![]() |
| Kamishna Msaidizi wa Jeshi la Zima moto na Uokoaji Mkoa wa Katavi,Regina Kaombwe |
Na George Mwigulu,Katavi.
Kukosekana kwa vifaa vya uokoleaji na kuzimia moto ni chanzo cha Jeshi la Zima Moto na Uokoaji Mkoa wa Katavi kushindwa kukabiliana na majanga mbalimbali yanayotokea katika Mkoa.
Kamishna Msaidizi wa Jeshi la Zima Moto na Uokoaji Mkoa wa Katavi,Regina Kaombwe akizungumza jana ofisini kwake alieleza kuwa juhudi zinahitajika kuimarisha miundombinu ya Jeshi hilo Mkoa wa Katavi.
Kaombwe aliweka wazi kuwa Mkoa wa Katavi kwa sasa una gari moja pekee la zima moto pamoja na kutokuwa na vifaa vya uokozi hali inayokwamisha uwajibikaji wa Jeshi hilo kwenye kazi zake.
“...kuhusiana na vitendea kazi tuna gari moja tu mkoa mzima na gari hilo linaujazo wa maji lita 1500 ndugu mwandishi fikiria gari lina lita 1500,nyumba inaungua hata nyumbani kwako lita 1500 utazitumiaje ni ndogo ndogo mno” alisema Kamishna huyo.
Aliongeza“kupatikana kwa vitendea kazi kunasaidia Jeshi la Zima moto na Uokoaji kuwajibika zaidi na kwa ufanisi mkubwa na uhaba mkubwa wa vifaa vya kuzimia moto na uokozi ni changamoto mojawapo inayokwamisha utendaji kazi wetu......na naamini sasa serikali itaanza kufuatilia au kutatua changamoto hiyo kwa wakati…”
Hivyo alisema kutokana na hali hiyo ambayo haiendani na hali halisi ya ukubwa wa kijiografia ya Mkoa wa Katavi huku kukichagizwa na ukuwaji wa maendeleo ya Mkoa wa Katavi kwa sasa wanatumia gari la Zima moto la Kituo cha Uwanja wa ndege licha ya kuwa gari hilo linasheria kali.
Kamishina Msaidizi wa Jeshi hilo Kaombwe alisema kuwa utoaji wa elimu kwa wananchi kumeleta matokeo chanya kwa Mkoa wa Katavi kuwa na matukio machache zaidi ya moto kuliko ya Uokoaji ambapo kuanzi Mwenzi wa 10,2021 hadi leo ni matukio matano ya moto huku matukio ya uokozi yakiwa thelathini na mbili.
Aidha katika sekta ya madini Jeshi hilo limekuwa na utaratibu wa kutoa mafunzo ya uokozi kwa wachimbaji kama njia ya kuchukua tahadhari endapo majanga kama ardhi kutitia wakiwa kwenye shughuli za uchimbaji waweza kujiokoa na kuokoa wenzao.
Alitoa Rai kwa wazazi na walezi kuwa na utamaduni wa kufuatilia mienedo ya watoto wao hususani wakati huu wa mvua za masika kwani baadhi ya watoto huenda kucheza kwenye madimbwi ya maji na kuhatarisha maisha yao.
