| Washiriki wa Kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa wa Katavi(RCC)wasikiliza kwa makini hutoba ya ufunguzi wa kikao hicho iliyotolewa na Mkuu wa Mkoa wa Katavi Mwanamvua Mrindoko |
Na Walter MguIuchuma
Katavi
Wazazi na walezi wa Mkoa wa Katavi wameagizwa kuhakikisha watoto waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka huu katika shule walizopangiwa na wale wanao anza darasa la kwanza na Awali waripoti shuleni bila kisingizio cha aina yoyote kabla ya msako mkali dhidi yao.
Agizo hilo limetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Katavi Mwanamvua Mrindoko wakati akifungua Kikao cha Kamati ya Ushauri cha Mkoa wa Katavi (RCC) kilichofanyika katika Ukumbi wa Idara ya Maji Manispaa ya Mpanda .
Alisema hakuna kisingizio chochote kitakachomzuia mwanafunzi kujiunga na kidato cha kwanza na darasa la kwanza na la Awali kwani Serikali ya Mkoa haija weka sharti lolote ambalo linamfanya mtoto ashindwe kwenda shule na ndio maana wameruhusu hata mwanafunzi asiye na sare za shule kupokelewe na kuanza masomo.
Aidha aliwaonya Wazazi na Walezi ambao bado watoto wao hawajaripoti shule watambue kuwa baada ya muda wa mwisho uliopangwa kupita Wazazi na Walezi wa watoto hao watakamatwa na kufikishwa Mahakamani ili hatua kali zichukuliwe dhidi yao .
Amebainisha kuwa kwa mara ya kwanza tangu kuanzishwa kwa Mkoa huu haijawahi kutokea Wanafunzi wote waliofaulu kidato cha kwanza kuingia darasani kwa wakati mmoja tofauti na ilivyokuwa awali wanafunzi kuanza kwa kwa awamu kutokana na upungufu wa madarasa lakini sasa hivi Mkoa wa Katavi hauna tena uhaba wa vyumba vya madarasa .
Hivyo amewataka Viongozi wa ngazi zote kuhakikisha wanapita nyumba kwa nyumba na mtaa kwa mtaa ,kitongoji kwa kitongoji na kila kijiji kuwasaka wanafunzi ambao watakuwa hawajaripoti shuleni .
Amefafanua kuwa hadi kufikia Januari 23 Idadi ya wanafunzi waliojiunga na kidato cha kwanza walikuwa ni 9,581 ambao ni sawa na asilimia 79.9 ambapo kwa siku ya kwanza wanafunzi walioripoti walikuwa ni asilimia nane.
Mkuu wa Mkoa Mwanamvua alisema kwa wanafunzi walioanza masomo ya darasa la kwanza Mkoa huu umefanikiwa kuvuka lengo kwani Idadi ya wanafunzi walionza masomo ya darasa la kwanza ni 34,932 sawa na asilimia 117.
Pia ametumia nafasi hiyo kuwataka Wakurugenzi wote wa Halmashauri za Mkoa wa Katavi kuhakikisha fedha zote walizokusanya kwenye mapato ya ndani ya kila Halmashauri na hazija rejeshwe kwenye mfumo ndani ya siku saba fedha hizo ziwe zimengizwa kwenye Mfumo kwa watakao shindwa kuteleleza watawajibishwa .
Aidha amesisitiza fedha zote za asilimia kumi za mapato ya ndani zilizotolewa kwa ajili ya mikopo kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu wahakikishe zinarejeshwa na vikundi vingine viweze navyo kunufaika na mikopo hiyo .
Kwa upande mwingine Mbunge wa Jimbo la Katavi Mhandisi Isack Kamwelwe alikiambia kikao hicho kuwa Mkoa wa Katavi umekuwa ukikabiliwa na tetemeko la ardhi mara kwa mara hali ambayo imekuwa ikileta hofu na taharuki kubwa kwa wananchi .
Hivyo alitaka kujua kwa kuwa tatizo hilo limekuwa la mara kwa mara wananchi wa Mkoa huu wamefanyiwa utaratibu wa aina gani wa kuweza kujihadhari na tetemeko la ardhi pindi linapo kuwa limetokea.
Mkuu wa Wilaya ya Tanganyika ambae pia ni Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Mpanda Onesmo Buswelu alikiri ni kweli kumekuwa na matetemeko ya mara kwa mara na kwa mwezi huu yametokea matetemeko ya ardhi matatu.
Alieleza kuwa wamekuwa wakifanya mawasiliano na Wataalam wa Miamba ya ardhini pindi tetemeko linapotokea na kutoa ushauri ambao wanakuwa wamepewa kutoka kwa Wataalam hao kwa wananchi pamoja na elimu.