinduzi wa Tawi la Mpanda ,Mtendaji wa Benki ya TCB Moshingi amesema kuwa Benki hiyo imekuwa ikitoa mikopo kwa wastaafu ambao hakuna mtu anayeweza kuwaamini na kuwakopesha.
Lakini wao Benki ya TCB wamekuwa wakiwaamini na kuwakopesha na wamekuwa wakikopa na kurejesha bila shida yoyote na endapo mstaafu atafariki Benki hiyo itafuta mkopo huo kwa kuwa akikopa wanakata kwenye kiinua mgongo chake(pensheni).
Aidha kwa upande wa matawi Moshingi alisema kuwa awali walikuwa na matawi 32 lakini kwa sasa wana matawi 82 na wanategemea kwenda kufungua Tawi Kigamboni Dar es salaam,Mbinga Mkoa wa Ruvuma na Bukoba Mkoa wa Kagera na ni miongoni mwa Benki saba zenye faida hapa nchini.
Katika hotuba yake Moshingi hakusita kuwashukuru wateja wote wanaopata huduma katika Benki ya TCB Mpanda na kuwahakikishia huduma Bora na nzuri huku akiwapongeza wakinamama kwa uaminifu katika kurejesha Mikopo wanayochukua.
"niwaponge sana akinamama wamekuwa waaminifu sana wakikopa wanarudisha kwa wakati,Mwaka 2018 Benki ya TCB iliyokuwa ikiitwa TPB iliunganishwa na Benki ya Wananawake na kuna dirisha maalum kwa ajili ya akina mama na Benki ya TCB imetoa mkopo kwa akina mama wenye thamani ya Bilioni 127 hivyo Wakina mama Mkoa wa Katavi wajitokeze kuchukua mikopo katika benki yao ya Kibiashara Tanzania."aliwahimiza Moshingi
Mgeni rasmi Mkuu wa Mkoa wa Katavi Mwanamvua Mrindoko aliwapongeza uongozi wa Benki ya TCB kwa kuwekeza katika Mkoa wa Katavi kwani wanachangia katika kuinua uchumi wa Mkoa wa katavi na kipato cha mtu mmoja mmoja katika familia.
Pia aliwataka kutoa huduma Bora na zilizotukuka zenye usawa kwa makundi yote waliopo vijiini na mijini waendelee kuwapa elimu ya kutumia huduma za Benki ya Biashara.
Mkuu wa Mkoa Mwanamvua aliwahakikishia shughuli zao za kibenki watazifanya katika hali ya usalama ili kuwawezesha waweze kufanya kazi katika Mazingira mazuri yatakayowafanya wawahudumie wananchi kwa kiwango bora.
Nae Mkurugenzi wa Tehama na Uendeshaji Matawi katika Benki hiyo ya TCB Jema Msuya aliushukuru Uongozi wa Mkoa wa Katavi kupitia Mkuu wa Mkoa Mwanamvua kwa kukubali ombi la Benki hiyo kuungana nao katika uzinduzi huo na kusema kuwa Tawi la Mpanda limekuwa Tawi la 82 kuzindulia.