Na Walter Mguluchuma
Katavi
Serikali kwa kupitia Wizara ya kilimo imepanga kuwapatia maafisa ugani wote nchini vifaa vya kupimia ubora wa udongo,pikipiki 2000 na elimu itakayo wasaidia wakulima wadogo na wakubwa kuweza kulima kilimo bora na cha kisasa kitakacho wasaidia kuongeza tija katika uzalishaji wa mazao na kukuza uchumi wao na kuongeza pato la Taifa .
Kauli hiyo ya Serikali imetolewa na Naibu Waziri wa Kilimo Antony Mavunde wakati alipokuwa akiongea na wananchi wa Halmashauri ya Mpimbwe wakati wa ziara ya Mjumbe wa Bodi ya Shirika la Kimataifa la AGRA linalojishughulisha kuinua hali ya wakulima wadogo wadogo wa Afrika ikiwemo na Tanzania Rais Mstaafu wa awamu ya nne Dr Jakaya Kikwete alipokuwa akifanya ziara katika Mkoa wa Katavi kuangalia utendaji kazi unaofanywa na shirika hilo aliyekuwa ameambatana na Naibu Waziri wa kilimo .
Alisema Serikali imedhamiria kuwapatia maafisa ugani wote hapa nchini elimu ambayo itawajengea uwezo wa kutoa elimu kwa wakulima ili waweze kulima kilimo bora cha kisasa na kuzalisha mazao yao ziada.
Amebainisha kuwa wamepanga kuwapatia maafisa ugani wote vipimo vya kupimia ubora wa udongo ili waweze kuwasaidia wakulima kujua ubora wa udongo kwenye maeneo yao wanayolima na kuwafanya wawe na uhakika wa eneo wanalo lima lina hitaji nini.
Naibu waziri Mavunde amesema kuwa Serikali inaupungufu wa Maafisa ugani katika mikoa yote hapa nchini kwani kuna uhitaji wa Maafisa ugani Elfu ishirini lakini waliopo sasa hawazidi elfu sita na mia tano .
Hivyo kwa kutambua umuhimu wa sekta ya kilimo Wizara imenunua pikipiki 2000 kwa ajili ya kuwapatia Maafisa Ugani kwenye Mikoa yote na kwakuzingatia maeneo yenye uzalishaji mkubwa ili kuwarahisishia Maafisa ugani kufikia wakulima kwa urahisi.
Rais Mstaafu wa awamu ya nne ambae ni Mjumbe wa Shirika la Kimataifa la AGRA Dr Jakaya Kikwete amesema kuwa shirika la Agra ni shirika la Kimataifa na lilianzishwa na aliyekuwa Katibu Mkuu wa umoja wa Mataifa Kofi Anani.
Alifafanua kuwa shirika hilo ni la kimataifa na shabaha yake kubwa ni kuleta mageuzi ya kilimo kwa wakulima wadogo wa Afrika ikiwemo na Tanzania ili kumfanya mkulima mdogo aweze kulima kilimo bora cha kisasa na chenye tija ili mkulima aweze kupata mazao mengi na aweze kuongeza kipato chake na aweze kubadili maisha yake na kukuza uchumi wa nchi.
Dr Kikwete amesema kuwa hakuna nchi inayopiga hatua katika uzalishaji wa mazao ya kilimo bila kuwepo kwa mchango wa wakulima wadogo na ndio maana AGRA kwa kutambua umuhimu wao wameamua kuwasaidia wakulima wadogo na wala sio wakulima wakati na wakubwa.
Amesema shirika hilo kwa Mkoa wa Katavi wamefanya ukarabati wa maghala 17 ya kuhifadhia mazao na wamejenga maghala mapya mawili lengo ikiwa ni kumfanya mkulima awe na sehemu ya kuhifadhia mazao na sehemu ya kuuzia na wamekuwa wakiwasaidia wakulima kupata mbegu bora na pembejeo za kilimo .
Makamu wa Rais wa AGRA Agy Konde ameeleza kuwa hali ya uzalishaji wa mkulima mdogo wa Tanzania bado upo chini tofauti na nchi ya Ephiopia ambao wao Ekari moja wanazalisha tani saba za mahindi wakati Tanzania wanazalisha tani mbili .
Nae Mkuu wa Mkoa wa Katavi Mwanamvua Mrindoko alisema AGRA wamekuwa na mchango mkubwa katika kuinua sekta ya kilimo kwa kupitia wakulima wadogo na ukarabati wa maghali waliofanya umesaidia Mkoa wa Katavi kuongeza vituo zaidi vya kununulia mazao.