ELIMU YA AWALI MSINGI WA ELIMU


Picha na mtandao

Na Irene Temu
Katavi

Elimu ya awali (chekechea) imeelezwa kuwa msingi wa ujifunzaji wa mwanafunzi  kabla ya kuanza elimu ya Msingi (darasa la kwanza hadi la saba) kwa kupata maarifa ya vitendo zaidi yanayorahisisha ujifunzaji pindi mwanafunzi anapoanza elimu ya msingi.

Sera ya elimu ya Mwaka 2014  imebainisha kuwa Elimu ya awali muda wake wa mafunzo ni mwaka mmoja na inawalenga watoto wenye umri wa miaka 3-5 kilingana na uelewa wa mtoto mwenyewe.

Sera ya elimu pia imebainisha  mafunzo hayo kotolewa pia kwa watoto wenye mahitaji maalum kwa sababu pindi watakapokuwa darasani ndipo Mwalimu atafahamu waanafunzi wenye uhitaji maalum.

Afisa Taaluma Mkoa wa Katavi Florence Ngua anasema kuwa Elimu ya awali inafundishwa ikiwa na malengo kadhaa.

Baadhi ya malengo hayo ni pamoja na kukuza maendeleo ya jumla ya mtoto kiakili,kimwili,jamii na kihisia pia kubaini watoto wenye mahitaji maalum na kuwapatia afua stahiki.

Aidha Afisa Taaluma Mkoa wa Katavi Ngua aliongeza pia Elimu ya awali inamjenga mtoto kimaadili,inakuza uwezo wa mtoto wa kudhamini, kudumisha,kujivunia utaifa wake na utamaduni wa jamii yake.

"Elimu ya awali inakuza stadi za awali za ujifunzaji wa mtoto na tabia ya kupenda kujifunza,kujenga uwezo wa mtoto kujiamini,kujitambua,kujithamini na kuthamini wengine sambamba na kumfundisha mtoto kutunza mazingira na rasilimali zilizopo,kukuza stadi za ubunifu na kufikiria kimkakati na kumuandaa mtoto kujiunga na Elimu ya Msingi"alisisitiza Ngua

Ngua alisema pia Elimu ya awali inatumia zaidi vitendo hususani kuimba na kucheza pindi mtoto anapojifunza kwa njia ya vitendo anaelewa zaidi na ndio maana Elimu ya awali inahitai ubunifu katika ufundishaji kutumia Ishara zaidi na michoro mingi ya picha.

Sambamba na ufundishaji wa vitendo zaidi kwa watoto wa umri wa miaka 3 hadi miaka 5 mtaala wa Elimu ya awali unalenga kukuza umahiri wa kuhusiana,kuwasiliana,kutunza afya,kutunza mazingira,kumudu stadi za kisanii na kutunza dhana za kihisabati.

Ambapo dhana hizo za kihisabati ni KKK 3,Kusoma,Kuandikia na Kuhesabu na ndio msingi mkubwa wa darasa la kwanza hadi la tatu mtoto anakuwa yatari ameshaelewa baada ya kujifunza kwa vitendo katika darasa la awali.

Nae Mwalimu Elias Makwaya wa Shule ya Mt. Kizito iliyopo eneo la  Kazima Manispaa ya Mpanda anaeleza kuwa mwanafunzi aliyepitia Elimu ya awali kwa Mwaka mmoja anautofauti na yule mwanafunzi aliyeanza darasa la kwanza bila kupitia Elimu ya awali katika ufundishaji.
"mwanafunzi aliyepitia Elimu ya awali anakuwa tayari ameshazoea mazingira ya shule na kuelewa pale Mwalimu anapokuwa akifundisha lakini kwa yule mwanafunzi anayeanza Elimu ya Msingi bila kupitia Elimu ya awali Mwalimu anakuwa na kazi mbili ya kumfundisha darasani na kumfundisha mazingira ya shule ili aweze kuendana nayo"alifafanua zaidi Mwalimu Elias.

Mwalimu Vumilia  Kisai anayefundisha Elimu ya awali katika kituo kilichopo eneo la Kazima  Manispaa ya Mpanda anasema kuwa mwanafunzi anayepitia Elimu ya awali anakuwa tayari na uelewa mzuri kwa kuwa Elimu ya awali inafundishwa kwa vitendo zaidi dhana inayomjenga kupokea Elimu ya Msingi bila shida yoyote.

Pia aliwaasa wazazi kuwapeleka watoto wao Elimu ya awali kabla ya kuwaandikisha Elimu ya Msingi kwani Elimu ya awali ndio Msingi wa mwanafunzi kujiunga Elimu ya Msingi

Search This Blog

CHAGUA HABARI

Pages