| Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi ACP Ali Makame Hamad akitoa Taarifa ya Matukio mbalimbali yaliyotokea ndani ya Mkoa wa Katavi mbele ya Waandishi wa Habari leo Mach 4,2022 |
Na Walter Mguluchuma
Katavi
Mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la Jeniviva Timotheo(29) Mkazi wa Kijiji cha Mtakuja Kata ya Nsekwa Tarafa ya Inyonga Wilaya ya Mlele Mkoa wa Katavi ameuawa kikatili kwa kuchinjwa na panga shingoni na mume wake aitwaye Anisent John(32) na baada na kumchinja nae akajinyonga juu ya dari na kuacha ujumbe wa maandishi .
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi ACP Ali Makame Hamad amewaambia Waandishi wa Habari kuwa mauwaji hayo ya kikatili na yakusikitisha ya mwanamke huyo yametokea Machi 2 majira ya saa tisa mchana huko nyumbani kwa wanandoa hao wawili waliokuwa wakiishi katika kijiji cha Mtakuja .
Alisema mtuhumiwa wa mauwaji hayo ambae ni marehemu kabla ya kutekeleza mauwaji hayo alivizia watoto wao wakiwa shuleni ndipo alipotekeleza mauaji hayo.
Ni kwamba kabla ya kufanya mauwaji hayo mtuhumiwa ambaye pia ni marehemu alifunga milango yote ya nyumba yake na kubaki ndani yeye na mke na ndipo alipomuuwa kikatili Mkewe huyo kwa kumchinja na panga shingoni pasipo watu kujua.
Kamanda All Makame Hamad ameeleza kuwa baada ya kutekeleza mauwaji hayo mtuhumiwa nae aliamua kujinyonga kwa kutumia chandarua kwa kujining'iniza kwenye kenchi ya dari ndani ya chumba alichofanyia mauwaji ya mke wake.
Amesema kuwa taarifa za vifo vya wanandoa hao viligundulika baada ya mtoto wao mmoja aliyekuwa ametoka shuleni kufika nyumbani na kukuta milango yote ya nyumba imefungwa licha ya kufanya jitihada za kufungua alishindwa na kulazimika kwenda kutoa taarifa kwa mjomba wake aliyekuwa akiishi jirani na walipofika eneo la tukio walivunja mlango na kukuta ndani miili ya Marehemu hao .
Majirani walifika nyumbani kwa marehemu hao baada ya kusikia kilio cha mtoto wa marehemu na kisha kutowa taarifa Kituo cha Polisi ambao walifika eneo hilo na walipoingia ndani kwenye chumba cha marehemu hao na walikuta ujumbe wa maandishi uliokuwa umeandikwa na Marehemu Anisent John usemao amejiuwa kwa hiari yake mwenyewe.
Kamanda Hamad amesema chanzo cha tukio hilo ni mgogoro baina yao wakifamilia unaohusishwa na wivu wa kimapenzi ambapo mke alikuwa akimtuhumu mumewe kuwa na wanawake wengine kijijini hapo .