| Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi ACP Ali Makame Hamad |
Na Walter MguIuchuma
Katavi
Watu wawili wakazi wa Vijiji vya Nkungwi na Sentamaria Wilaya ya Tanganyika Mkoa wa Katavi wanashikiliwa na Jeshi la Polisi akiwemo mume wa marehemu Dutu Maige na Yusuph Sita kwa tuhuma za kumuuwa Mariamu Paschal(36) na mtoto wake Editha Dutu(04) kisha kuwafukia kwenye shimo kufuatia ugomvi wa kugombania gunia sitini za mpunga .
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi All Makame Hamad watuhumiwa hao wamekamatwa Machi9,2022 kufuatia Upelelezi uliofanywa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Katavi
Amebainisha kuwa Jeshi hilo lilipokea taarifa kutoka kwa Paschal Masheku mkazi wa kijiji cha Sentamaria ambae ni Baba mzazi wa Marehemu Mariamu kuwa mtoto wake aitwaye Mariamu Paschal na Mjukuu wake Editha Dutu wametoweka katika mazingira ya kutatanisha tangu Julai 2021 .
Baada ya Jeshi la Polisi kupokea taarifa hizo Upelelezi wa kina ulianza mara moja na ndipo tarehe 9 March watuhumiwa hao wawili ambao ni Dutu Maige na Yusup Sita walikamatwa kuhusiana na mauaji hayo .
Kamanda All Makame Hamad ameeleza kuwa baada ya watuhumiwa hao kukamatwa na kufanyiwa mahojiano wote wawili kwa pamoja walikiri kumuuwa Mariamu Paschal na mtoto wake Editha Dutu na kisha miili yao kuifukia katika shimo kwenye pori la Kalilankulunkulu lililopo kwenye mashamba ya Magereza Wilaya ya Tanganyika.
Baada ya kukiri kutenda mauaji hayo ndipo March 12 mwaka huu watuhumiwa hao wote wawili waliwaongoza Askari wa Jeshi la Polisi kuonyesha mahali ilipo miili hiyo ya marehemu hao .
Baada ya kufukua kwenye shimo hilo yalipatikana mabaki ya miili ya marehemu hao ya sehemu ya mbavu na kichwa .
Kamanda Hamad ameeleza kuwa chanzo cha tukio hilo ni ugomvi wa kifamilia kati ya mtuhumiwa Dutu Maige na aliyekuwa mkewe Mariamu Paschal waliokuwa wakidaiana gunia sitini za mpunga .
Upelelezi wa tukio hili bado unaendelea na mara utakapokamilika watuhumiwa hao wote watafikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazo wakabili .