Na Mwandishi wetu,
Wafugaji ndani ya Mkoa wa Katavi wametakiwa kuachana na ufugaji wa mazoea unaoambatana na kuswaga ng'ombe makundi kwa makundi badala yake wafanye ufugaji wenye tija utakao inua pato la nchi na mtu mmoja mmoja pia.
Hayo yameelezwa na Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Sekta ya Mifugo)Tixon Nzunda wakati akiweka jiwe la Msingi katika eneo la Ujenzi wa kiwanda cha Usindikaji wa Maziwa cha MSS-NSIMBO kilichopo Halmashauri ya Nsimbo Mkoa wa Katavi.
Na kuwataka wafugaji kutumia fursa hiyo ya kiwanda kwa kuuza maziwa ya ng'ombe wao watakao kuwa wamewafuga vizuri kwa kufuata ushauri wa Wataalam wa Mifugo unaowataka kufanya ufugaji wenye tija.
Akizungumza katika uwekaji wa jiwe hilo la Msingi katika eneo la Ujenzi wa kiwanda hicho cha Usindikaji wa Maziwa Afisa Mifugo Mkoa wa Katavi Zidihery Mhando amesema kuwa kiwanda hicho baada ya Ujenzi wake kukamilika kitakuwa mkombozi kwa wafugaji wa Mkoa wa Katavi kwani asilimia kubwa ya maziwa ya jioni yaliyokuwa yakipatikana yalikuyakimwaga kutoka na changamoto ya kukosekana kwa soko la maziwa.
| Afisa Mifugo Mkoa wa Katavi Zidihery Mhando |
"hivyo kukamilika kwa kiwanda hiki kutakuwa mwarobaini wa yale maziwa yote yaliyokuwa yakimwaga na wafugaji kwa kigezo cha kukosa soko kwa kuwa sasa wafugaji wataleta maziwa katika kiwanda hiki kwa ajili ya kuchakatwa"alifafanua Mhando
Pia katika uwekaji wa jiwe la Msingi katika eneo la Ujenzi wa kiwanda hicho cha Usindikaji wa Maziwa cha MSS-NSIMBO Katibu Mkuu Nzunda alimpongeza mwekezaji na Mkurugenzi wa kiwanda hicho Marick Salum kwa kutekeleza Mpango wa Serikali wa Mwaka 2020/2025 wa adhima ya Viwanda hususani katika sekta ya uzalishaji ya Mifugo na kuwa mwekezaji wa mwanzo katika sekta ya mziwa ndani ya Mkoa wa Katavi.
"tunaamini kwa mwanzo huu ambao tumeanza,sekta ya Mifugo na maziwa inaenda kukua na sisi Serikali kupitia Serikali ya Mkoa na Halmashauri tutakupa ushirikiano kuhakikisha unafanikiwa katika mradi wako mkubwa ambao naamini pia unakwenda kubadilisha mfumo wa ufugaji kwa wafugaji wetu na hususani wafugaji wa Mkoa wa Katavi"alibaisha Katibu Mkuu Nzunda
Aidha Katibu Mkuu Nzunda aliongeza kuwa wanataka kusikia kuwa Mkoa wa Katavi ni eneo litakalokuwa halina magonjwa hivyo amewaomba wadau wote waliopo ndani ya Mkoa wa Katavi ambao ni vyama vya wafugaji wakiwemo wafugaji wenyewe pamoja na Serikali ya Mkoa na Wilaya kuhakikisha wanashirikiana na mwekezaji ili kiwanda hicho kiweze kukamilika kwa haraka na kuanza kuzalisha sambamba na kuhakikisha malighafi inayopatikana ni salama.
Nae Mkurugenzi wa kiwanda hicho cha Usindikaji wa Maziwa cha MSS-NSIMBO Marick Salum aliupongeza Uongozi wa Serikali ya Mkoa wa Katavi kwa kupokea wazo lake la kuwekeza katika kiwanda cha maziwa na kumpa ushirikiano pamoja na Wataalam ambao ndio wasimamizi wa Ujenzi unaoendelea katika kiwanda hicho.