Rais Mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Nne Dr Jakaya Mrisho Kikwete(kulia) |
Na Walter Mguluchuma
Katavi
Rais Mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Nne Dkt Jakaya Mrisho Kikwete ambae ni Mjumbe wa Bodi ya Shirika la Kimataifala la AGRA linalojishughulisha na kuinua hali ya kilimo cha wakulima wadogo ili wazalishe chakula zaidi na kuangalia usalama wa chakula wa nchi za Afrika ikiwemo Tanzania ameshauri vyama vya Msingi Amcos kuimarishwa ili kuweze kusaidia upatikanaji wa masoko ya uhakika kwa wakulima .
Ushauri huu ameutowa kwa wakati tofauti alipokuwa akiongea na wakulima wadogo wa Wilaya ya Mpanda,Mlele na Tanganyika wakati wa ziara yake katika Mkoa wa Katavi ya kutembelea miradi mbalimbali inayotekelezwa na Shirika hilo la AGRA.
Amebainisha kuwa hali ya masoko ya wakulima kwa sasa hapa nchini imetetereka hivyo ni vema ikaonekana namna bora ya kujiimarisha vyama vya msingi vya wakulima ili kuweza kusaidia wakulima .
Dkt Kikwete ameeleza kuwa vyama vya msingi endapo vitaimarishwa vitasaidia sana kutafuta masoko ya kuuza mazao ya wakulima wao kwenye vyama vyao kwani Amcos zikiwa imara hata urahisi wa kupata masoko utakuwepo kuliko ilivyo sasa ambapo Amcos nyingi hazipo imara.
"vyama vingi vya Ushirika vimekuwa havifanyi vizuri kutokana na aina ya viongozi ambao wamekuwa wakiviongoza kwani baadhi yao wamekuwa sio waaminifu na nakumbuka wakati wa utawala wangu Serikali ililazimika kulipa kwenye mabenki madeni yote ya vyama vya ushirika hivyi sipendi tena vyama vifikie kwenye hali hiyo"alisema Dkt Kikwete
Amebainisha pia kuna haja ya Wizara ya Kilimo kuangalia namna ya kuweka mpango wa kutowa ruzuku kwa wakulima kwani kwa sasa wakulima wengi ndio imekuwa kilio chao ingawa hapo nyuma serikali iliwahi kutowa ruzuku kwa wakulima kwenye pembejeo kupitia mawakala waaminifu hivyo inatakiwa kuwepo na njia bora zaidi kuliko ya awali.
Dkt Kikwete amesema kuwa ziara aliyoifanya haina uhusiano na Urais mstaafu kwani Tanzania hakuna kazi ya Rais Mstaafu yeye amefanya ziara kama Mjumbe wa bodi ya shirika la Kimataifa la AGRA.
Naibu Waziri wa Kilimo Antony Mavunde ameeleza kuwa Serikali imerahisisha utaratibu wa utowaji wa vibali vya kusafirishia mazao nje ya nchi ambapo hata mwananchi wa kijijini anaweza kuomba kibali akiwa kijijini kwake kwani vibali hivyo vinatolewa kwa njia ya mtandao.
Amesema kuwa katika kuimarisha soko la kuuzia mazao nje ya nchi serikali imeweka vituo vya kufikishia mazao ya wakulima wanao safirisha mazao yao nje ya nchi na tayari wanavituo katika nchi za Sudani ya kusini katika mji wa JUBA na Lugumbashi nchini Congo.
Nae Meneja wa kiwanda cha kusindika mazao ya nafaka cha Flamingo Food Company Ltd kilichoko Kata ya Majimoto Halmashauri ya Mpimbwe Justine Mpangala amesema Kampuni ya Flamingo ilifanikiwa kuongeza kipato cha wakulima kwa kununua wastani wa Tani Elfu moja za Mpunga na kutoa Ajira kwa wananchi baada ya kupata Ufadhili kutoka AGRA hivyo kusaidia kuinua uchumi wa nchi na familia pia.
Aidha Mpangala amesema wanamshukuru Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuimarisha mazingira ya kazi za uwekezaji katika sekta ya Viwanda na Kilimo kwenye maeneo mbalimbali hapa nchini.