Na Walter MguIuchuma
Katavi
Ofisi ya Wakala wa barabara Mkoa wa Katavi TANROADS imepokea Jumla ya Tshs Bilioni 9.342 sawa na asilimia 58 ya Bajeti ya Matengenezo ya Barabara za Mkoa katika mwaka wa fedha unaoendelea wa 2021/2022.
Hayo yameelezwa na Meneja wa Tanroads Mkoa wa Katavi Mhandisi Martin Mwakabende wakati alipokuwa akitowa taarifa ya utendaji kazi wa Tanroads wakati wa kikao cha bodi ya barabara cha Mkoa wa Katavi kilichofanyika katika ukumbi wa maji.
Ameeleza kuwa katika mwaka wa fedha wa 2021/2022 Mkoa wa Katavi ulitengewa bajeti ya Tshs bilioni 15. 997 kwa ajili ya matengenezo na ukarabati wa Barabara kati ya fedha hizo mfuko wa Barabara ni Tshs bilioni 12.757 na fedha za maendeleo ni Tshs bilioni 3.240.
Amebainisha kuwa mapendekezo ya bajeti ya mwaka wa fedha wa 2022/2023 wamependekeza kiasi cha jumla ya Tshs bilioni 24.61 huku Tshs bilioni 15.708 zikiwa ni fedha kutoka mfuko wa barabara na Tshs bilioni 8.901 kutoka mfuko wa Maendeleo .
Mwakabende ameeleza kuwa kwa mwaka wa fedha unaoendelea Tanroads Mkoa wa Katavi wamesaini mikataba 28 na Wakandarasi mbalimbali na Miradi hiyo ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji ambapo kwa ujumla ipo hatua ya asilimia 39.
Amefafanua kuwa upembuzi yakinifu na usanifu wa kina barabara ya Mpanda Ugala Kaliua , Ulyankuru hadi Kahama yenye urefu wa km 457 mhandisi mshauri amewasilisha nyaraka za ufanifu kwa mwajiri ambae sasa anafanya mapitio ya mwisho na utekelezaji wake upo asilimia 85.
Utekelezaji wa Barabara ya Kagwira hadi Karema yenye urefu wa km 112 upembuzi yakinifu umefanywa na hatua ya utekelezaji imefikia asilimia 80.
Kuhusu Miradi ya Barabara za Kitaifa Mhandisi Mwakabende amesema kuwa serikali imetangaza zabuni za Ujenzi wa Barabara kwa kiwango cha lami katika Barabara za Kibaoni kuja Mpanda urefu wa km 50 na Vikonge kwenda Luhafe km 25 ambapo manunuzi ya miradi hiyo yote imekamilika na Maandalizi ya kusaini mikataba ipo katika hatua za mwisho .
Amezitaja baadhi ya changamoto za utekelezaji wa kazi ni utaratibu wa kupata msamaha wa kodi kwa Miradi ya Ujenzi inachukua muda mrefu sana hivyo kuchelewesha utekelezaji wa kazi za Matengenezo ya barabara .
Changamoto nyingine ni wananchi kufanya shughuli za kilimo ndani ya maeneo ya Uhifadhi wa barabara,uharibifu wa alama za Barabarani na kuchelewa kupatikana kwa GN pia kwenye maeneo ya Barabara zinako pita hifadhi kumekuwa na tatizo kwa Wakandarasi kutoruhusiwa kuchimba vifusi kwenye Hifadhi za Tanapa .
Mratibu wa Rarura wa Mkoa wa Katavi Inocent Mlay ameeleza kuwa Mkoa wa Katavi bado kuna shida ya Wakandarasi kwani Wakandarasi wengi waliopo hawana vifaa vya Ujenzi wa Barabara hali inayosababisha Wakandarasi wengi kutoka nje ya Mkoa na hasa wakati wa Matengenezo ya barabara za lami .
Mkuu wa Mkoa wa Katavi Mwanamvua Mrindoko amezitaka Tanroads na Tarura kuhakikisha barabara zote ambazo wanazisimamia zinapitika wakati wote licha ya kuwa bado mvua zinaendelea kuonyesha kwa kipindi hiki .
Amewaonya Wakandarasi ambao wamekuwa hawafanyi kazi zao vizuri kwa kutokuwepo katika maeneo yao ya kazi Bodi ya Barabara ya Mkoa haita sita kuwachukulia hatua na kupeleka mapendekezo kwenye mamla husika ili wafutiwe leseni zao za ukandarasi.