| Hali halisi inavyoonekana katika Vijiji vya Kapalamsenga na Songambele Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika Mkoa wa Katavi baada ya mvua kunyesha March 13 na 14,2022 |
Nyumba zaidi ya 30 za vijiji vya Songambele na Kapalamsenga Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika Mkoa wa Katavi zimebomoka baada ya kujaa maji yaliyosababishwa na mvua zinazoendelea kunyesha katika Mkoa huo.
Mvua kubwa iliyonyesha usiku wa March13, kuamkia March14,2022 kwa muda mrefu ilisababisha nyumba hizo kujaa Maji na kupelekea kubomoka na kuwaacha wakazi wa vijiji hivyo wakiwa hawana makazi huku uharibifu mkubwa wa mazao mbalimbali mashambani ukitokea.
Diwani wa Kata ya Kapalamsenga Wilaya ya Tanganyika,Jefu Lameck ameeleza kuwa mvua hiyo ilianza kunyesha saa 4 hadi 7 usiku na saa 3 asubuhi hapo March14,2022 nakusababisha uharibifu mkubwa wa makazi ya watu na mazao.
Ameelezea pia nyumba zaidi ya 14 katika kijiji cha Kapalamsenga na zaidi ya nyumba 16 katika Kijiji cha songambele zimebomolewa na nyingine kuingiliwa na maji.
"....inasikitisha sana watu wamekosa makazi hawana pakwenda kujihifadhi…mbaya zaidi mazao yao kama vile mpunga,mahindi,pamba,ufuta na alizeti yameharibiwa kiasi kwamba kuna hatari ya wimbi la njaa kuweza kutokea mahali hapa” alisisitiza Diwani huyo.
| Wakazi wa Kijiji cha Kapalamsenga |
Aliongeza Diwani Lameck “hasara hii haielezeki kwa sababu ya hali mbaya waliyonayo wananchi wetu,vyakula vimesombwa na maji pia hawajui watakula nini wao na watoto wao jambo ambalo linahitaji utatuzi wa haraka”.
Katika kuhakikisha hatua zinachukuliwa za kuwaokoa wananchi hao Diwani aliiomba serikali kutoa msaada wa haraka wa chakula na kutafuta maeneo mengine ya kuwahifadhi.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Kapalamsenga Paul Mpaga aliiambia UHURU kuwa wananchi hasa wakulima wamepata hasara kutokana na kukopeshwa mbengu za Alizeti na Kampuni ya Nondo Investment iliyopo Manispaa ya Mpanda ambapo walitarajia kuvuna kwa tija zao hilo na kuweza kulipa deni la mbengu hizo.
Mpaga alisema wananchi msimu huu wa kilimo wamejitokeza kwa wingi kulima zao la Alzeti baada ya kupata elimu kutoka kwa serikali na wadau wa kilimo ambapo uharibifu uliosababishwa na mvua umekuwa kikwazo cha kupiga hatua za kimaendeleo huku wakiwa hawajui ni namna gani watalipa deni hilo.
Naye Mkazi wa kijiji hicho,Anastazia Kitatange alielezea masikitiko yake juu ya uharibufu uliotokea huku akiomba serikali kutoa msaada wa haraka wa chakula na makazi pamoja na kuiomba kampuni ya Nondo Investment kutoa msamaha wa deni la mbengu.
Anastazia alisema licha ya kuwa na imani na serikali ya Wilaya na Mkoa kuwa zitachukua hatua za haraka kunusuru hali zao mbaya pia ameiomba Serikali kuchukua hatua mahususi za kuzuia magonjwa ya mlipuko ambayo yanaweza kutokea.